Kila unapotaka kupata fedha zaidi, nakushauri uangalie sehemu moja, matatizo magumu ambayo yanawasumbua wengi kisha yatatue hayo.

Fedha ipo kwenye matatizo magumu na yanayowasumbua wengi.

Kwa sababu ni magumu, hakuna wengi wanaohangaika nayo, na hivyo unapoyatatua, unajiwekea upekee ambao unapatikana kwako tu.

Usikimbizane na vitu rahisi, vitu ambavyo kila mtu anaweza kufanya. Kimbizana na vitu vigumu, vitu ambavyo wachache sana wanafanya na wengi wanavikimbia.

Unapokimbilia vitu rahisi unajipeleka kwenye ushindani mkubwa, kwa sababu wengi tayari wanafanya. Japo wahitaji wa vitu hivyo rahisi wanaweza kuwa wengi, lakini utasumbuka sana mpaka kupata fedha unayotaka.

Kwenye vitu vigumu utaumia mwanzo unapotafuta suluhisho, lakini baada ya hapo njia inakuwa rahisi kwako.

Pia ni kweli kwamba wateja wanaweza kuwa wachache wenye uhitaji wa suluhisho la vitu hivyo vigumu, lakini ni wateja wanaojali na walio tayari kulipa ili kupata suluhisho wanalotaka.

Tunaweza kusema kwamba kwenye maisha kila mtu atalipa gharama fulani, kuna ambao wanachagua kulipa gharama hiyo mwanzoni na baadaye wanakwenda vizuri. Na kuna ambao wanajaribu kuikwepa mwanzoni na kujiona wajanja kwamba wamekwepa ugumu, ila wanajikuta wakilipa gharama hiyo kidogo kidogo kwa maisha yao yote.

Chagua kulipa gharama mwanzoni, chagua kubobea kwenye mambo magumu ambayo wengi wanayakimbia, na baada ya hapo utakuwa na uhakika wa kupata kiasi cha fedha unachotaka. Kwa sababu fedha ipo kwenye matatizo magumu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha