Hakuna kitu kimoja pekee ambacho kitakupa wewe kila unachotaka, hakipo.

Lakini wengi huwa tunaweka matumaini makubwa sana kwenye kitu fulani ambacho tunakuwa tunakitegemea.

Labda kuna kitu tunataka kufanya, ambacho tunaona ni kikubwa na kitakuwa na matokeo bora sana. Basi mawazo yetu yote yanakuwa kwenye kitu hicho na kusahau kabisa vitu vingine.

Huwa tunaacha hata kufanya vitu vingine tukiamini matokeo makubwa tutakayoyapata kwenye kile tunachotegemea yatafidia kabisa vitu vingine ambavyo tungepaswa kufanya.

Lakini kama wote tunavyojua, ni vitu vichache mno ambavyo huwa vinakwenda kama tulivyopanga, vichache mno. Vitu vingi sana huwa vinakwenda tofauti na tulivyopanga.

Matokeo mengi tunayoyapata huwa siyo sawa na matarajio ambayo tulikuwa nayo.

Ndiyo maana nakukumbusha na kukusisitiza sana kwamba usiache kila unachofanya au kutegemea kwa sababu ya kitu kimoja. Hata kama unachotegemea ni kikubwa kiasi gani na unachofanya sasa ni kidogo kiasi gani.

Usikubali maisha yako yasimame kwa ahadi yoyote ile. Chochote unachotegemea, usijihesabie kama unacho mpaka pale utakapokuwa umeshakipata tayari.

Hivyo usiache mipango yako yote kwa sababu ya mategemeo fulani. Hii haimaanishi usiwe na mategemeo, bali inamaanisha kutokukubali mategemeo yako yawe kikwazo kwenye vitu vingine unavyofuata.

Huwa zipo kauli nyingi na nzuri za kutukumbusha kuhusu hili, mfano; usihesabu vifaranga kabla mayai hayajaanguliwa. Nyingine usiweke kwenye bajeti fedha unayodai kwa mwingine hata kama amekuahidi kukulipa, mpaka pale unapokuwa umeishika fedha mkononi ndiyo unaweza kuipangia bajeti.

Haijalishi una mipango na mategemeo makubwa kiasi gani, vitu vingine unavyofanya na unavyopaswa kufanya inabidi viendelee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha