Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Tumepata nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili tuwezw kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ACHA MARA MOJA…
Rafiki, akili na mwili wako vina uwezo mkubwa sana, lakini umekuwa hutumii uwezo huo,
Badala yake umekuwa unaudekeza mwili na kuendekeza akili yako, kitu ambacho kinakuzuia kufanikiwa.

Chukua mfano kwenye tabia ulizonazo ambazo ni kikwazo kwa mafanikio yako.
Kwa kuwa tayari ni tabia, basi unajiambia huwezi kuacha mara moja, u ajiambia utaacha kidogo kidogo.
Sasa kwenye mafanikio, hakuna kitu kama kuacha kidogo kidogo.
Ni labda unaacha au unafanya, kidogo kidogo haina nafasi.

Hivyo ninachotaka utafakari asubuhi hii, ni namna ya kuacha mara moja chochote unachofanya ambacho hakichangii mafanikio yako.
Najua unavijua vingi sana unavyofanya sasa, ambavyo mchango wake kwenye mafanikio yako ni sifuri. Lakini unajiambia huwezi kuacha mara moja, utaacha kidogo kidogo.

Acha mara moja, amua leo sitafanya tena na usifanye kweli.
Tena acha kwa mbwembwe, acha kwa maneno makali kwamba hutafanya tena na endelea na maisha yako.
Kwa mfano kama umekuwa mtumiaji wa vilevi na unajiambia huwezi kuacha, chukua kile kilevi ambacho umekuwa unatumia sasa na kiharibu ukisema hutakitumia tena. Kama ni bia shika chupa yake na ipasue (ikiwa na bia) na jiambie hutatumia tena kilevi hicho.

Kadhalika kama tabia inayokuzuia ni mitandao ya kijamii, ingia kwenye mitandao hiyo na tangaza kuanzia sasa hutakuwa tena kwenye mitandao hiyo, kisha futa kabisa hapo hapo bila ya kuwa na subira.

Chochote ambacho hakichangii kukufikisha kwenye mafanikio yako, basi kinakuzuia usiyafikie.
Chochote ambacho siyo muhimu kabisa kwako kukifanya ili ufanikiwe, basi ni kikwazo kwako kama utakifanya.

Muda ni mchache, nguvu zinaisha haraka, tumia muda na nguvu zako kwa yale yanayochangia kwenye mafanikio yako.
Mengine yote ACHA MARA MOJA.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kutafakari kila unachofanya na kama kuna kisichokuwa na mchango kwenye mafanikio yakom unakiacha mara moja.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha