“Nothing is so exhausting as indecision, and nothing is so futile.” — Bertrand Russell
Siku mpya,
Siku bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine bora sana kwetu kwenda kuitumia siku hii kwa kufanya makubwa zaidi ya tulivyozoea.
Ianze siku hii kwa shukrani kwa sababu siyo wote walioiona.
Pia tumia kila dakika ya siku hii kwa uangalifu kwa sababu dakika ikishapotea hutaweza kuipata tena.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KINACHOKUCHOSHA ZAIDI…
Rafiki yangu, hakuna kitu kinachokuchosha kwenye maisha yako kama KUTOKUFANYA MAAMUZI.
Hakuna ubatili unaopitiliza kitendo cha kutokuwa na maamuzi.
Kwa sababu bila ya maamuzi, unajikuta unahangaika na kila kitu na hakuna matokeo makubwa utakayoweza kupata.
Kufanya maamuzi maana yake ni kuchagua nini utafanya kisha kuachana na vingine vyote.
Kufanya maamuzi ni kujua wapi unapeleka nguvu zako ili kuweza kupata matokeo bora.
Ukishafanya maamuzi, unayasimamia mpaka upate matokeo unayotaka.
Hujafanya maamuzi kama unejiambia utafanya biashara fulani, halafu baadaye watu wanakuambia biashara nyingine inalipa, unaacha ile uliyopanga mwanzo na kwenda kwenye hiyo inayolipa, wakati unaanza unaambiwa kuna fursa nyingine bora zaidi, unakimbilia hiyo tena.
Unajikuta umehangaika na kila kitu na hakuna ulichopata, umechoka sana na hakuna hatua uliyopiga.
Fanya maamuzi rafiki, na ukishafanya maamuzi, yasimamie, usitetereke, achana na kila aina ya kelele na nguvu zako zote peleka kwenye kutekeleza maamuzi hayo.
Ni bora ukosee lakini uwe na maamuzi kuliko kupatia lakini huna maamuzi.
Kufanyia kazi maamuzi uliyokosea lakini ukayasimamia, kutakuwa na manufaa kwako kuliko kuhangaika na vitu vingi ambavyo havitakupa manufaa yoyote.
Fanya maamuzi rafiki, kama utapanda au utashuka, kama utasuka au utanyoa, kisha achana na dunia ifanye yake na wewe fanya yako.
Unapokuwanna maamuzi thabiti ambayo unayasimamia, dunia nzima itakuwa ya msaada kwako kuhakikisha unapata unachotaka.
Lakini kama hueleweki nini unataka, leo uko na hiki, kesho uko na kile, unaichanganya hata dunia, isijue ikupe kipi.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kufanya maamuzi na kuyasimamia mpaka upate matokeo mazuri.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha