Rafiki yangu mpendwa,
Mtu mmoja amewahi kusema kwamba huwa tunajenga tabia, kisha tabia zinatujenga. Na hili ni kweli kabisa. Mwanzoni wakati tunajifunza tabia yoyote ile, iwe nzuri au mbaya huwa tunaweka kazi hasa. Lakini baadaye ikishakuwa tabia tunajikuta tunafanya bila hata ya kufikiri.
Maisha yetu yapo pale yalipo sasa kutokana na tabia ambazo tumejijengea siku za nyuma. Kila tunachofanya kwenye siku yetu ya leo, ni tabia ambazo tumezijenga sisi wenyewe wakati mwingine bila hata ya kujua.
Yale tunayojiambia tunaweza au hatuwezi, yale tunayojiambia tunapenda au hatupendi, ni matokeo ya tabia ambazo tumejijengea.
Ni kutokana na umuhimu huu mkubwa sana wa tabia kwenye maisha na mafanikio yetu ndiyo nimeamua kukuandalia semina ya TABIA ZA KITAJIRI.
Kwenye semina hii, nakwenda kukushirikisha kwa kina sana tabia kumi ambazo ukiweza kuziishi kila siku, maisha yako yataweza kuwa bora sana. Utaweza kujijengea utajiri mkubwa kwenye maisha yako na kuwa na mafanikio makubwa sana.
Nitakupa maelekezo kamili ya jinsi ya kushiriki semina hii mwisho wa makala hii. Lakini kabla sijakupa utaratibu huo, nina zawadi nzuri sana kwako kwa sababu wewe ni rafiki yangu na tumekuwa pamoja kwa muda sasa.
Huenda kwa sababu moja au nyingine ukashindwa kushiriki semina hii, ambayo itakwenda kuzama ndani sana kwa kila tabia. Lakini kwa sababu nakupenda sana, sitaki ukose kabisa kuzijua tabia hizi kumi.
Ndiyo maana leo, nakwenda kukushirikisha tabia zote kumi nitakazokwenda kuzifundisha kwa kina kabisa kwenye semina ya TABIA ZA KITAJIRI.
Nakushirikisha tabia zote kumi bila ya kuacha hata moja, kisha wewe utachagua, kama ni tabia unazoona zinakufaa na hivyo ukashiriki semina kwa kina ili kuondoka na mkakati wa kufanyia kazi.
Na hata kama utashindwa kushiriki semina, basi ujue nini cha kuzingatia kwenye kila siku ya maisha yako ili kuwa na mafanikio makubwa sana kwako.
Rafiki, nakusihi sana uzisome tabia hizi kumi na mara moja uanze kuzijenga kwenye maisha yako, mwanzo zitakuwa ngumu lakini kadiri unavyokwenda zitakuwa rahisi.
Na kama unataka kujifunza mkakati bora wa kuzijenga tabia hizi ili ziwe sehemu ya maisha yako, basi usikose kushiriki semina ya TABIA ZA KITAJIRI, maelezo kamili yapo mwisho wa makala hii.
Zifuatazo ni tabia kumi unazopaswa kuziishi kila siku ili uweze kupata utajiri na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Moja; KUWA MTUMWA WA TABIA NZURI.
Hatua ya kwanza kabisa kwenye kutengeneza mafanikio ni kujijengea tabia nzuri za kila siku na kuwa mtumwa wa tabia hizo. Na wala huhitaji kuanzia mbali sana kujenga tabia nzuri, bali anza na tabia ulizonazo sasa kisha zigeuze kuwa tabia nzuri.
Kwa mfano kama sasa hizi unatumia muda wako mwingi kuangalia tv au kwenye mitandao ya kijamii, jiwekee ukomo kwenye mambo hayo. Mfano jiambie utatenga saa moja pekee kwenye siku yako kwa ajili ya habari, tv na mitandao ya kijamii. Kwa tabia kama hii utaokoa muda wako mwingi ambao kwa sasa unaupoteza.
Kadhalika badili tabia ulizonazo sasa kwenye ulaji, unywaji, muda wa kuamka, muda wa kulala na mengine yote unayofanya kila siku ya maisha yako.
Zoezi la kuchukua; orodhesha tabia zote unazofanya kwenye kila siku yako, kisha angalia zipi ni nzuri kwako na zipi siyo nzuri kwako. Zile nzuri endelea na nazo na zile mbaya zigeuze kuwa nzuri.
Mbili; KUWA NA MALENGO YA KILA SIKU, KILA WIKI, KILA MWEZI, KILA MWAKA NA YA MUDA MREFU.
Bila ya kuwa na malengo unayoyafanyia kazi, juhudi zozote unazoweka unapoteza. Unaweza ukachoka sana, lakini ukiangalia hakuna kikubwa ulichokamilisha.
Unapaswa kuwa na malengo unayoyafanyia kazi kila siku, malengo yako yanapaswa kugawanywa kwenye siku, wiki, mwezi, mwaka na muda mrefu.
Malengo ya siku unayaweka mwanzo wa siku, kwa kuweka orodha ya vile utakavyofanyia kazi siku hiyo.
Kila mwanzo wa wiki weka malengo ambayo unataka kuyakamilisha wiki hiyo. Kadhalika kwenye mwezi na hata mwaka.
Unapaswa kuwa na malengo ya muda mrefu, miaka 5, 10, 20 na mpaka 50 ijayo. Kila wakati unapaswa kuwa unasukumwa na malengo unayoyafanyia kazi.
Zoezi la kufanya; kaa chini na weka au pitia malengo uliyonayo, kisha yaweke kwenye mafungu ya malengo ya muda mrefu, malengo ya mwaka, ya mwezi, ya wiki na kisha ya siku. Anza kila siku yako ukiwa na malengo na mipango unayofanyia kazi na hutapoteza muda kabisa kwenye siku yako.
Tatu; JIENDELEZE ZAIDI KILA SIKU.
Ukomo pekee ambao unao kwenye maisha yako ni ule unaojiwekea ndani yako. Mafanikio yako hayawezi kukua zaidi ya unavyokua wewe. Hivyo tabia muhimu sana unayopaswa kujijengea ni ya kujiendeleza zaidi kila siku.
Jiendeleze kila siku kwa kujifunza na kujisomea angalau kwa dakika 30 kila siku. Yaani siku isipite kama hujajifunza kitu kipya. Tenga muda wa dakika 30 wa kujifunza ili uwe bora zaidi.
Soma vitabu, sikiliza vitabu, angalia mafunzo kwa njia ya video na kadhalika, lakini hakikisha kila siku unajifunza. Hakikisha siku inapoanza na kuisha, unakuwa bora zaidi kuliko ulivyoanza siku hiyo.
Zoezi la kufanya; tenga dakika 30 kwenye kila siku yako kwa ajili ya kujifunza na kuwa bora zaidi. Tenga vitabu utakavyosoma, kusikiliza na hata mafunzo utakayoangalia. Usikubali siku ipite hujajifunza kitu kipya.
Nne; JALI NA BORESHA AFYA YAKO.
Yote unayotaka kwenye maisha yako yatabaki kuwa ndoto kama hutakuwa na afya bora. Kwa sababu kama afya siyo bora, hutaweza kuweka mapambano yanayohitajika. Pia kama utaweka juhudi sana kupata mafanikio na ukasahau afya yako, ukayapata mafanikio lakini afya ikawa mbovu hutaweza kufurahia mafanikio hayo.
Tengeneza tabia ya kujali afya yako kila siku. Na maeneo mawili ya kujali na kuboresha afya yako ni kwenye ulaji na mazoezi.
Kwenye ulaji unapaswa kula chakula bora kiafya na kula kwa kiwango ambacho siyo kingi. Epuka vyakula vinavyoandaliwa haraka maana huwa siyo vizuri kiafya.
Pia kuwa na mpango wa mazoezi kila siku. Kila siku fanya mazoezi kwa angalau dakika 30. Mazoezi ya kukimbia ni mazuri kuliko mazoezi ya aina nyingine yoyote.
Zoezi la kufanya; pangilia mlo wako wa kila siku ili kuwa na afya bora. pia tenga nusu saa kwenye kila siku yako kwa ajili ya mazoezi.
Tano; JALI NA BORESHA MAHUSIANO YAKO.
Huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe, kauli ya jeshi la mtu mmoja ni kauli ya kujidanganya, hakuna jeshi la mtu mmoja. Mafanikio yako yanahitaji timu kubwa sana ya watu, kuanzia familia yako, watu wako wa karibu, unaohusiana nao kwenye kazi na hata biashara na jamii inayokuzunguka kwa ujumla.
Moja ya tabia muhimu ya kujijengea kila siku ni kutengeneza na kuboresha mahusiano yako na watu wengine. Kila unachokitaka kinatoka kwa watu wengine hivyo mahusiano haya yanapokuwa bora, unaweza kupata zaidi kila unachotaka.
Zoezi la kufanya; yajue mahusiano muhimu kwenye kila eneo la maisha yako, kuanzia familia, marafiki, kazi, biashara na jamii kwa ujumla. Kisha tenga muda wa kuboresha mahusiano haya kupitia mawasiliano na hata kufanya vitu kwa ajili ya wengine.
Sita; ISHI KILA SIKU KWA KIASI.
Kila unachofanya kwenye maisha yako, kinapaswa kuwa kwa kiasi, hupaswi kufanya kwa kiwango kidogo sana wala kufanya kwa kupitiliza.
Kuanzia kwenye maisha binafsi na hata kazi au biashara, fanya kwa kiasi. Usile kupitiliza, usinywe kupitiliza, usiwe na hisia kali kupitiliza na wala usipumzike kupitiliza.
Kuishi kwa kiasi ni tabia muhimu sana ambayo itakuwezesha kufika kwenye mafanikio makubwa. Kwa sababu unapofanya kupita kiasi, unauchosha mwili na unashindwa kufanya yale ambayo ni muhimu.
Zoezi la kufanya; kwa yale unayofanya kila siku kwenye maisha yako, fanya kwa kiasi, jidhibiti wewe mwenyewe usifanye jambo lolote kupitiliza. Usile kupitiliza, kunywa kupitiliza au kupatwa na hisia zilizopitiliza. Kufanya hivyo kutakupeleka kwenye matatizo makubwa.
Saba; KAMILISHA MAJUKUMU YA KILA SIKU.
Tabia ya saba ya kuishi kila siku ili uweze kupata mafanikio makubwa ni kukamilisha majukumu unayojiwekea kila siku. Kila unachopanga kufanya, unapaswa kukifanya kwa muda uliopanga kufanya. Kamwe usiahirishe chochote, usijiambie nitafanya kesho, chochote kinachoweza kufanyika leo kifanye.
Pale wazo la kuahirisha kitu linapoingia kwenye akili yako, mara moja jiambie NITAFANYA SASA, rudia maneno hayo mara nyingi na utasahau kuhusu kuahirisha na kuweza kuchukua hatua mara moja.
Zoezi la kufanya; kila unachoorodhesha kufanya kwenye siku yako kifanye, usiwe mtu wa kuahirisha mambo. Wazo la kuahirisha linapokujia, jiambie NITAFANYA SASA, kisha fanya.
Nane; KUWA NA FIKRA ZA KITAJIRI KILA SIKU.
Kuna fikra za kitajiri na fikra za kimasikini. Fikra za kitajiri ni fikra chanya, za hamasa na matumaini makubwa. Fikra za kimasikini ni fikra hasi, za kukata tamaa na kushindwa.
Ili uweze kufanikiwa unapaswa kuwa na fikra za kitajiri kila siku, unapaswa kuwa na kauli chanya ambazo unajiambia kila siku, kauli ambazo zinakupa hamasa na kukusukuma kusonga mbele zaidi. Jijengee taswira ya kile unachotaka kwenye maisha yako na mara kwa mara jione umeshapata kitu hicho. Kwa kufanya hivi unaipa akili yako kazi ya kuhakikisha unapata unachotaka.
Zoezi la kufanya leo; dhibiti fikra zako ziwe chanya na za kitajiri kila siku. Fikiria yale ambayo yanakufikisha kwenye kile unachotaka. Jione tayari umeshafika pale unapotaka na weka picha hiyo kwenye akili yako mara zote. Hili litakufanya uvutie mazingira yatakayokuwezesha kupata unachotaka.
Tisa; WEKA AKIBA SEHEMU YA KUMI YA KIPATO CHAKO.
Kwenye kila kipato unachoingiza, asilimia kumi ya kipato hicho hupaswi kuitumia kwa shughuli nyingine yoyote, bali unapaswa kujilipa wewe mwenyewe. Hichi ni kipato ambacho unakiweka pembeni maalumu kwa ajili ya uwekezaji ambao utakulipa zaidi baadaye.
Unapopata fedha, kabla hujaanza kulipa bili mbalimbali unazodaiwa au kununua vitu unavyohitaji, jilipe wewe mwenyewe kwanza. Hii ni tabia moja rahisi ambayo imewawezesha wengi kufikia utajiri mkubwa, bila ya kujali kiasi cha kipato walichonacho. Unapaswa kujilipa kwanza kabla hujafanya matumizi, kwa sababu ukisema utumie halafu itakayobaki ndiyo ujilipe, hutabakiwa na kitu.
Zoezi la kufanya; kwenye kila kipato unachoingiza, kabla hujaanza kupangilia unakitumiaje, ondoa kwanza asilimia kumi ya kipato hicho na weka pembeni, weka mahali ambapo hutakitumia hata iweje. Kipato hicho ni kwa ajili ya uwekezaji, ndiyo kitakachokufanyia wewe kazi.
Kumi; DHIBITI MAWAZO NA HISIA ZAKO KILA SIKU.
Ili uweze kufanikiwa, unapaswa kuzitawala hisia na mawazo yako kila wakati. Hupaswi kuruhusu mawazo hasi kuingia kwenye akili yako. Hisia hasi kama za hasira, wivu, huzuni, hofu na hata kukata tamaa, hazipaswi kupata nafasi ndani yako.
Unapaswa kuwa bize na malengo na mipango yako ya kila siku kiasi kwamba mawazo na hisia hasi havipati nafasi kabisa kwenye akili yako. Na ukiweza kufanya hivi hutapata nafasi ya kuwa na huzuni au kupata sonona.
Zoezi la kufanya; kila wakati kagua mawazo na hisia ambazo unazo, je ni hasi au chanya. Kama ni hasi badili mara moja kwenda chanya. Huwezi kufanikiwa ukiwa na mawazo na hisia hasi. Lazimisha akili yako ifikiri chana na mara zote jiweke kwenye hisia chanya. Hili litakuwezesha kuona matumaini na kujituma zaidi.
Rafiki, hizo ndiyo tabia kumi za kuishi kwenye kila siku ya maisha yako, tabia ambazo zitakuwezesha kuwa na mafanikio makubwa na utajiri pia.
Tabia hizi ni matokeo ya tafiti mbalimbali ambazo zimeangalia wale waliofanikiwa sana na wale walioshindwa, kisha ikaangaliwa kipi hasa kinawatofautisha na ndipo tabia hizo zilipoonekana.
Rafiki yangu mpendwa, kama nilivyokuambia, hapa nimekuonjesha tu, nimekupa kwa ufupi sana nini unapaswa kufanya.
Kama unataka kupata kwa kina zaidi, kama unataka kujua jinsi ya kufanya na hatua kwa hatua jinsi ya kuishi kila siku yako ili uweze kufikia utajiri na mafanikio makubwa, basi usikose semina ya TABIA ZA KITAJIRI.
Kwenye semina ya tabia za kitajiri tunakwenda kujadili kwa kina tabia hizi kumi na jinsi ya kuzifanya kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
KARIBU KWENYE SEMINA YA TABIA ZA KITAJIRI.
Rafiki yangu mpendwa, nimekuandalia semina bora na muhimu sana kwako katika kuuanza mwaka 2019 kwa mafanikio makubwa.
Ni semina inayoitwa TABIA ZA KITAJIRI, ambapo tutajifunza tabia kumi za kuishi kila siku ili kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yetu.
Semina itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap, hivyo utaweza kushiriki ukiwa popote pale bila ya kuacha shughuli zako.
Semina itaanza tarehe 03/01/2019 mpaka tarehe 13/01/2019.
Kupata nafasi ya kushiriki semina unalipa ada ya KISIMA CHA MAARIFA (tsh 100,000/=) au kama huwezi hiyo unalipia ada ya kushiriki semina tu (tsh 20,000/=)
Namba za kufanya malipo ni 0755 953 887 au 0717 396 253 majina Amani Makirita.
Mwisho wa kulipia ni tarehe 02/01/2019 ila nafasi zikijaa kabla hutapata tena nafasi.
Unaweza kumlipia mtu wa karibu kwako akajifunza tabia hizi za kitajiri.
Kujiunga na kundi la semina hii tumia kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/JvJBnoKixGrJZpZdw3shRv (kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA usijiunge na kundi hili).
Karibu sana tupate maarifa sahihi ya kutujenge tabia zitakazotufikisha kwenye utajiri mkubwa. Fanya malipo yako ya ada leo ili uweze kupata nafasi ya kujifunza TABIA HIZO 10 ZITAKAZOKUPELEKA KWENYE UTAJIRI MKUBWA.
Pia fanya malipo yako leo ili usikose nafasi ya kujifunza tabia hizo kumi za kitajiri na kuondoka na mpako mkakati wa kufanyia kazi kwenye maisha yako ya kila siku.
Rafiki, nimalize kwa kukuambia kauli hii moja muhimu sana, kinachokukwamisha siyo unachojua, bali kile usichojua. Na kwa upande wa tabia, zile tabia nzuri ambazo huzijui, ndiyo zinakukwamisha. Zijue tabia nzuri na muhimu kwa mafanikio, zifanye kuwa sehemu ya maisha yako, na kitakachobaki ni wewe kuvuna matunda ya tabia hizo nzuri.
Semina ya TABIA ZA KITAJIRI, ni semina ambayo hupaswi kuikosa kama umeamua kuwa makini na maisha yako. Jiunge sasa hivi na kundi hili la semina na ulipe ada ya tsh elfu 20 kwa namba 0717396253 au 0755953887 ili ujipatie nafasi hii adimu sana na ya muhimu kwa mafanikio yako.
Kujiunga na kundi la semina hii tumia kiungo hiki; https://chat.whatsapp.com/JvJBnoKixGrJZpZdw3shRv (kama tayari wewe ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA usijiunge na kundi hili).
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge