“Don’t just read the easy stuff. You may entertained by it, but you will never grow from it.” – Jim Rohn

Tumepata nafasi nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni fursa bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni siku ya kwenda kujitofautisha na wengine badala ya kushindana nao.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari KUSOMA KUBURUDIKA AU KUSOMA KUKUA?
Swali la msingi sana kujiuliza ni je kipi kinakusukuma kusoma?
Je unasukumwa kusoma kwa sababu unaburudika na kufurahia kile unachokuwa unasoma?
Au unasukumwa kusoma kwa sababu unataka kukua zaidi, unataka kupata maarifa ya tofauti yatakayokuwezesha kupiga hatua zaidi?

Wale wanaosoma kwa kuburudika huishia kusoma vitu rahisi, vitu ambavyo haviwafanyi wafikiri kwa kina na kuja na majibu ya tofauti.
Wanasoma vitu ambavyo ni rahisi, vitu ambavyo wanakubaliana navyo na havitikisi imani wala uelewa wao.
Wanasoma na kufurahi sana, lakini hakuna hatua kubwa wanayopiga, kwa sababu hakuna cha tofauti wanachoondoka nacho.

Wale wanaosoma ili kujifunza na kuwa bora, wanasoma vitu vigumu, vitu ambavyo vinawafanya wafikiri kwa kina na kuja na majibu tofauti. Vitu ambavyo vinawafanya wajiulize kumbe ndiyo iko hivi! Vitu ambavyo vinatikisa imani waliyonayo, vinahoji ukweli waliokuwa wameubeba miaka mingi na vitu ambavyo vinakwenda kunyume na kile wanachokubaliana nacho.
Ni vitu hivi vigumu ambavyo vinamfanya mtu afikiri tofauti na kuweza kuja na njia tofauti za kufanya kwa ubora na utofauti mkubwa.

Tupo kwenye zama ambazo watu hawataki kabisa kusoma vitu vigumu, wanataka vitu rahisi, vitu vilivyotafunwa tayari kwa kumeza. Watu hawataki kusoma vitu vinavyooingana na kile wanachoamini wao, hivyo kinachotokea wanakuwa wanwjilisha upepo, kwa kusoma yale tu yanayowafurahisha.

Jifunze kusoma vitu vigumu, jifunze kuifanya akili yako itulie na kujifunza, kwa kufikiri kwa kina na kuweza kupiga hatua zaidi.
Na vitu vigumu haimaanishi vyenye lugha ngumu, bali vitu ambavyo lazima uwe na utulivu mkubwa kuelewa.

Kadiri wengi wanavyokimbilia vitu rahisim ndivyo vitu vigumu vinavyozidi kuwa na thamani kubwa.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kusoma ili kujifunza na siyo kusoma ili kuburudika. Kadiri unavyoifanyisha kazi akili, ndivyo inavyozidi kuwa bora na imara.
#SomaKujifunza, #SomaVituVigumu, #JifunzeUsivyokubalianaNavyo

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha