Huu ni ule wakati wa mwaka ambapo kuna kelele nyingi sana kuhusu malengo. Watu wanaulizana mwaka umeisha na umefanya nini na wengine wanahamasishana kuanza kuweka malengo ya mwaka mpya mapema.
Nasema hizi ni kelele kwa sababu karibu kila mtu huwa anajiwekea malengo mwanzoni mwa mwaka. Kila mtu utamsikia akisema mwaka mpya mambo mapya na kisha kuorodhesha mambo makubwa atakayofanya mwaka huo.
Lakini unapokuja kukutana na mtu huyo huyo mwezi januari unapokuwa unaisha, anakuwa ameshasahau kabisa malengo aliyojiwekea kwenye mwaka huo mpya. Anakuwa amerudi kwenye mazoea na hakuna kipya kikubwa anachofanya kwenye maisha yake.
Rafiki, kama unataka mwaka mpya 2020 na mingine ijayo kuwa wa tofauti na wenye mafanikio makubwa kwako, basi unapaswa kuweka malengo pembeni na kukazana na kitu kimoja ambacho nakwenda kukushirikisha kwenye makala hii. Karibu twende pamoja, ujifunze kwa mifano na uweze kuchukua hatua ili maisha yako yawe bora sana.
Mwandishi James Clear kupitia kitabu chake kinachoitwa Atomic Habits: An Easy & Proven Way to Build Good Habits & Break Bad Ones ametushirikisha njia bora sana ya kujijengea tabia ambazo tutadumu nazo. Njia hiyo pia ndiyo tunakwenda kuitumia katika safari yetu ya mafanikio kwa mwaka mpya 2020 na mingine inayokuja.
James anaanza kwa kutushirikisha historia ya timu ya baiskeli ya Uingereza. Kwa miaka 100 (kuanzia 1908 mpaka 2008) timu hiyo ilikuwa imeshinda medali moja tu ya dhahabu kwenye mashindano ya Olympic. Ilikuwa ni timu mbovu kiasi kwamba watengenezaji wa vifaa vya mchezo huo hawakutaka hata kuiuzia timu hiyo vifaa ili wasiharibu majina yao.
Mwaka 2003 timu hii iliajiri kocha mpya aliyeitwa Dave Brailsford. Tofauti na makocha wa awali, Dave alikuja na kitu cha tofauti, hakuhangaika na mambo makubwa kwenye mchezo huo. Badala yake alihangaika na mambo madogo mno. Aliuvunja mchezo huo wa mbio za baiskeli kwenye vipande vidogo vidogo na kisha kuwapa wachezaji wake jukumu la kupiga hatua ndogo sana (asilimia 1) kwenye kila kipande.
Kupitia njia hii, waliweza kuboresha muundo wa baiskeli, kujua muda sahihi wa kulala, aina ya mto mzuri kutumia, jinsi ya kunawa vizuri mikono ili kuepuka maambukizi na hata aina ya vyakula walivyokula.
Miaka mitano baada ya kuanza kwa mabadiliko haya madogo sana, mwaka 2008 matokeo makubwa sana yalianza kuonekana. Kwenye mashindano ya Olympic yaliyofanyika Bijing China, timu hiyo ilishinda asilimia 60 ya medali zote za dhahabu. Miaka minne baadaye, kwenye mashindano ya Olyimpic yaliyofanyika Uingereza, timu hiyo iliweka rekodi 9 za Olyimpic na rekodi 7 za dunia.
Kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia 2007 mpaka 2017, timu ya baiskeli ya Uingereza iliweza kushinda mashindano 178 ya dunia na mashindano 66 ya Olympic ambayo ni mafanikio makubwa mno kwa kipindi kifupi ukilinganisha na muda mrefu ambao timu hii ilikuwa inajaribu.
Swali la kujiuliza ni je miujiza hii imewezaje kutokea? Ni kwa namna gani timu ambayo ilikuwa hovyo kwa miaka mingi na kuweza kuleta mabadiliko makubwa ndani ya miaka mitano? Kwa hakika siyo malengo, kwa sababu kwa miaka yote timu hiyo ilikuwa inaweka malengo ya kushinda lakini hayo hayakutokea. Lakini kuna kitu kimoja kilibadilika na kikaleta matokeo makubwa sana.
Kujifunza jinsi unavyoweza kutengeneza miujiza kwenye maisha yako bonyeza hapa
SAHAU KUHUSU MALENGO, KAZANA NA MCHAKATO.
Ushauri maarufu kwenye mafunzo ya hamasa na mafanikio ni kwamba kama unataka kufanikiwa basi lazima uwe na malengo na uyafanyie kazi. Hivyo kila mtu anahamasika kuweka malengo, lakini wengi bado wanashindwa kupiga hatua.
Kinachowafanya wengi kushindwa kufanikiwa licha ya kuwa na malengo ni kwa sababu wanaweka mkazo mkubwa kwenye malengo na kusahau kitu muhimu ambacho kinawawezesha kupiga hatua. Kitu hicho ni mchakato ambao mtu anapaswa kuufuata katika kufikia lengo ambalo amejiwekea.
Tukirudi kwenye mfano wa timu ya baiskeli ya Uingereza, kwa miaka 100 imekuwa inaiwekea malengo ya kushindwa, lakini hakikuwa inashinda. Ni mpaka pale walipoanza kuweka mkazo kwenye mchakato unaopelekea ushindi ndipo walipoanza kushinda kwa viwango vya juu.
Kadhalika hata kwako pia, kinachokuzuia usifikie malengo yako ya kuanzisha na kukuza biashara, kupunguza uzito, kusoma vitabu, kuongeza kipato, kuboresha mahusiano na mengine mengi, ni kwa sababu unahangaika sana na malengo na kusahau mchakato.
Kitakachokuwezesha wewe kufanikiwa mwaka 2020 na miaka mingi ijayo siyo malengo unayojiwekea, bali mchakato unaofanyia kazi kila siku ili kufikia malengo hayo. Nguvu ipo kwenye mchakato na wale wanaotengeneza mchakato unaowasukuma kuchukua hatua ndogo kila siku, ndiyo wanaovuma matokeo makubwa.
Tofauti ya malengo na mchakato ipo kwenye eneo moja, matokeo. Malengo yanalenga matokeo unayotaka kupata, mchakato unalenga njia ya kufikia malengo hayo. Hivyo hapo unajifunza wazi kwa nini mchakato una nguvu, kwa sababu huo ndiyo unakufikisha kwenye matokeo.
MATATIZO MAKUU YA MALENGO.
Malengo yamekuwa kikwazo cha wengi kufanikiwa kwa sababu yana matatizo makubwa manne;
Moja; wanaoshinda na wanaoshindwa wote wana malengo.
Kama timu za Simba na Yanga zinaingia uwanjani kushindana, kila timu inaingia uwanjani ikiwa na lengo la kushindwa. Lakini tuna uhakika kwamba kuna timu moja tu inayoweza kushinda hapo. Hivyo kinachoisaidia timu inayoshinda siyo malengo ambayo wanayo, kwa sababu hata wanaoshindwa wana malengo pia, bali kinachowatofautisha ni mchakato wanaotumia.
Usijidanganye kwamba kuwa na malengo pekee kunakutosha wewe kufanikiwa, una historia nzuri, ulishaweka malengo mengi huko nyuma na hukuyafikia. Sasa unahitaji kitu cha tofauti, unahitaji mchakato wa kukupeleka kwenye mafanikio.
Mbili; malengo yanaleta mabadiliko yasiyodumu.
Umewahi kuweka lengo fulani, ukalifanyia kazi na kulifikia, halafu mwisho ukajikuta unarudi ulikokuwa mwanzo? Hii ipo sana kwenye malengo kama ya kupunguza uzito au kutoka kwenye madeni. Unaweka lengo, unalifanyia kazi na kulifikia. Baada ya kulifikia unaona umeshamaliza, ukisha kustuka uzito umerudi kama mwanzo au umerudi tena kwenye madeni.
Malengo hayaleti mabadiliko yanayodumu, bali ni mabadiliko ya muda mfupi. Ili uweze kuleta mabadiliko yanayodumu kwenye maisha yako, unahitaji kuwa na mchakato ambao unaufuata kila siku kwenye maisha yako.
Tatu; malengo ni kikwazo kwa furaha.
Watu wengi wamekuwa wanashikiza furaha zao kwenye malengo. Mtu anajiwekea lengo, kisha anajiambia kwamba akishakamilisha lengo hilo ndiyo atakuwa na furaha. Kwa namna hii, mtu anashindwa kuishi kwa furaha. Kwa sababu hata pale anapofikia lengo, furaha hiyo hukaa kwa muda mfupi na baadaye anagundua anahitaji kuweka lengo kubwa zaidi.
Kwa kuwa na mchakato, husubiri mpaka ufikie lengo ndiyo ufurahi, badala yake kila siku inakuwa ya furaha kwako kwa sababu kuna mchakato unaofanyia kazi. Kila siku unakuwa na furaha kwa hatua ndogo unazoendelea kuchukua.
Nne; malengo ni kikwazo cha maendeleo ya kudumu.
Umewahi kuona mtu anaanzia chini kabisa, anajiwekea lengo la kufika juu, anafanya kazi usiku na mchana, anang’anga’ana kweli na anafika kule alikopanga kufika. Lakini baada ya kufikia lengo hilo kubwa, anakosa kabisa hamasa ya kuendelea tena kujisukuma. Anarudi kwenye mazoea na hilo linamfanya aanguke. Hii ipo sana kwenye michezo na sanaa na hata kwenye biashara. Kwa mtu kuhangaika sana na lengo, anapolifikia anaona ameshamaliza kila kitu na hapo ndipo anapoanza kuanguka.
Kama unataka maendeleo ya kudumu, basi unapaswa kuwa na mchakato unaoufanyia kazi kila siku, kwa namna hii, hakuna wakati utakaojiambia kwamba umemaliza au umefika kileleni na hivyo unapaswa kupumzika.
Kujifunza vigezo vitano unavyopaswa kutumia kuweka malengo ili uyafikie bonyeza hapa.
Hayo ndiyo matatizo ya malengo na jinsi ambavyo yanawapoteza wengi.
Swali ambalo najua unajiuliza ni je ina maana sihitaji tena kuweka malengo? Je nitayaendeshaje maisha yangu bila ya malengo? Nitajipimaje?
Majibu ni unapaswa kuweka malengo, kwa sababu ndiyo njia ya kukuwezesha kutoka hapo ulipo sasa na kufika mbali zaidi. Lakini ukishaweka malengo yako, kazana zaidi na mchakato unaofanyia kazi kila siku na siyo lengo hilo tu. Ukiweka nguvu zaidi kwenye mchakato, unajiweka kwenye nafasi ya kufikia lengo lolote ulilonalo.
Hapo chini nimekupa mifano ya jinsi ya kutumia mchakato kufikia malengo yako ya 2020.
MIFANO YA JINSI YA KUTUMIA MCHAKATO 2020 ILI KUFANIKIWA.
Rafiki, pamoja na changamoto za malengo tulizojifunza, bado unapaswa kujiwekea malengo, lakini unapaswa kuhakikisha unaweka mchakato wa kufikia malengo yako na nguvu zako unaziweka kwenye mchakato husika.
Kama lengo lako ni kupunguza uzito, usikazane sana na namba unayotaka kufikia, badala yake tengeneza mchakato wako wa siku, unakula nini, huli nini na mazoezi gani unafanya. Ukiweza kukazana na vitu hivyo, ulaji na mazoezi kila siku, utalifikia lengo bila hata ya kusumbuka.
Kama lengo lako ni kuanzisha au kukuza biashara yako, tengeneza mchakato wa kutoa huduma bora kwa wateja wako, kwa kila namba. Kila siku fanya kitu ambacho kinamfanya mtu atake kurudi kwako, awaambie wengine kuhusu biashara yako. Kwa kurudia mchakato huu kila siku, utalifikia lengo lako.
Kama lengo lako ni kuweka akiba na kufikia uhuru wa kifedha, weka mchakato ambapo kila kipato kinachoingia, kiasi fulani unaweka pembeni kabla ya kuanza matumizi. Unachopaswa kuhakikisha ni kwamba matumizi yako ni madogo kuliko kipato chako. Hata kama unayoweka pembeni ni elfu moja tu, ina tofauti kubwa na kutokuweka kabisa.
Kama lengo lako kusoma vitabu zaidi usikimbilie kuangalia vitabu vingapi utamaliza kusoma. Badala yake weka mchakato wa usomaji kila siku. Unaweza kuchagua kusoma ukurasa mmoja kila siku, au kurasa 5 au kumi kila siku. Na kugawa kurasa hizi asubuhi, mchana na jioni. Ukifuata mchakato huo kila siku, utajikuta unasoka zaidi kuliko ukisumbuka na namba ya vitabu unavyotaka usome.
Kama lengo lako ni kuwa mwandishi, usiangalie ni vitabu vingapi unataka kuandika au makala ngapi. Wewe weka mchakato wa kuandika idadi fulani ya maneno kila siku, labda maneno 500 au maneno 1000 kila siku. Kisha rudia mchakato huo kila siku na mwisho utajikuta umeandika kiasi kikubwa sana.
Kama lengo lako ni kuwa mfanyakazi bora kwenye eneo lako la kazi, weka mchakato wa kuboresha zaidi kila unachofanya kila siku. Nenda hatua ya ziada, fanya zaidi ya unavyotegemewa na weka umakini kwenye kila unachofanya. Hatua ndogo ndogo kama hizi mwisho zinaleta matokeo makubwa sana kwako.
NI MCHAKATO GANI UNAKWENDA KUJIWEKEA 2020?
Rafiki, umeona jinsi mchakato ulivyo na nguvu, umeona jinsi ambavyo hatua ndogo ndogo zinajikusanya na kuleta matokeo makubwa.
Swali langu kwako ni hili, je ni mchakato gani unaokwenda kujiweka kwa mwaka 2020? Najua ukikazana na mchakato kwa mwaka mzima, hutabaki pale ulipo sasa.
Hivyo nikusihi sana, weka lengo ulilonalo, kisha weka mchakato utakaofuata kila siku. Na kama unahitaji twende pamoja 2020 katika kuishi kwa mchakato kila siku, ambapo napata nafasi ya kukufuatilia kwa karibu, basi nakukaribisha sana kwenye programu ya KISIMA CHA MAARIFA kama bado hujawa mwanachama. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma ujumbe kwenda wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utapata maelekezo.
Pia nikukaribishe kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA ambapo utakwenda kupata uchambuzi wa kina wa kitabu ATOMIC HABITS, kwenye kitabu hichi, mwandishi ametushirikisha hatua nne za kujenga au kuvunja tabia yoyote ile. Hatua hizi ni KICHOCHEO, TAMAA, HATUA NA ZAWADI. Ukiweza kuzielewa hatua hizi na kuzifanyia kazi, tabia hazitakuwa tatizo tena kwako. Kujiunga na channel hii ili upate uchambuzi wa kitabu hicho na vingine vingi, fungua kiungo hiki; https://www.t.me/somavitabutanzania
Karibu sana rafiki yangu tuendelee kujifunza na kuchukua hatua ili maisha yetu yaendelee kuwa bora sana.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania