Habari rafiki yangu mpendwa,

Wapo watu ambao wamekuwa wanayaendesha maisha yako kama saa ya mshale ambayo imeharibika. Kwa nje mishale inaweza kuonekana kama inafanya kazi, lakini kwa hakika imesimama.

Wapo watu ambao kila mwanzo wa mwaka huwa wanaweka malengo makubwa, malengo yanayowahamasisha sana na kuwafanya waone wanaweza kufanya makubwa kwenye maisha yao. Lakini siku chache baada ya kuweka malengo hayo, wanajikuta wamesharudi kwenye maisha ya mazoea na kusahau kabisa malengo waliyojiwekea.

Sasa kinachowafanya watu wafanane na saa iliyoharibika ni kwamba mwaka unapoisha na kuanza mwingine, wanaweka tena malengo yale yale na siku chache baadaye wanajikuta wameshayasahau. Hivyo kinachotokea ni mtu kwa miaka mingi anakuwa anarudi kuweka malengo yale yale lakini hachukui hatua wala kuyafikia.

Watu wengi wanaoweka malengo huwa wanashindwa kuyafikia kwa sababu hawavijui vigezo vitano muhimu sana vya kuweka malengo ambayo mtu ataweza kuyafikia.

Kwa kuwa wewe rafiki yangu nakupenda sana, nimekuandalia makala hii inayochambua vigezo hivyo vitano vya kuweka malengo ambayo mtu utakuwa na uhakika wa kuyafikia.

Karibu ujifunze vigezo hivyo hapa, na kila malengo unayoweka kuanzia sasa yakidhi vigezo hivyo vitano.

Kwa lugha ya kiingereza, huwa wanasema malengo mazuri na yanayofikiwa ni yale yanayozingatia vigezo vitano vinavyofupishwa kwa neno SMART. Neno hili linabeba maneno matano ambayo ni SPECIFIC, MEASURABLE, ATTAINABLE, RELEVANT na TIMELY.

smart goals

Usiogope kwa ugumu huo wa maneno ya kiingereza, nakwenda kukufafanulia vizuri sana kwenye makala yetu ya leo.

Na ili tuelewane vizuri, nitatumia mfano wa lengo la kifedha, ambalo nina uhakika kila mtu huwa anajiwekea lengo hilo kila mwaka.

Kigezo cha kwanza; LENGO LINAPASWA KUWA MAALUMU (SPECIFIC).

Kigezo cha kwanza muhimu kwenye kuweka malengo ambayo utayafikia ni umaalumu wa lengo husika. Unapaswa kuweka lengo ambalo linaeleweka ni nini hasa unachotaka.

Unapaswa kujua ni nini kwa hakika unachotaka kwenye lengo hilo, unakipata wapi, utashirikiana na nani, kwa nini unakitaka na hatua zipi unapaswa kuchukua.

Tukienda kwenye mfano wetu wa fedha, usiweke lengo kwamba nataka fedha zaidi, au nataka kuwa bilionea. Unapaswa kuweka kiasi cha fedha unachotaka na kujua utakipataje kwa hatua zipi unazopaswa kuchukua.

Utaona tofauti kubwa kati ya hali hizo mbili, unaposema unataka fedha zaidi, ukipata elfu kumi ambayo hukuwa nayo ni fedha zaidi. Lakini unaposema unataka milioni 50 au bilioni moja, hapo sasa unakuwa na uhakika nini unataka.

Usiweke malengo yanayoelea hewani, jua kabisa nini unataka na nenda mbali zaidi kujua unakipataje na kwa kufanya nini. Pia unapaswa kuwa na kwa nini inayokusukuma kufikia lengo hilo.

Kigezo cha pili; LENGO LIPIMIKE (MEASURABLE).

Kigezo cha pili kwenye kuweka malengo utakayoweza kuyafikia ni kila lengo linapaswa kuwa linapimika. Hapa unapaswa kuona kabisa ni jinsi gani kupata kile unachotaka kutabadili maisha yako.

Pia unapaswa kuligawa lengo lako kubwa kwenye hatua ndogo ndogo ambazo unaweza kuzitumia kupima maendeleo yako kwenye lengo hilo.

Kwa mfano kama lengo lako ni kupata milioni 50 kwa mwaka, unaweza kuligawa kwa miezi 12 na ukapata kama milioni 4 kwa mwezi, hii inakuwa rahisi kwako kujipima kila mwezi kuona unaelekeaje kwenye lango lako.

Kuweza kuligawa lengo lako kubwa kwenye hatua ndogo ndogo zinazopimika kutakuondolea kukata tamaa pale lengo linapoonekana ni kubwa sana.

Hakikisha kila lengo unaloweka unaweza kupata taswira ya ukiwa umelikamilisha kisha ligawe kwenye hatua ndogo ndogo ambazo ni rahisi kwako kupima.

SOMA; Mambo Kumi (10) Ya Kufanya Mwezi Disemba Ili Mwezi Januari Uwe Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

Kigezo cha tatu; LENGO LIWE NINAFIKIKA (ATTAINABLE).

Kigezo cha tatu ni lengo liwe linafikika. Tumekuwa tunayaelewa sana mafunzo ya maendeleo binafsi ambayo yanatufundisha kwamba ndani yetu tuna uwezo mkubwa na tunaweza kufanya chochote tunachotaka kufanya. Hili ni kweli kabisa kwamba tuna uwezo mkubwa na kuweza kufanya chochote tunachotaka.

Lakini inahitaji muda, nguvu na hata vipaji kufikia lengo lolote tunalojiwekea. Hivyo unapoweka lengo, lazima ujiulize je kwa muda, nguvu, rasilimali na hata vipaji ulivyonavyo utaweza kufikia lengo hilo? Kama siyo unajidanganya.

Kwa mfano kama mwaka huu kipato chako ni shilingi milioni moja kwa mwezi, kujiambia kwamba mwaka kesho unataka upate bilioni moja ni kujidanganya na kujiandaa kushindwa. Ni kweli lengo la bilioni moja linafikika, lakini linachukua muda, na linahitaji jitihada zaidi.

Kwenye kila lengo unalojiwekea, angalia rasilimali ulizonazo kisha weka lengo kubwa ambalo litakusukuma, lakini lisikukatishe tamaa.

Kigezo cha nne; LENGO LIWE NA UHUSIANO NA KUSUDI LA MAISHA YAKO (RELEVANT).

Kigezo cha nne kwenye kuweka malengo utakayoyafikia ni lengo liwe na uhusiano na kusudi la maisha yako. Mara nyingi wengi wamekuwa wanaweka malengo ambayo siyo yao. Kwa sababu wamesikia wengine wakiweka malengo hayo basi na wao wanaona inabidi wayaweke la sivyo wataachwa nyuma.

Watu wengi wamekuwa wanafuata mkumbo kwenye uwekaji wa malengo, wanaweka malengo ambao hayahusiani kabisa na lile kusudi walilonalo kwenye maisha. Wanapokuja kugundua hili wanashindwa kuendelea na malengo yao.

Kwenye kila lengo unalojiwekea, hakikisha linaendana na kusudi kubwa la maisha yako. Hata kama ni lengo kubwa kiasi gani, kama halitokani na kusudi lako kubwa, utaishia kushindwa.

Usijiambie unataka kupata mabilioni ya fedha kupitia biashara fulani ambayo inaonekana kuwa yenye faida kubwa, wakati wewe unapenda kufanya kitu kingine tofauti kabisa. Lengo unaloweka liendane na kile unachopenda na kujali kufanya.

Kigezo cha tano; LENGO LIWE NA UKOMO WA MUDA (TIMELY).

Kigezo cha tano katika kuweka malengo ambayo utayafikia ni kuwa na ukomo wa muda. Wote tunajua jinsi ambavyo ukomo wa muda unavyotusukuma kuchukua hatua. Watu wanaweza kupewa nafasi ya kufanya kitu kwa muda mrefu lakini wasifanye, inapofikia tarehe ya ukomo ndiyo kila mtu anafanya.

Tumia nguvu hii ya ukomo wa muda kwenye malengo unayoweka, kila lengo liwe na ukomo wake wa muda na ujikumbushe ukomo huo ili uweze kujisukuma kufanya zaidi na kufikia lengo hilo. Kwenye kila lengo ulilogawa kwenye hatua ndogo, jiwekee ukomo kwenye kila hatua na ufuate ukomo huo.

Kama umejiambia unataka kupata bilioni moja ndani ya miaka kumi, basi gawa kiasi cha kupata kila mwaka, kila mwezi, kila wiki na hata kila siku, kisha weka muda wa kufuatilia kila kiwango unachotaka kupata ili kuona maendeleo yako yakoje.

Rafiki, hivyo ndivyo vigezo vitano muhimu unavyopaswa kuvitumia kuweka malengo ambayo kwa hakika utayafikia. Tumia vigezo hivi katika kila lengo unaloweka na utaona jinsi utakavyolielewa lengo lako vizuri, kuona kila hatua unayopaswa kuchukua na kuwa na msukumo wa kuchukua hatua kabla muda uliojiwekea haujaisha.

KARIBU KWENYE SEMINA YA TABIA ZA KITAJIRI.

Rafiki yangu mpendwa, nimekuandalia semina bora na muhimu sana kwako katika kuuanza mwaka 2019 kwa mafanikio makubwa.

Ni semina inayoitwa TABIA ZA KITAJIRI, ambapo tutajifunza tabia kumi za kuishi kila siku ili kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yetu.

Semina itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap, hivyo utaweza kushiriki ukiwa popote.

Semina itaanza tarehe 03/01/2019 mpaka tarehe 13/01/2019.

Kupata nafasi ya kushiriki semina unalipa ada ya KISIMA CHA MAARIFA (tsh 100,000/=) au kama huwezi hiyo unalipia ada ya kushiriki semina tu (tsh 20,000/=)

Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253 majina Amani Makirita.

Mwisho wa kulipia ni tarehe 02/01/2019 ila nafasi zikijaa kabla hutapata tena nafasi.

Unaweza kumlipia mtu wa karibu kwako akajifunza tabia hizi za kitajiri.

Kujiunga na kundi la semina hii tumia kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/JvJBnoKixGrJZpZdw3shRv  (kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA usijiunge na kundi hili).

Karibu sana tupate maarifa sahihi ya kutujenge tabia zitakazotufikisha kwenye utajiri mkubwa. Fanya malipo yako ya ada leo ili uweze kupata nafasi ya kujifunza TABIA HIZO 10 ZITAKAZOKUPELEKA KWENYE UTAJIRI MKUBWA.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge