Siku za wengi huwa zinaharibika asubuhi.
Hata uwahi kuamka asubuhi kiasi gani, kama hutaipangilia vizuri siku yako asubuhi hiyo, siku hiyo itapotea bila ya wewe kujua imepoteaje.
Kuianza siku yako kwa mazoea, kwa kuona utafanya kile kinachojitokeza, utaimaliza siku ukiwa umechoka sana lakini ukiangalia utagundua hakuna kikubwa ambacho unakuwa umefanya.
Ili uweze kuitumia vizuri siku yako, ili uweze kufanya makubwa kwenye siku yako, kuna swali moja muhimu sana unapaswa kuanza nalo kwenye kila siku yao.
Swali hilo ni; je ni kitu gani kimoja ambacho nikikifanya leo siku hii itakuwa ya mafanikio makubwa?
Jiulize na ujipe jibu la swali hilo kwenye kila asubuhi yako, kabla hujafanya chochote.
Jua kitu kimoja tu, ambacho ukiweza kukikamilisha kwenye siku yako hiyo basi siku hiyo itakuwa ya mafanikio makubwa sana.
Hata kama una vingi vua kufanya, chagua kipi ndiyo muhimu zaidi.
Kwa kujua kitu hicho na kukifanya, siku yako itakuwa ya mafanikio makubwa sana, na hata vingine vitakuwa rahisi zaidi kwako kufanya.
Usikubali kuanza siku yako ukiwa huna kipaumbele chako namba moja, kwa sababu usipokuwa na kipaumbele, dunia itakupa vipaumbele, ambavyo havina manufaa yoyote kwako.
Anza siku yako na swali hili ulilojifunza hapa, andika jibu lake kwenye kijitabu chako ambacho unatembea nacho siku nzima, na kila wakati jikumbushe jibu la swali lako na jiulize umefikia wapi katika kufanyia kazi lile ambalo ni muhimu zaidi.
Kama huwezi kujua ni kipi muhimu zaidi kwako kufanyia kazi kwenye siku yako, upo kwenye hatari kubwa ya kutokufanikiwa kwenye maisha yako, kwa sababu huenda hujui hata unataka nini na maisha yako.
Hivyo kama unashindwa kujua kipi muhimu kwako kwenye kila siku yako, ni wakati sasa wa kukaa na kufikiria nini unataka na maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,