“The only way to forgive hate, to suffer through pain, is to be grateful for the many things we often take for granted in life.” – James Altucher
Siku nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu ipo mbele yetu.
Ni fursa nzuri sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari SHUKRANI NI JAWABU…
Utakapoamua kuyaishi maisha yako, kufanya yale ambayo ni muhimu kwako, kuna watu watakuchukia kwenye hilo.
Lakini hutaweza kuondokana na chuki za watu hao kwa kuwachukia pia, au kuwalazimisha waone umuhimu wa unachofanya.
Bali njia pekee ya kushinda chuki hizo, ni kuwa na shukrani kwa mambo yote mazuri uliyonayo kwenye maisha yako.
Kushukuru kwa watu wengi wanaokujali ulionao kwenye maisha yako.
Pia utakapoanza kupiga hatua kubwa kwenye maisha yako, utaanza kukutana na kushindwa na kuanguka. Kuangalia zaidi kuanguka huko hakutakuwa na msaada kwako.
Badala yake unapaswa kuwa mtu wa shukrani,
Kwa kushukuru yale mengi mazuri uliyonayo, unaona ni kwa namna gani mambo mengi mazuri yanaendelea kwenye maisha yako.
Sisi binadamu ni viumbe wa ajabu sana, huwa tunasahau haraka sana mambo mazuri na kukumbuka muda mrefu mno mambo mabaya.
Ndiyo maana mtu anaweza kufanya mazuri mengi tukachukulia poa, lakini akikosea mara moja tu tutakazana na kosa hilo moja kwa muda mrefu sana.
Njia pekee ya kuondoka kwenye udhaifu huu mkubwa kwa binadamu ni kuwa na shukrani.
Kwa kitendo cha kushukuru, unajilazimisha kukumbuka mazuri yanayotokea au kuendelea kwenye maisha yetu.
Pia kushukuru kunaifanya akili ivutie zaidi yake ambayo tunashukuru, kwa sababu ndiyo yanakuwa yametawala fikra zetu kwa muda mrefu.
Anza kila siku yako kwa kushukuru, andika kila kitu kizuri na watu wazuri ulionao.
Kila unapokutana na changamoto au kikwazo kwenye siku yako, shukuru kwa mambo mengine mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako. Andika mambo mengine mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako.
Kwa kufanya hivi, hakuna changamoto yoyote itakayoonekana kubwa sana kwako.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kushukuru kwa yale mazuri mengi yanayoendelea kwenye maisha yako.
Na kila mmoja wetu, ana mazuri mengi mno yanayoendelea kwenye maisha yake, ni kitendo cha kuyaangalia tu.
#KuwaMtuWaShukrani, #FikraHuumba, #OnaMazuriKwenyeUbaya
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha