Wahenga walisema debe tupu haliachi kuvuma.

Wakimaanisha ya kwamba ukiona kitu kinapiga kelele basi jua kwa hakika ndani yake kuna utupu.

Vitu vyote vyenye kelele havina nguvu, na vile vyenye nguvu havina kelele.

Chukua mfano wa nguvu kubwa sana zilizopo hapa duniani, huwa hazina kelele, lakini huwa tunaona madhara yake, ambayo ni makubwa sana.

Angalia nguvu ya mvutano, nguvu ambayo inavuta vitu vyote kwenye dunia, ni nguvu kubwa sana ambayo madhara yake tunayaona kila siku, lakini hatusikii kelele zake. Ukirusha jiwe juu linarudi chini, hata ulirushe kwa nguvu kiasi gani. Ni nguvu hii ndiyo inayotuzuia sisi tusiweze kuruka juu sana kama ndege.

Angalia pia nguvu ya joto, hutasikia kelele zake lakini madhara yake utayaona pale utakapokutana na nguvu hii. Weka mkono wako kwenye nguvu hii ya joto na utayapata maumivu makali sana, pamoja na hata kuharibika kwa mkono wako, lakini hutazisikia kelele.

Hata kwenye maji, maji yaliyotulia sana ni maji yenye kina kirefu, na haya ni maji ambayo yana nguvu kubwa sana. Ukiona maji yana kelele na mawimbi mengi, jua hayo hayana kina kirefu.

Rafiki, haya yote yanatukumbusha umuhimu wa kutumia nguvu badala ya kelele. Kwa sababu tunaishi kwenye zama ambazo kelele inaonekana kama ndiyo nguvu, kitu ambacho siyo sahihi.

Nguvu kubwa ipo kwenye utulivu, hivyo kwa kadiri unavyoweza kuwa na utulivu mkubwa, ndivyo unavyoweza kuwa na nguvu kubwa kwenye maisha yako.

Kwenye kila unachofanya, tengeneza utulivu wa hali ya juu, kifanye kwa umakini na madhara yake yataonekana kwa watu. Usikazane na kelele, zinaweza kukutambulisha kwa watu haraka, lakini baadaye kila mtu atajua kwamba ulichonacho ni kelele tu na hakuna nguvu kubwa.

Kazana kutengeneza nguvu kubwa na yenye madhara, na siyo kelele nyingi zisizokuwa na mpango wowote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha