“What is the fruit of these teachings? Only the most beautiful and proper harvest of the truly educated—tranquility, fearlessness, and freedom. We should not trust the masses who say only the free can be educated, but rather the lovers of wisdom who say that only the educated are free.” – EPICTETUS, DISCOURSES, 2.1.21–23a

Ni siku nyingine mpya na ya kipekee sana kwetu rafiki.
Nafasi nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa mwongozo wetu wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA pamoja na msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA tuna nafasi nzuri ya kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari ELIMU NI UHURU…
Kama unataka utulivu wa akili,
Kama unataka ujasiri,
Na kama unataka uhuru wa kweli kwenye maisha yako,
Basi hivi vyote ni zao la elimu.
Elimu ndiyo njia ya uhakika ya kujijengea uhuru kwenye maisha yako.

Kwa kadiri unavyojua zaidi, ndivyo unavyokuwa huru zaidi.
Kwa kadiri unavyokuwa na uelewa mkubwa kuhusu wewe, ndivyo unavyokuwa na wigo mpana wa kufanya mengi.
Kwa kadiri unavyojua zaidi kuhusu kile unachofanya, ndivyo unavyoweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu zaidi. Na unapofanya kwa ubora zaidi, ndivyo unavyojijengea uhuru zaidi.

Kama kuna kitu kimoja unachopaswa kukipa kipaumbele kwenye maisha yako basi ni elimu, hasa ile elimu binafsi ya kujifunza na kujisomea yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.
Usikubali usumbufu wa dunia ukuzuie kupata elimu muhimu itakayokupa uhuru wa maisha yako.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kuweka kipaumbele kwenye elimu na kujifunza ili uzidi kuwa huru zaidi.
#ElimuNiUhuru, #SomaVitabu, #JifunzeVituVipya

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha