Kwa chochote unachotaka kwenye maisha yako, zipo mbinu za kukufikisha pale haraka.

Zipo mbinu kwenye kila eneo la maisha yetu, kuanzia kazi, afya, biashara, fedha, mahusiano.

Mbinu ni vile vitu ambavyo ukivifanya unapata matokeo mazuri ndani ya muda mfupi.

Lakini mbinu hizi huwa na changamoto moja kubwa, huwa hazidumu. Mbinu zinabadilika kila wakati.

Mbinu ambayo ilifanya kazi jana, ni vigumu sana ikafanya kazi leo. Pia mbinu ambayo imefanya kazi eneo fulani, inaweza isifanye kazi eneo jingine. Kadhalika mbinu iliyofanya kazi kwa mtu mmoja, mara nyingi haitafanya kazi kwa mtu mwingine.

Hivyo kuipata mbinu sahihi kwako kutumia wakati wowote na ikakupa matokeo bora wakati wote ni vigumu sana. Inachosha sana kuweza kupata mbinu inayokufaa, na hata baada ya kuipata, muda siyo mrefu inabadilika.

Njia pekee ya kutumia ili kupata kanuni sahihi ya mafanikio kwako ni kufuata misingi. Misingi huwa haibadiliki, misingi inafanya kazi kwa watu wote, wakati wowote na eneo lolote.

Msingi sahihi unaleta matokeo mazuri mara zote na kwa mtu yeyote. Na msingi ukifuatwa kwa usahihi unaleta matokeo yanayotarajiwa.

Hivyo rafiki, badala ya kukimbizana na mbinu, hebu tengeneza na ishi misingi sahihi ya mafanikio kwako. Badala ya kukimbizana na vitu vya kupita, hebu komaa na kisichopita.

Ni kweli misingi itachukua muda mpaka uanze kuona matokeo, lakini yatakuwa matokeo ya uhakika na yanayoweza kujirudia wakati wote.

Waache wasiojua wakimbizane na mbinu ambazo hazitawachukua muda mrefu kabla hazijachoka. Wewe kazana na misingi ambayo utaiishi maisha yako yote na itakupa matokeo bora sana wakati wote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha