Huwa tunatamani sana kuwa na maisha ambayo hayana changamoto yoyote.

Maisha ambayo tunapata kila tunachotaka kwa namna tunavyotaka na wakati tunaotaka.

Maisha ambayo hayana misukosuko, kila kitu kinakwenda vizuri kabisa.

Japo hii ni ndoto nzuri, lakini ikiwa kwenye uhalisia ni hatari sana.

Hakuna maisha hatari na mabovu kama ambayo mtu hakutani na changamoto yoyote.

Pale mtu anapopata kila anachotaka kwa namna anavyotaka, pale ambapo hakutani na changamoto yoyote, mtu huyo anaacha kukua, anadumaa na maisha yanakuwa mabovu na magumu sana kwake.

Kila mtu anahitaji kukutana na changamoto zaidi kwenye maisha yake ili kukuza zaidi. Na pia changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kwenye maisha huwa zinakuja na fursa ndani yake.

Kila unapokutana na changamoto, kwanza kabisa unajifunza, kitu ambacho hapo awali hukukijua, pili kwa kujifunza huko unakutana na fursa ambayo awali hukuwahi kukutana nayo.

Unapokosa kile unachotaka, kwanza kabisa unajifunza thamani yake, na pili unajua ipi njia sahihi ya kukipata, kwa kuwa njia uliyozoea kutumia haijakupatia.

Usitake maisha yasiyokuwa na changamoto, badala yake kazana kuwa imara ili uweze kukabiliana na kila aina ya changamoto.

Ishi maisha ya kusudi lako, maisha ambayo kila siku kuna hatua kubwa zaidi za kupiga na ondoka kwenye maisha ya mazoea, ambayo yanakufanya uwe kwenye gereza ulilojitengenezea mwenyewe.

Kama kuna kitu unahitaji zaidi kwenye maisha yako ili kufanikiwa basi ni changamoto. Kwa sababu hizi zinakukomaza na kukuonesha vitu bora ambavyo huwezi kuviona kama hujaingia kwenye changamoto.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha