Hongera sana rafiki yangu kwa juma hili la 49 ambalo tumekuwa nalo kwa mwaka huu 2018. Najua ni juma ambalo limekuwa la mafanikio makubwa sana kwako. Kama umekuwa unaiishi misingi ambayo nakushirikisha kila siku kwenye makala mbalimbali, basi juma hili litakuwa limeleta vitu vipya kwako.
Tunakwenda kulimaliza juma letu bora, na kujiandaa na juma jingine linalokwenda kuanza. Hivyo tupate tano za juma, mambo matano muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi ili maisha yetu yaweze kuwa bora sana.
Karibu sana kwenye tano za juma la 49, nimekuandalia mambo mazuri sana kuhusu mafanikio na fedha, mambo ambayo ukiyafanyia kazi, hutabaki pale ulipo sasa.
#1 KITABU NILICHOSOMA; JINSI YA KUVUTA CHOCHOTE UNACHOTAKA.
Moja ya vitabu nilivyosoma juma hili ni kitabu kinachoitwa THE ATTRACTOR FACTOR, Hatua tano rahisi za kutengeneza utajiri au chochote unachotaka kwa kuanzia ndani yako. Kitabu hiki kimeandikwa na Joe Vitale.
Kitabu hiki kimeandikwa kwenye msingi wa sheria kuu ya mafanikio, sheria ya mvutano (LAW OF ATTRACTION). Sheria ya mvutano inasema kwamba chochote kinachotokea kwenye maisha hakiji kama ajali, badala yake kimevutwa.
Hii ina maana kwamba, chochote ambacho kimewahi kutokea kwenye maisha yako na kila kitakachoendelea kutokea, hakiji kama ajali au bahati mbaya, bali ni wewe mwenyewe umevutia hicho kilichotokea. Wewe ndiye umekikaribisha na kukiruhusu kitokee.
Ni kanuni ngumu kuelewa kama utaifikiria kwa hali ya ubinadamu, lakini unapoifikiria kiroho, ndipo unapoona nguvu yake. Kwamba hakuna chochote kinachotokea tu, kila kitu kinatengenezwa na kuvutiwa.
Umekuwa unavutia vitu kwenye maisha yako kupitia fikra ambazo zinatawala akili yako. Nilishakushirikisha sehemu zetu mbili za akili, akili inayofikiri (conscious mind) na akili inayotekeleza (subconscious mind). Mawazo yoyote ambayo yanakaa kwenye akili yako inayofikiri, ndiyo yanayotekelezwa na akili isiyo fikiri.
Hivyo kama utatumia muda mwingi kufikiria unatokaje kwenye umasikini, basi unajikuta unavutia umasikini uendelee kubaki kwako. Kama utatumia muda mwingi kufikiria unakwepaje ajali, basi unavutia ajali. Kwa kifupi, unapaswa kufikiria kile unachotaka na siyo usichotaka. Maana akili isiyofikiri haijui kutofautisha hasi na chanya, yenyewe inatekeleza kile ambacho umekibeba kwa muda mrefu.
Nafikiri sasa unaanza kuelewa ni kwa namna gani kila kinachotokea kwenye maisha yako unakuwa umekivutia mwenyewe, hata kama ulikuwa hukitaki. Kitendo tu cha mawazo kuwa ndani yako kwa muda mrefu, kinatosha kuvutia kitu hicho.
Kwa kutumia kanuni hii, kitu cha kwanza tunachopaswa kukilinda sana ni mawazo na fikra zetu, mara zote tuwe tunafikiria kile tunachotaka tu na siyo tusichotaka. Kwa kufikiria unachotaka, akili isiyofikiri inakuandalia mazingira ya kukipata.
Na hili ndiyo Joe anatushirikisha kwenye kitabu hiki cha THE ATTRACTOR FACTOR.
Kwenye kitabu hiki, Joe ametushirikisha hatua kuu tano za kuvutia chochote unachotaka kwenye maisha yako, iwe ni fedha, mali, mwenza, kazi, biashara, chochote unachoweza kufikiria basi jua unaweza kukivutia kwenye maisha yako.
Na hatua zenyewe ni hizi;
Hatua ya kwanza; JUA USICHOTAKA NA KITUKIE KUPATA UNACHOTAKA.
Hatua ya kwanza kwenye kuvutia chochote unachotaka ni kuanza ni kile usichotaka. Kama tulivyoona kama unafikiria kile usichotaka kwa muda mrefu, ndiyo kitakachotokea kwenye maisha yako. Kama upo kwenye madeni na unajiuliza utaondokaje kwenye madeni, kitendo tu cha neno deni kuwa kwenye fikra zako, kinavutia madeni zaidi.
Hivyo hatua ya kwanza ni kujua kipi usichotaka, kisha kukibadili kuwa kile unachotaka. Hatua ya kwanza ni kuondoka upande hasi wa kutaka na kwenda upande chanya.
Kwa mfano kama upo kwenye madeni na unataka kutoka kwenye madeni, badala ya kufikiria unaondokaje kwenye madeni, unafikiria utapataje fedha zaidi ili kufikia uhuru wa kifedha. Kwa kuondoa deni kwenye fikra zako, unaondokana kabisa na madeni.
Hatua ya kwanza ya kuvutia chochote ni kutokukiri chochote hasi, kukaa upande chanya na kuyajaza mawazo yako kwa fikra chanya za kule unakotaka kufika. Hata kama upo kwenye umasikini mkubwa, usikiri umasikini, usifikirie chochote kuhusu umasikini, badala yake kiri utajiri na fikiria kuhusu utajiri.
Kama unataka kupata mwenza bora, usiseme nataka mtu ambaye hana tabia fulani, utaishia kumpata mwenye tabia hizo, badala yake sema zile tabia ambazo unazitaka kwa mwenza wako.
Kwenye hatua ya kwanza unabadili kabisa fikra zako na hata maongezi yako na watu wengine, usikiri chochote hasi kwa wengine na ili kujilinda na mawazo hayo hasi, unapaswa kuwaepuka wale ambao muda wote wanakiri vitu hasi, maana hao wataharibu hatua zako tano za kuvutia unachotaka.
Hatua ya pili; THUBUTU KITU KIKUBWA.
Hatua ya pili ya kupata chochote unachotaka ni kuthubutu kutaka na hata kufanya vitu vikubwa. Usijiwekee ukomo wowote kwenye maisha yako. Sisi binadamu tunao uwezo mkubwa sana ndani yetu, uwezo ambao hakuna anayeweza kuutumia wote. Lakini tumefundishwa kujiwekea ukomo, kujiambia hiki hatuwezi au hakiwezekani.
Ondokana kabisa na ukomo huo na thubutu kuweka malengo na mipango mikubwa na kuifanyia kazi. Jiambie utakuwa bilionea au hata trilionea, hakuna wa kukuzuia.
Unapaswa kuwa na nia thabiti, nia isiyovunjika, nia ya kupata kitu kikubwa ambacho hujawahi kupata na pia hakijazoeleka.
Jua ni nini unachotaka kwenye maisha yako, fanya maamuzi, chagua kisha jiwekee tamko la kupata kile unachotaka.
Vunja mazoea, kwa sababu wengine wamejaribu wakashindwa, usibebe hilo kwamba haiwezekani, kwa sababu hakuna ambaye amewahi kufanya haimaanishi kwamba hakiwezi kufanyia. Wewe jua nini unataka, fanya maamuzi ya kukipata kisha tamka hilo kama kitu utakachofanyia kazi na usikubali yeyote akuyumbishe.
Unapasa kujijengea imani inayounga mkono kile unachotaka kwenye maisha yako, imani isiyoyumbishwa na isiyokuwa kikwazo kwa kile unachotaka. Wengi wamekuwa wanajiambia wanataka makubwa, lakini ndani yao hawaamini kwenye makubwa. Hivyo nje wanasema wanataka makubwa, wakati imani zao zipo kinyume, na zinawazuia kupata hayo makubwa.
Unapaswa kuamini, bila ya kuwa na shaka kwamba kile unachotaka utakipata na hakuna cha kukuzuia. Bila ya kiwango hiki cha imani, utaishia kuwa mpangaji na msemaji, lakini hutapata kile unachotaka.
Hatua ya tatu; SIRI INAYOKOSEKANA.
Baada ya kuwa umeondokana na mawazo hasi, na kuthubutu kufanya makubwa, kuna kikwazo kimoja ambacho kinaweza kukuzuia hata kama umeshajua nini unataka na unakubaliana nacho.
Kila mmoja wetu ana imani fulani ambazo zimejengeka ndani yake tangu akiwa mtoto, imani ambazo zinakinzana na kile unachotaka. Imani hizi siyo rahisi kuzigundua wewe mwenyewe, kwa sababu mara nyingi unakuwa umejifunza kuzificha. Kwa mfano mtu ambaye akiwa mtoto alikuwa anaona wazazi wake wakisumbuka na fedha, anakua na imani kwamba fedha ni ngumu na hazipatikani kwa urahisi, hivyo maisha yake yatavutia hilo kila wakati.
Kwenye hatua ya tatu, unapaswa kuwa na kocha ambaye anaweza kukusaidia kuondokana na imani zilizojengeka ndani yako.
Na hii ni hatua muhimu sana kwa sababu wengi huipuuza, kwa kujiamini kwamba hawana imani zinazowazuia, lakini ukweli ni kwamba kila mtu, ndiyo kila mtu ana imani fulani zilizojificha ndani yake, ambazo zinamzuia asifanikiwe.
Unapaswa kuwa na kocha ambaye anaweza kukuangalia kwa ukweli bila ya hisia na kuona yale makosa unayofanya kutokana na imani ulizonazo ndani yako. Pia lazima uwe tayari kufungua imani hizo na kuziondoa ili uweze kupata unachotaka.
Maisha yako ni kama timu ya mpira, ili timu ishinde, lazima wachezaji wote waamini kwenye ushindi na washirikiane kupata ushindi. Kama mchezaji mmoja hataamini kwenye ushindi, atawaangusha wachezaji wengine wote. Kadhalika kwenye maisha yako, kama kuna eneo ambalo una imani isiyo ya mafanikio, hata kama ni ndogo kiasi gani, itakuzuia usifanikiwe.
Kila tatizo au changamoto unazokutana nazo kwenye maisha yako, linaanzia ndani yako, kwa zile imani ambazo umejijengea ndani yako. Kama ukiweza kuzijua na kuzifanyia kazi imani hizo, utaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako.
Hatua ya nne; WEKA HISIA KWENYE MALENGO YAKO.
Hatua ya nne ya kuvutia chochote unachotaka, ni kuweka hisia kwenye malengo yako. Baada ya kuweka malengo na mipango ya kile unachotaka, unapaswa kuwa na taswira ya kile ambacho unataka, kama tayari umeshakipata, kisha jisikie kama tayari una kitu kile. Yaani pata hisia kama tayari umeshapata kile ambacho unakitaka. Na hii itakuwa na nguvu kubwa sana ndani yako.
Unapoyapa hisia malengo yako, akili yako ya ndani haiwezi kutofautisha kama unayo au huna, inachojua ni kitu ambacho tayari unacho na hivyo inakutengenezea mazingira ya kuendelea kuwa na kitu hicho.
Hii ni hatua muhimu mno kwenye hatua hizi tano, kwa sababu wengi huwa wanapuuza kwa kuona ni jambo lisilo na umuhimu, lakini wanajikosesha wenyewe kupata wanachotaka.
Kwa chochote unachotaka, jione kama tayari umeshakipata, yaendeshe maisha yako kama tayari umeshapata kitu hicho na akili yako itayavuta mazingira yanayoendana na kitu hicho.
Na hili halimaanishi kuiga maisha, kama wengi wanavyofanya, badala yake linahusisha kujenga imani kubwa ndani yako kwamba tayari una kile unachotaka, na imani hiyo ndiyo inakileta kwako.
Fanya haya yote ukiwa na imani na usijiwekee shaka kwenye lolote, na hakuna kitakachokuzuia usipate unachotaka.
Hatua ya tano; SIRI ILIYO KUU.
Hatua ya tano ya kuvutia chochote unachotaka Joe anaiita ni siri iliyo kuu, siri ya kupata chochote unachotaka. Siri hiyo ni kuachilia.
Baada ya kuchagua nini unachotaka, baada ya kuondokana na imani kinzani na baada ya kuweka hisia kama vile tayari umeshakipata, unapaswa kuachilia. Unapaswa kusahau kama vile unakitaka au hujakipata. Unapaswa kuipa dunia na asili nafasi ya kuleta kitu hicho kwako.
Usijiwekee ukomo wowote, usijiambie lazima nikipate leo au kesho, na wala usijiambie maisha yako hayawezi kwenda mpaka upate kitu hicho. Badala yake kiachilie, wewe endelea kuishi maisha yako, endelea kuchukua hatua na endelea kuamini kwamba umeshapata unachotaka.
Na siku moja, ukiwa hata hutegemei utakutana na kile unachotaka. Au kuna fursa itakayojitokeza ambayo itakuwezesha kupata unachotaka.
Ukiwa mtu wa kung’ang’ana, ukiwa mtu wa kusema lazima upate sasa la sivyo maisha hayataenda, utafukuza kabisa kile unachotaka kisije kwako.
Kuwa na imani kwamba dunia inafanyia kazi hitaji lako, na usiwe na wasiwasi kwamba hutakipata. Wewe endelea na maisha na endelea kuamini, endelea kuweka juhudi na siku itafika ambapo utapata kile unachotaka.
Rafiki, hizo ndizo hatua tano za kuweza kuvutia chochote unachotaka kwenye maisha yako, tumia hatua hizi kwenye maisha yako na utaweza kupata chochote unachotaka.
Nguvu ya kupata chochote unachotaka tayari ipo ndani yako, ni kuitambua na kuanza kuitumia. Yeyote asikuambie na wala usikubaliane na yeyote kwamba kuna vitu huwezi au haviwezekani, usiwasikilize watu wa aina hiyo. Badala yake jisikilize mwenyewe, sikiliza roho yako na ina vitu vingi sana kwa ajili yako.
#2 MAKALA YA WIKI; HATUA 7 ZA KUTENGENEZA MTAZAMO WA MAFANIKIO.
Rafiki, mtazamo ambao tunao kwenye maisha, ndiyo unaoamua kila kitu kwenye maisha yetu. Kama tuna mtazamo chanya, mtazamo wa kuwezekana, tutaweza kufanya makubwa na hata kufanikiwa sana.
Lakini kama tuna mtazamo hasi, mtazamo wa haiwezekani, hatutaweza kupiga hatua yoyote kwenye maisha yetu.
Juma hili nilikuandalia makala ya hatua saba za kutengeneza mtazamo wa mafanikio kwenye maisha yako. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hii isome hapa; Hatua Saba (07) Za Kutengeneza Mtazamo Bora Wa Kimaisha Na Kuongeza Kipato Chako.
Pia endelea kutembelea www.amkamtanzania.com kila siku kupata makala mpya. Pia nimekuwa natuma makala za DAKIKA MOJA kila siku kwenye email, kama hujapokea email hizi jiandikishe sasa kupitia kiungo hiki; www.amkamtanzania.com/jiunge
#3 TUONGEE PESA; JINSI YA KUVUTA FEDHA IJE KWAKO.
Kwa kutumia hatua tano za kuvutia chochote unachotaka, tulizojifunza hapo juu, unaweza kuvutia fedha kwenye zaidi kwenye maisha yako.
Hatua ya kwanza acha kufikiria yale usiyotaka kwa upande wa fedha. Usifikirie madeni, usifikirie umasikini, usifikirie kupata hasara. Badala yake fikiria kupata fedha zaidi.
Hatua ya pili thubutu kutaka kupata fedha nyingi zaidi, fikiria kupata mabilioni na matrilioni. Usifikirie kwamba hutaweza kwa sababu ni vigumu au kwa kuwa wengine hawajaweza kupata. Wewe jiwekee lengo kubwa zaidi.
Hatua ya tatu ondoa kila aina ya imani hasi uliyonayo ndani yako kuhusu fedha. Imani kwamba fedha ni mbaya na matajiri ni watu wabaya iondoe kabisa. Imani kwamba fedha ni ngumu na ili kuipata lazima uteseke ondokana nayo. Na imani kwamba ukipata fedha basi watu watakuchukia au watakuonea wivu unapaswa kuivunja. Ondokana na kila imani hasi uliyonayo kuhusu fedha, na hapa unahitaji kuwa na kocha wa kukusaidia.
Hatua ya nne jione tayari umeshapata fedha unazotaka, ona maisha yako kwa namna ambayo umeshapata mabilioni na matrilioni unayotaka. Ishi kama utakavyojisikia ukiwa na fedha hizo. Na hapa haimaanishi utapanye fedha ulizonazo sasa, lakini namna unavyofikiri, namna unavyofanya mambo yako iwe kama tayari umeshapata fedha unazotaka.
Hatua ya tano, achilia na amini dunia na asili vinafanyia kazi hitaji lako. Usiwe mtu wa kung’ang’ana kwamba lazima fedha hiyo uipate sasa, usijiwekee ukomo kwamba maisha yako hayawezi kwenda kama hujapata fedha hizo. Badala yake endelea na maisha yako kama tayari umeshapata fedha hizo na utashangaa kila mara fursa zitakuja kwako za kukufikisha kwenye kiwango hicho cha fedha. Na fursa zinapojitokeza, zifanyie kazi, usichelewe.
Tumia hatua hizo tano kuvutia fedha zaidi kwako.
#4 HUDUMA NINAZOTOA; SEMINA YA KUUANZA MWAKA 2019.
Rafiki, nimekuandalia semina bora kabisa ya kuuanza mwaka 2019, semina inaitwa TABIA ZA KITAJIRI.
Kwenye semina hii tutakwenda kujifunza tabia 10 za kuishi kila siku ili kuweza kutengeneza utajiri mkubwa kwenye maisha yetu.
Semina itaanza tarehe 03/01/2019 na kumalizika tarehe 13/01/2019. Semina itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap hivyo unaweza kushiriki ukiwa popote na bila kuacha chochote unachofanya sasa.
Kupata nafasi ya kushiriki semina hii unapaswa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA kwa kulipa ada ya uanachama ambayo ni tsh laki moja kwa mwaka.
Lakini pia kama huwezi kulipa ada au huna mpango wa kuwa mwanachama, unaweza kulipia tsh elfu 20 kwa ajili ya kushiriki semina hii tu.
Namba za kufanya malipo ni 0717 396 253 au 0755 953 887, mwisho wa kulipia ili kuweza kushiriki semina hii ni tarehe 02/01/2019.
Karibu sana rafiki, kama upo makini na maisha yako na unataka kufanikiwa, basi hii siyo semina ya kukosa.
Karibu pia ujiunge na kundi maalumu la semina hii, kwa kubonyeza kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/JvJBnoKixGrJZpZdw3shRv (kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA usijiunge na kundi hili).
Karibu sana ujifunze tabia kumi za kitajiri ambazo zitakuwezesha kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha yako.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KINACHOTOKEA SASA NI MATOKEO.
“Everything that is happening at this moment is a result of the choices you’ve made in the past.” – Deepak Chopra
Chochote kinachotokea kwenye maisha yako sasa ni matokeo ya maamuzi uliyofanya siku za nyuma. Hivyo kuhangaika na matokeo hakutayabadili maisha yako. Badala yake unapaswa kuhangaika na maamuzi unayofanya sasa, ili kesho uweze kupata matokeo bora.
Kama ulipanda mbegu ambayo hukuijua, ila ulidhani ni mchungwa, matunda yakaanza kutoka milimao, kuondoa matunda hayo hakutabadili ulichopanda. Ili kupata machungwa unapaswa kupanda mbegu ya mchungwa.
Matokeo unayopata sasa huwezi kuyabadili, bali unaweza kubadili matokeo ya kesho kwa maamuzi unayofanya leo. Jifunze kwa matokeo unayopata sasa ili uweze kufanya maamuzi bora na kesho upate matokeo mazuri.
Rafiki, hizi ndiyo tano za juma hili, tano ambazo nakusihi utenge muda wa kujifunza kwa umakini, kwa sababu kuna mambo mazito hapa, usiyoweza kuyaelewa juu juu. Pata muda wa kujifunza kwa utulivu, kisha panga hatua za kuchukua na chukua hatua hizo mara moja.
Nakutakia kila la kheri kwenye juma la 50 la mwaka huu 2018 tunalokwenda kuanza, likawe juma bora sana kwako, juma la kuvutia makubwa kwenye maisha yako na kufanya maamuzi yatakayoleta matokeo bora ya baadaye.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu