Kuweka mipango ni rahisi, kila mtu anapanga na kila mtu anasema.
Na hii mitandao ya kijamii na mawasiliano yamerahisisha sana watu kupanga na hata kusema, hata kama hawajui wanafanyaje.
Kile kitendo tu cha kupanga, kimekuwa ushindi mkubwa kwa wengi. Lakini ushindi huu unayeyuka pale wanaposhindwa kuchukua hatua za kutekeleza yale waliyopanga.
Kadiri mtu anavyopanga na kushindwa kutekeleza alichopanga, anaanza kujidharau na kujiona ni mtu asiyeweza kukamilisha chochote. Anafika hatua anashindwa hata kujiamini kupanga tena, maana ameshajifunza kwamba akipanga hatekelezi.
Sasa leo nimekuandalia hatua mbili rahisi sana za kukuwezesha kuanza chochote unachopanga na usiishie njiani. Kama utafanyia kazi njia hizi mbili, kwa hakika utaweza kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.
Hatua ya kwanza ni kutafuta hamasa yako iko wapi.
Mtu mmoja amewahi kusema hakuna mtu mvivu hapa duniani, sema tu kuna watu ambao hawajajua hamasa zao zipo wapi. Na anasema ukitaka kudhibitisha hilo, mchukue mtu ambaye unafikiri ni mvivu kupitiliza na hataki kufanya chochote, kisha mzamishe kwenye maji kiasi cha kukosa pumzi, na hapo utagundua nguvu kubwa alizonazo mtu huyo.
Hivyo anza kwa kutafuta hamasa yako iko wapi, unapenda kufanya au kufuatilia nini. Ni vitu gani ukiviona vinakusukuma sana, vitu gani vinakupa hamasa, vinakupa matumaini kwamba inawezekana. Tafuta hamasa yako kisha iunganishe na kile unachopanga kufanya. Kile unachofanya, kiweke kwa namna ambayo kinakufikisha kwenye ile hamasa yako. Hata kama havihusiani moja kwa moja, basi unaweza kutumia hamasa hiyo kama zawadi baada ya kufanya ulichopanga.
Kila mtu ana hamasa zake, jua hamasa yako na iunganishe na kile unachopanga kufanya.
Hatua ya pili anza na hatua rahisi ambayo huwezi kuacha.
Eneo ambalo wengi wanashindwa ni huwa wanapenda kuanza na makubwa, wanapenda kuanzia juu, hakuna anayependa kuanzia chini na kwa hatua ndogo. Hivyo wewe anza kwa hatua ndogo kabisa, hatua ambazo huwezi kuacha.
Yaani gawa mipango yako kwa hatua ambazo hata hazikuchoshi kuchukua, huhitaji kufanya maamuzi makubwa ndiyo uanze. Unagawa hatua ziwe ndogo kiasi kwamba kufanya inakuwa sehemu ya maisha yako ya kawaida.
Kwa kufanya hivyo ufanyaji wako unakuwa sehemu ya tabia yako na unaweza kuanza na kuendelea bila ya kuishia njiani.
Kwa kujua hamasa yako na kuitumia kukusukuma, kisha kugawa kwenye hatua ndogo ambazo huwezi kushindwa kuzichukua, utaweza kuanza na hutoishia njiani
Kipi kinakusumbua kwenye kuanza? Anza na hatua hizo mbili na kisha nipe mrejesho wa hatua unazoendelea kupiga.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,