Unapochagua nini unataka kwenye maisha yako, na unapojitoa kuhakikisha unapata kile unachotaka, yapo makundi mengi ya watu watakaojitokeza na kuja kwako kwa njia mbalimbali.
Kundi moja kubwa ni la wale ambao watakukosoa kwa kile unachofanya. Kama utakuwa na ndoto kubwa watakuambia achana na ndoto hizo kubwa, hutaweza kuzifikia.
Kama utajituma sana watakuambia acha kujitesa, maisha yanapaswa kufurahia.
Kila unachofanya hawatakosa namna ya kukosoa, kukuonesha kwa nini unachofanya siyo sahihi au unapotea.
Na ukianza kuwasikiliza watu hao, unaweza kuona wapo sahihi, na mwishowe ukakubaliana nao.
Rafiki, leo nakukumbusha kwamba kwa sababu unawasikia, haimaanishi kwamba wapo sahihi.
Kwa sababu wanaweza kusema na kukosea haiwafanyi wapaswe kusikilizwa.
Ukishachagua kile unachotaka, na kujitoa kukipata, hupaswi kumsikiliza yeyote anayekushawishi chochote ambacho ni kinyume na unachotaka wewe.
Unapaswa kuwapuuza wale wote wanaokuja kwako na ushahidi kwamba unachotaka hakiwezekani au unayofanya unakosea. Na wala usitake kila mtu akubaliane na wewe ndiyo ufanye kitu. Kama unachofanya hakiendi kinyume na sheria na taratibu, hakuna ambaye anakulazimisha usikilize anachokuambia.
Na ukitaka kujipa sababu kwa nini hupaswi kuwasikiliza wanaokukosoa na kukukatisha tamaa, kwanza angalia maisha yao, angalia nini wamefanya na maisha yao. Jaribu kuchimba ndani, jaribu kuona yapi makubwa wamefanya, hatua zipi kubwa wamechukua na utajionea mwenyewe kwamba watu wa aina hiyo, mafanikio pekee waliyonayo kwenye maisha yao ni kuua ndoto za wengine.
Hakuna makubwa wanayokuwa wamefanya na maisha yao, na hivyo hupaswi kuwasikiliza hata chembe.
Wakati unapoianza safari ya mafanikio unapaswa kujua kabisa itakuwa safari ngumu, yenye vikwazo na changamoto na hivyo kujitoa kushinda licha ya chochote unachokutana nacho. Hivyo huhitaji tena kuwa na watu wa kukukumbusha hilo kila wakati. Wapuuze wote wanaokukatisha tamaa na kukukosoa wakati wao hakuna kubwa walilofanya kwenye maisha yao.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha kwa ujumbe huu mzr
LikeLike
Karibu James.
LikeLike
Shukran kocha kwa ujumbe yahan raman ya maisha yangu niichore mimi mwingine aweje anisomehe
LikeLike
💪
LikeLike