Rafiki yangu mpendwa,

Watu husema ya kwamba kauli zinaumba. Kile unachofikiri na kusema muda mrefu, ndiyo kinachotokea kwenye maisha yako.

Hapo ulipo sasa ni matokeo ya fikra ambazo umekuwa nazo kwa muda mrefu na kauli ambazo umekuwa unazitumia.

Na linapokuja swala la fedha, zipo kauli nyingi ambazo umekuwa unatumia na zinachangia wewe kubaki kwenye umasikini. Kauli hizo zinatukuza umasikini kama vile ni kitu kizuri na kuona utajiri kama ni kitu kibaya.

Rafiki, kama lengo lako ni kuwa tajiri kwenye maisha yako, basi lazima kwanza uukubali utajiri, uupende utajiri na uuthamini utajiri. Huwezi kupata utajiri kama kila siku unautukuza umasikini.

kauli hasi kwenye fedha

Hapa kuna kauli nane kuhusu fedha ambazo umekuwa unazitumia sana, sasa nataka uziache mwaka 2018 ili unapoanza mwaka 2019 uweze kupiga hatua kubwa kifedha.

  1. Vyuma vimekaza.

Kauli ya kwanza kabisa unayopaswa kuiacha mwaka 2018 ni kauli ya vyuma vimekaza. Hii imekuwa kauli maarufu tangu raisi wa awamu ya tano aingie madarakani. Kutokana na mifumo mingi kubadilika, wale waliozoea kupata fedha kirahisi hawapati tena na hivyo kilio kimekuwa na vyuma vimekaza.

Sasa iwe vyuma vimekaza kweli au la, hii siyo kauli ambayo wewe unapaswa kuitumia. Usikiri vyuma kukaza kwako. Chagua tatizo walilonalo watu unaloweza kulitatua na utalipwa kwa kile unachofanya.

Mwaka 2019 angalia fursa za kutatua matatizo ya watu na utaweza kuongeza sana kipato chako.

  1. Fedha siyo kila kitu.

Usemi huu ni maarufu sana kwa wengi, hasa masikini, kwamba usijisumbue sana na fedha kwa sababu fedha siyo kila kitu. Hii kauli siyo sahihi kwa asilimia 100, ni kweli kuna vitu muhimu kwenye maisha ambavyo tunavipata bura, kama hewa tunayopumua. Lakini ukiwa mgonjwa na huwezi kuvuta hewa mwenyewe, utauziwa hewa hiyo kwa bei ya juu sana.

Usitumie kauli hii ya fedha siyo kila kitu, kiri kwamba fedha ina mchango mkubwa sana kwenye maisha yako na kazana kuipata ili maisha yako yawe bora.

Vitu kama mahusiano yako na wengine unaweza kuona havihitaji fedha, lakini unapokuwa huna fedha ndiyo unagundua ni vigumu kiasi gani kuendesha mahusiano yako na wengine.

  1. Fedha haiwezi kununua furaha.

Je umasikini unanunua furaha? Kama jibu ni hapana basi acha kulinganisha fedha na furaha. Furaha ni matokeo ya kuwa na maisha bora, na fedha inakuwezesha kuwa na maisha bora.

Na pamoja na yote hayo, ni bora usiwe na furaha ukiwa ndani ya nyumba na una chakula, kuliko ukawa huna furaha ukiwa umelala nje na una njaa.

Acha kutumia kauli hii mwaka 2019.

  1. Kazi ya fedha ni kutumia.

Hivi ndivyo wengi wanavyotengeneza mahusiano yao na fedha, wakizipata watazitumia mpaka ziishe ndiyo waweze kutulia.

Hupaswi kutumia kila fedha unayoipata mpaka iishe, na kwa hakika unapaswa kuweka akiba na kuwekeza kabla hata hujaanza kutumia fedha uliyonayo.

Acha kujiambia kazi ya fedha ni matumizi, au kutumia kauli kama tumia fedha ikuzoee. Kila fedha unayopata weka fungu fulani pembeni kwa ajili ya akiba na uwekezaji kabla hujaanza kutumia.

  1. Sisi ni watu masikini.

Rafiki yangu, kama kuna kitu kimoja unachopaswa kukikataa kwa mwaka 2019 basi ni kukiri umasikini. Usikiri kwa kinywa chako kwamba wewe ni mtu masikini au mtu mnyonge, utaendelea kubaki kwenye hali hiyo.

Hata kama huna fedha, usijiite masikini, badala yake jiite tajiri mafunzoni. Tumia kauli chanya kuhusu fedha na utajiri na hilo litakaribisha fedha kwako zaidi na zaidi.

  1. Kila mtu hawezi kuwa tajiri.

Wengi huamini kwamba kila mtu hawezi kuwa tajiri, kwamba kuna wachache wametengewa utajiri na wengi kubaki kwenye umasikini.

Rafiki, hata kama hili ni kweli, lakini kwa nini uwe wewe. Waache wengine wachague kukaa upande wa umasikini, lakini siyo wewe.

Wewe unaweza kuwa tajiri, bila kujali umetokea wapi au wengine wapo kwenye hali gani.

  1. Matajiri wana roho mbaya.

Huu ni kama wimbo wa taifa kwa masikini, na ndiyo kitu pekee kinachowapa faraja kwamba hata kama hawana fedha basi angalau wana roho nzuri.

Rafiki, matajiri wa kweli hawana roho mbaya, na fedha haina uhusiano wowote na roho mbaya. Roho mbaya ni tabia ya mtu na masikini na matajiri wote wana roho mbaya.

Kama matajiri wana roho mbaya, basi hiyo inapaswa kuwa hamasa kwako kuwa tajiri mwenye roho nzuri ili uweze kufanya makubwa kwenye jamii yako.

  1. Fedha ni ngumu.

Kamwe usikiri kwamba fedha ni ngumu kupatikana au inabidi uumie ndiyo uipate. Jua fedha ni mabadilishano ya thamani, angalia thamani unayoweza kuitoa kwa wengine na wao watakupa fedha.

Ukikiri fedha ni ngumu, utakata tamaa na kushindwa kutoa thamani kwa wale wenye uhitaji.

Kiri fedha ni matokeo ya thamani na kazana kuzalisha thamani zaidi ili kupata fedha zaidi.

Rafiki, kauli hizo nane kuhusu fedha ziache kabisa mwaka 2018 na unapokwenda kuuzana mwaka 2019 anza ukiwa na mtazamo chanya kuhusu fedha na utajiri.

Kabla hujaondoka nina zawadi kubwa sana kwako ya mwaka mpya 2019;

KARIBU KWENYE SEMINA YA TABIA ZA KITAJIRI.

Nachukua nafasi hii kukukaribisha na kukukumbusha kuhusu semina ya TABIA ZA KITAJIRI.

Kwenye semina hii ya TABIA ZA KITAJIRI, utajifunza tabia kumi za kuishi kwenye kila siku ya maisha yako ambazo zitakuwezesha kufikia utajiri na mafanikio makubwa.

Semina hii itaendeshwa kwa njia ya mtandao wa wasap, hivyo unaweza kushiriki ukiwa popote.

Semina hii itaanza tarehe 03/01/2019 na kumalizika tarehe 13/01/2019 zitakuwa siku kumi za kupata nondo kumi za moto ambazo nitaweka msingi muhimu sana wa mafanikio makubwa na utajiri kwenye maisha yako.

Kuna njia mbili za kuweza kushiriki semina hii;

Njia ya kwanza ni kwa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, hivyo kama tayari wewe ni mwanachama moja kwa moja unapata nafasi ya kushiriki semina hii. Na kama bado hujawa mwanachama, unaweza kujiunga sasa kwa kulipa ada ya mwaka ambayo ni tsh laki moja (100,000/=) na kupata nafasi ya kushiriki semina pamoja na kuendelea kupata mafunzo mengine kwa kipindi cha mwaka mzima.

Njia ya pili ni kujiunga na kundi maalumu la semina hii, hili ni kundi kwa wale ambao siyo wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA na kwa sasa hawawezi kulipa ada na kujiunga. Hawa watapata nafasi ya kushiriki semina hii kwa kulipia tsh elfu 20 pekee (20,000/=). Kwa kulipa ada hiyo unapata nafasi ya kupata mafunzo haya ya semina ya TABIA ZA KITAJIRI.

Ili kufanya malipo ya kushiriki semina, iwe ni kwa kuwa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA au kujiunga na kundi maalumu, lipa ada yako kwa namba zifuatazo; mpesa 0755 953 887 au tigo pesa/ airtel money 0717 396 253. Majina ya namba hizo ni AMANI MAKIRITA. Ukishatuma ada, tuma ujumbe wenye majina yako kwa njia ya wasap namba 0717396253.

Kama kuna zawadi moja unayoweza kujipa kwa mwaka 2019 ambayo miaka mingi ijayo utajishukuru sana, basi ni wewe kushiriki semina hii ya TABIA ZA KITAJIRI.

Pia unaweza kumlipia mtu wa karibu kwako akaweza kujifunza na kuyabadili kabisa maisha yake kwa mwaka 2019. Mlipie tsh elfu 20 ili aweze kuingia kwenye kundi maalumu la semina hii na ajifunze.

Kamilisha malipo yako leo ili uweze kupata nafasi hii ya kipekee sana ya kupata maarifa sahihi ya kujijengea tabia sahihi zitakazokufikisha kwenye utajiri na mafanikio makubwa.

Rafiki yangu, nakusisitiza tena, usipange kukosa semina hii, nimekupa kila njia ambayo itakuwa rahisi kwako kushiriki semina hii, ni wewe tu kuitumia.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge