“Do not spoil what you have by desiring what you have not; remember that what you now have was once among the things you only hoped for.” ― Epicurus

Tumeipata nafasi nyingine nzuri siku ya leo,
Nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo makubwa sana.
Tunapaswa kuitumia vizuri nafasi hii ya leo, ili kuweza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yetu.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari USIHARIBU ULICHONACHO KWA KUTAMANI USICHOKUWA NACHO…
Tunapokuwa tunataka kitu, huwa tunakazana sana kukipata,
Huwa tunayaumiza maisha yetu ili kukipata,
Huwa tunapoteza vitu vingine ili tu kupata kile tunachotaka.

Cha kushangaza sasa, tunapopata kile tunachotaka, tunakifurahia kwa muda mfupi, baadaye tunakizoea na kuanza kutamani kingine zaidi ya kile.
Tunazoea kile tulichonacho kama vile hakina maana tena.
Tunasahau kwamba tuliumiza maisha yetu kukipata, tulipoteza baadhi ya vitu kukipata.

Rafiki, chochote ambacho tunacho kwenye maisha yetu, tusikizoee, tuaikichukulie poa kabisa. Hata kama tumekuwa nacho kwa muda mrefu, tusisahau namna tulivyokuwa tunakitamani kabla ya kukipata.
Tuendelee na mapenzi na shauku ya mwanzo kwenye kila tulichonacho kwenye maisha yetu.

Kumbuka siku ya kwanza kupata kile ulichokuwa unataka, iwe ni kazi, biashara, kitu cha kutumia, mahusiano na hata mali nyingine. Hukuwa unafikiria kingine ila kile ulichopata.
Sasa unapaswa kuendelea na shauku ile ya mwanzo bila ya kujali umekaa na kitu hicho kwa muda gani.
Kwa kuendelea na shauku hiyo, utaweza kuvutia vingine vilivyo bora zaidi.

Lakini kama utazoea na kuona ni kawaida, huku ukikimbizana na vitu vingime vipya, kila wakati maisha yako yatakuwa kama bembea, ni juu kwa muda mfupi, kisha chini, juu, chini. Mpaka unaondoka kwenye hii dunia, utakuwa hujawahi kuwa na utulivu wa kutosha ndani yako.

Chochote ulichonacho sasa, kumbuka ulikitamani sana, na ulijitoa sana kukipata, hivyo acha kukitumia kwa mazoea.
Ukawenna siku bora sana ya leo, siku ya kupenda kila ulichonacho kama vile ndiyo siku ya kwanza kukipata.
#MazoeaMabaya, #FanyaKamaSikuYaKwanza, #TamaniUlichonacho

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha