“Your level of success will rarely exceed your level of personal development, because success is something you attract by the person you become.” -Hal Elrod
Hongera sana rafiki kwa nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu tuliyoipata leo.
Tumeweza kuiona siku nyingine nzuri sana kwetu, siku ambayo tunaweza kwenda kufanya makubwa sana na kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari UKOMO WA MAFANIKIO YAKO…
Ukomo wa mafanikio yako ni ukomo wa ukuaji wako binafsi.
Huwezi kufanikiwa zaidi ya ukuaji binafsi ulionao.
Hivyo unapotaka mafanikio zaidi, anza kwanza kufanyia kazi ukuaji wako binafsi, anza kwanza kukua wewe zaidi.
Popote ulipo sasa na ukajiona kama umekwama, jua unajikwamisha wewe mwenyewe, kwa kutokukua zaidi.
Kama kipato chako kimekwama na hakikui tena, jua hayo ni matokeo ya kukwama kwa ukuaji wako binafsi.
Kama biashara yako iko vile vile miaka nenda miaka rudi, jua tatizo ni wewe hukui.
Mafanikio siyo kitu ambacho tunakitengeneza, bali ni kitu ambacho tunakivutia kwa namna tunavyokuwa sisi wenyewe.
Kama mafanikio ni chuma, basi ili tuyavutie tunapaswa kuwa sumaku. Na kwa jinsi ambavyo usumaku wetu unavyokuwa mkubwa, ndivyo tunavyovuta vyuma vingi zaidi.
Unapogundua kwamba umekwama pale ulipo sasa, wala uaimtagute mchawi au kutaka kuangalia nani anakuweka hapo.
Jua tatizo lipo ndani, tatizo lipo kwenye ukuaji wako binafsi.
Tatua tatizo hilo la ndani, kazana kukua zaidi na utaweza kupiga hatua kubwa zaidi kimafanikio.
Pia usiombe mafanikio yakuangukie kwa bahati kama ndani hujakua, utaishia kupoteza kile ulichopata na huenda hata maisha yako yakaharibika pia.
Wale wanaoridhi mali au kushinda bahati nasibu na wakapoteza fedha zote siyo kwamba ni wajinga sana, bali wanakuwa wamekutana na mafanikio makubwa kuliko ukuaji wao wa ndani.
Hivyo hakikisha wewe una ukuaji wa ndani endelevu, kila siku unayoianza, hakikisha unaimaliza ukiwa mwerevu zaidi kuliko ulivyoianza.
Jipatie maarifa ya kukuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako. Maarifa haya yanakusanyika kidogo kidogo na kuleta mapinduzi makubwa kwako.
Ukawe na siku bora sana kwako leo, siku ya kukua zaidi ndani yako ili kuvutia mafanikio makubwa zaidi.
#UkuajiWaNdani, #JifunzeKilaSiku, #KuwaBoraLeoKulikoJana
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha