Kila mtu anapenda kupiga hatua kubwa kwenye maisha yake na wengi wanafika mpaka hatua ya kupanga kufanya makubwa.

Lakini inapofika kwenye utekelezaji, wengi sana hushindwa kutekeleza. Wengi huishia kuja na sababu kwa nini hawawezi kutekeleza sasa.

Na sababu zimekuwa hazikosekani, kuanzia hali binafsi, mazingira, hali ya hewa, hali ya uchumi na kadhalika.

Ukisikiliza sababu za wengi unaweza kufikiri ni sahihi kabisa na hata kuwaonea huruma kwa namna walivyo kwenye hali ngumu. Lakini ukweli ni kwamba sababu hizo huwa zinakuwa zimeficha kitu nyuma yake.

Nyuma ya sababu za kutokufanya kitu umejificha ukweli kwamba watu wengi hawapendi kujitesa na kuumia ili wapate wanachotaka. Wengi wanafikiri ipo namna ya kupata wanachotaka bila ya kuumia.

Hivyo wanapojaribu na kugundua kuna maumivu, wanajipa sababu kwa nini kwa sasa hawawezi kufanya na inabidi wasubiri kwanza.

Chukua kila sababu unayojipa na utaona namna unavyoficha ukweli halisi.

Mfano unataka kuanza biashara lakini unasema huna mtaji, hivyo unasubiri kwanza. Hiyo siyo sababu halisi. Sababu halisi ni haupo tayari kuumia kwa kuanza na biashara ndogo zisizohitaji mtaji, haupo tayari kuumia kwa kuweka sehemu kubwa ya kipato chako kama akiba ili uwe mtaji.

Ni mpaka pale unapoikubali sababu halisi na kuifanyia kazi ndiyo unaweza kutoka pale ulipokwama sasa. Kama hutaikabili sababu ya kweli, utaishia kujidanganya na hakuna hatua kubwa utakayoweza kupiga kwenye maisha yako.

Acha kujidanganya sasa, kila unapojiambia huwezi kufanya kitu fulani, jiulize sababu halisi ni ipi na kabili sababu hiyo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha