Watu wananunua kwa watu wanaowajua, ndiyo maana hatua ya kwanza kwenye biashara yako ni kuhakikisha watu wanakujua, wateja wenye uhitaji wa kile unachouza wanajua upo na unacho wanachotaka. Hata uwe na kitu kizuri kiasi gani, kama watu hawajui uwepo wako huna biashara. Kujulikana ni muhimu na hapa ndipo unapopaswa kutangaza sana.

Watu wanaendelea kununua kwa watu wanaowapenda. Unaweza kutangaza sana na watu wakaja kununua, lakini wasinunue tena. Labda hawakupendezwa na huduma au hawakupata walichotaka. Hivyo hitaji la pili muhimu baada ya kutangaza, ni kuwapa wateja wako huduma bora sana kiasi kwamba watakupenda mno. Wape huduma bora itakayowafanya watake kuja kwako zaidi zaidi. Wateja wakikupenda, wanakuja kwako tena na tena.

Watu wanawaambia watu waende kununua kwenye biashara ambazo wanaziamini. Mteja anaweza kujua upo kwenye biashara, akaja kununua kwako, lakini asiwe tayari kuwaambia wengine waje kwako. Kama mtu hakuamini, itakuwa vigumu kwake kumleta mtu mwingine kwako. Mteja anaweza kuwa ananunua kwako, lakini kwa jinsi anavyokujua, anajua akiwaleta wengine kwako itaishia kuwa lawama kwake.

Hivyo basi, katika kuikuza biashara yako, nenda hatua kwa hatua, kwanza wateja wakujue, kwa kutangaza, kisha wape huduma bora sana wakupende, halafu endelea kuwapa huduma bora wakati wote kiasi cha kuweza kukuamini na kuwaambia wengine waje kwako.

Kuna ugumu wowote kwenye hilo rafiki?

Kama utaweka maamuzi, ukaweka kazi, ukajipa muda, hakuna kinachoshindikana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha