Hongera sana rafiki yangu mpendwa kwa siku hii mpya kabisa ya leo.
Ni ukurasa mwingine mpya kwenye kitabu cha maisha yetu ambapo tumepata nafasi nyingine ya kukiandika kitabu hiki kwa vile tunavyotaka sisi wenyewe.
Kwa kuitumia siku hii ya leo vizuri, kwa kuweka juhudi kubwa na kusimamia vizuri muda wetu, tunaweza kufanya makubwa sana kwenye siku hii.
Msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA ndivyo vinavyotuwezesha kufanya makubwa sana leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari AMINI LAKINI THIBITISHA…
Rafiki, mtu wako wa karibu sana, akikupa fedha kama zawadi, na kukuambia hiki ni kiasi fulani cha fedha, bado utazihesabu. Japokuwa ni zawadi mtu amekupa, na hata kama hazijatimia kiasi alichokuambia bado ni zawadi, ila unathibitisha kiasi hicho.
Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwenye kila eneo la maisha yetu, pamoja na kuwaamini sana wale tunaojihusisha nao, bado tunapaswa kuthibitisha vitu vingi wanavyotuambia au kufanya.
Matatizo mengi ambayo watu wanaingia kwenye maisha yao, yanatokana na kuamini pasi na kuthibitisha.
Watu wanapenda kuchukua maneno ya watu kama yalivyo na kuyaamini moja kwa moja.
Hata wale wanaotapeliwa na kulaghaiwa, ni matokeo ya kuamini bila ya kuthibitisha. Mtu anakuwa amepewa maneno matamu na mazuri kiasi cha kuyaamini sana na kuona hakuna haja ya kutaka uthibitisho zaidi. Na hapo ndipo wanapofanya maamuzi ambayo yanawagharimu sana.
Rafiki, uweke kuwa msimamo wako kwamba kabla hujafikia maamuzi fulani, lazima kwanza uwe umethibitisha wewe mwenyewe.
Pamoja na mtu kukueleza vizuri, bado ni muhimu wewe uthibitishe.
Na kama unapotaka kuthibitisha mtu anakuambia haina haja, unapoteza muda au unaikosa fursa, basi nusa harufu ya uongo au utapeli unaotaka kufanyiwa hapo.
Rafiki, ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kuamini lakini kuthibitisha kwanza kabla ya kufanya maamuzi muhimu.
#AminiLakiniThibitisha, #HarakaItakuponza, #UsifanyeMaamuziHaraka
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha