Rafiki yangu mpendwa,

Inapokuja swala la fedha na utajiri, imani ambayo mtu unayo ina nguvu kubwa kuliko kitu kingine chochote.

Utajiri unaanzia kwenye imani ambayo mtu unayo kuhusu wewe mwenyewe, kuhusu maisha na kuhusu fedha.

Kama mtu utakuwa na imani chanya kuhusu fedha basi utaweza kupata fedha na utajiri mkubwa.

Lakini kama utakuwa na imani potofu kuhusu fedha, utajizuia wewe mwenyewe kufikia utajiri.

Najua umewahi kuona hili, baadhi ya watu wanapata fedha nyingi kwenye maisha yao lakini wanaishia kuzipoteza zote. Siyo kwamba watu hawa ni wajinga na wazembe sana, wengi imani zao kuhusu fedha ndiyo zinawapelekea wapoteze fedha.

 

KWA NINI SIYO TAJIRI

Leo nimekuandalia imani saba potofu ambazo zinakuzuia kuwa tajiri na jinsi ya kuzivuka imani hizo ili uweze kupata fedha na utajiri kwenye maisha yako.

Karibu tujifunze na kuchukua hatua ili maisha yetu yaweze kuwa bora zaidi.

Imani ya kwanza; SISTAHILI KUPATA FEDHA NA UTAJIRI.

Imani potofu ya kwanza na inayowazuia watu wengi sana ni pale mtu anapojiona hastahili kupata fedha na utajiri. Hapa mtu anakuwa amekosa imani ndani yake kiasi kwamba haoni kama anaweza kufanya makubwa na maisha yake.

Kukosa huku imani ndani yake kunaweza kutokana na jamii inayomzunguka ambayo imekuwa inamkatisha tamaa au kukatokana na mambo aliyojaribu na akashindwa.

Ili kufikia utajiri, lazima kwanza ujiamini wewe mwenyewe, lazima uamini unastahili kupata utajiri na ndani yako upo uwezo mkubwa wa kufikia utajiri. Kwa kuanza na imani utaweza kuchukua hatua na kufanya makubwa.

Imani ya pili; MATAJIRI NI WATU WENYE ROHO MBAYA.

Angalia kwenye jamii unayoishi, sikiliza maneno ya watu wanaokuzunguka na utaona jinsi ambavyo watu matajiri wanaonekana ni wabaya na wenye roho mbaya. Watu masikini wanaamini wao wamekuwa masikini kwa sababu matajiri wachache wameshikilia fedha zote. Na wapo watu ambao wamekuwa wakifikiri kama fedha zote zitachukuliwa kwa matajiri na kugaiwa sawa kwa watu wote basi maisha ya kila mtu yatakuwa bora.

Rafiki, kuwachukia matajiri, kuwasema vibaya matajiri ni kikwazo cha kwanza kwako kuwa tajiri. Kwa sababu ukishaamini matajiri ni watu wabaya, basi utakazana usiwe tajiri ili na wewe usiwe mbaya.

Ondokana kabisa na imani hii kwamba matajiri ni watu wabaya, amini matajiri ni watu wazuri, watu wanaofanya jamii iende. Wapende matajiri, waseme vizuri na hilo litakupa wewe hamasa ya kuwa tajiri.

Imani ya tatu; HAKUNA MWINGINE KWENYE FAMILIA AMEWAHI KUFANYA AU KUWA TAJIRI.

Wapo watu wengi ambao wamenasa kwenye umasikini kwa sababu wazazi wao au ndugu zao nao ni masikini. Wakitaka kujaribu kitu kipya na kikubwa wanazuiwa na imani kwamba hakuna mtu mwingine kwenye familia yao amewahi kufanya kitu hicho.

Watu wengi wanabaki kwenye umasikini kwa sababu hawataki kuwazidi wazazi wao au ndugu zao. Wengine wanajisikia vibaya kufanya kile ambacho wazazi wao au ndugu zao wameshindwa.

Rafiki jua ya kwamba maisha yako ni tofauti kabisa na maisha ya mtu mwingine, jua kabisa ya kwamba kushindwa kwa wengine hakumaanishi kushindwa kwako. Na hakuna sheria yoyote inayosema hupaswi kuwazidi wazazi au ndugu zako, ishi maisha yako na utakuwa huru zaidi.

Imani ya nne; NIKIWA TAJIRI NITAWAPOTEZA WATU WA KARIBU KWANGU.

Imani nyingine inayowafanya wengi wanase kwenye umasikini ni ile imani kwamba mtu ukiwa tajiri utawapoteza watu wa karibu kwako, kama ndugu jamaa na marafiki. Hili ni kweli kwa sababu kadiri unavyopanda ngazi kuelekea kwenye utajiri, unajikuta hamna kitu kinachowaleta pamoja na wale uliozoeana nao.

Lakini unachopaswa kufahamu ni kwamba, kadiri unavyopanda ngazi, ndivyo unavyowavutia watu waliopo kwenye ngazi ya juu zaidi. Kwa sasa unazungukwa na wale uliozungukwa nao kwa sababu mpo ngazi sawa. Ukipanda ngazi ya juu kidogo, utajikuta unazungukwa na wengine ambao wapo ngazi ya juu. Hivyo usiogope kwamba utawapoteza watu wa karibu kwako, jua utawavutia wengine ambao mpo ngazi sawa ya kimafanikio.

Imani ya tano; FEDHA HAINUNUI FURAHA AU MATAJIRI HAWANA RAHA.

Imani hii imejichimbia mizizi kwa wengi, kwa kuamini kwamba fedha haiwezi kununua furaha, fedha siyo kila kitu na matajiri wengi hawana furaha. Ukweli pekee ni kwamba fedha siyo kila kitu, lakini inafanya kila kitu kiwe bora zaidi. Na siyo kweli kwamba fedha hainunui furaha, wengi hawajui namna ya kununua furaha. Na kama kuna mtu anaonekana ni tajiri lakini hana furaha, basi huyo siyo tajiri.

Ondokana na imani hii rafiki kwa kuacha kubeba hilo kwamba fedha hainunui furaha, hata kama ni kweli, je umasikini unanunua furaha. Wanasema ni bora kukosa furaha lakini una fedha, kuliko kukosa furaha na huku huna fedha, ni mzigo mara mbili. Pia usimsemee yeyote, kama kuna tajiri unamwona hana furaha, usijiambie na wewe ukiwa tajiri hutakuwa na furaha, maisha yetu yanatofautiana.

Imani ya sita; MATAJIRI HAWATAUONA UFALME WA MBINGUNI.

Hii ni imani ambayo imejengeka kwa wengi kutokana na tafsiri potofu ya baadhi ya maandiko ya kidini. Watu wengi kupitia dini wamekuwa wanaamini umasikini ndiyo tiketi ya kuingia kwenye ufalme wa mbinguni. Wengi wanajifariji kwamba hata kama watakuwa masikini kwenye maisha ya duniani, basi mbinguni wataishi vizuri. Na kuwaona matajiri wa hapa duniani wataenda kuungua moto.

Ondokana kabisa na imani hii potofu rafiki, hakuna dhambi yoyote kwenye utajiri kama umeupata kwa njia sahihi za kuwasaidia wengine. Na pia dini yako itakamilika vizuri kama utakuwa tajiri kuliko ukiwa masikini. Hebu fikiria ni nini kinajenga makanisa na misikiti, fikiria ni nini kinawezesha taasisi hizo kutoa misaada kwa wenye uhitaji kwenye jamii. Ni fedha, na siyo kitu kingine.

Pata fedha, ipate kwa njia sahihi na itakuwezesha kuishi maisha mazuri hapa duniani na kukuhakikishia ufalme wa mbinguni hapo baadaye.

Imani ya saba; UTAJIRI UTANIBADILISHA.

Watu wengi wamekuwa wanawaona watu waliowajua kabla ya kuwa na fedha, lakini baada ya kupata fedha wakabadilika sana. Hivyo wanahofia kwamba na wao wakipata fedha watabadilika. Wengi huamini fedha zinawabadili watu na wanakuwa na roho mbaya au wasiojali.

Ukweli ni kwamba fedha haimbadili yeyote, fedha inaonesha ile tabia halisi iliyopo ndani ya mtu. Fedha inakuza kile ambacho tayari kipo ndani ya mtu. Kama mtu ana ubaya ndani yake fedha inakuza zaidi ubaya huo, na kama ana wema fedha inakuza wema huo.

Ile kauli kwamba pata fedha tujue tabia zako ni sahihi, fedha haibadili chochote, bali inakifunua kiweze kuonekana. Hivyo usiogope kuwa tajiri kwa sababu utajiri utakubadilisha. Badala yake kazana kuwa tajiri na kuwa na tabia njema pia maana utajiri utaonesha zaidi kile ambacho tayari kipo ndani yako.

Rafiki, hizo ndizo imani saba potofu kuhusu fedha zinazokuzuia usifikie utajiri kwenye maisha yako, zivuke imani hizi na ondokana nazo kabisa, weka juhudi kwenye kazi zako na ishi vizuri misingi ya fedha, utakuwa na maisha bora na kuweza kufikia utajiri mkubwa.

KARIBU KWENYE SEMINA YA TABIA ZA KITAJIRI.

Rafiki yangu mpendwa, nimekuandalia semina bora na muhimu sana kwako katika kuuanza mwaka 2019 kwa mafanikio makubwa.

Ni semina inayoitwa TABIA ZA KITAJIRI, ambapo tutajifunza tabia kumi za kuishi kila siku ili kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yetu.

Semina itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap, hivyo utaweza kushiriki ukiwa popote.

Semina itaanza tarehe 03/01/2019 mpaka tarehe 13/01/2019.

Kupata nafasi ya kushiriki semina unalipa ada ya KISIMA CHA MAARIFA (tsh 100,000/=) au kama huwezi hiyo unalipia ada ya kushiriki semina tu (tsh 20,000/=)

Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253 majina Amani Makirita.

Mwisho wa kulipia ni tarehe 02/01/2019 ila nafasi zikijaa kabla hutapata tena nafasi.

Unaweza kumlipia mtu wa karibu kwako akajifunza tabia hizi za kitajiri.

Kujiunga na kundi la semina hii tumia kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/JvJBnoKixGrJZpZdw3shRv  (kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA usijiunge na kundi hili).

Karibu sana tupate maarifa sahihi ya kutujenge tabia zitakazotufikisha kwenye utajiri mkubwa. Fanya malipo yako ya ada leo ili uweze kupata nafasi ya kujifunza TABIA HIZO 10 ZITAKAZOKUPELEKA KWENYE UTAJIRI MKUBWA.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge