Watu wengi wamekuwa wakitafuta kitu kimoja pekee ambacho kitayabadili sana maisha yao.

Wanaamini kuna kitu kimejificha mahali, ambapo wakikijua au kukipata basi wataweza kupata kila wanachotaka.

Wengi itafuta kitabu kimoja pekee ambacho wakikisoma kitabadili sana maisha yao.

Wengine wanatafuta wazo moja pekee la biashara ambalo wakilitekeleza maisha yao yatakuwa bora.

Wapo pia wanaomtafuta mtu mmoja, ambaye huyo atawawezesha kuwa na maisha bora sana.

Yote haya ni kujidanganya rafiki, na kukwepa kazi unayopaswa kuweka ili kufanikiwa.

Hakuna kitu kimoja pekee ambacho kitabadili maisha yako, na hata kama kipo, itabidi kwanza upitie vitu vingi kabla hujakutana na hicho kimoja.

Hakuna kitabu kimoja pekee ambacho ukikisoma utajua kila unachopaswa kujua ili kufanikiwa. Utahitaji kupitia vitabu vingi, na huko ujifunze mengi ambayo utayakusanya pamoja na kuja na msingi muhimu kwako.

Kama yupo mtu mmoja ambaye ukikutana naye basi maisha yako yatabadilika kabisa, itakuchukua kukutana na watu wengi mpaka pale utakapomkuta huyo muhimu.

Kwa kifupi rafiki, usitafute njia ya mkato, usitake kurahisisha mambo, weka kazi unayopaswa kuweka ili kufanikiwa. Itakuchukua vitu vingi mpaka kuweza kupata kile unachotaka. Kuwa mvumilivu na weka juhudi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha