Watu ambao hawana matumizi mazuri na akili zao, huwa wanatafuta njia ya kuzishughulisha lakini isiyo na maana.
Kwa kuwa akili huwa haiwezi kukaa tupu bila ya kuwa na majukumu yoyote, usipoipa majukumu ya kufanyia kazi, yenyewe itatafuta majukumu ya kufanyia kazi.
Usipokuwa na kitu muhimu unachofikiria, fikra hasi na hofu vitakutawala muda wote.
Usipokuwa na mipango unayoifikiria, akili itatafuta mipango ambayo haina umuhimu na kujihusisha nayo.
Akili yako haipendi kukaa na upweke, hivyo itakazana mpaka kupata kitu cha kufanya.
Hii ndiyo naiita kucheza akili au kucheza karata. Kwamba unaweza kucheza akili yako kwa kuitumia kwa yale mambo muhimu kwako, au unaweza kucheza karata kwa kutumia nguvu yako kubwa ya akili kwa vitu vidogo vidogo kama michezo ya karata na mingineyo.
Ukishaona akili yako inakimbilia kwenye michezo, jua hakuna kikubwa unachofanya na fikra zako na hivyo zinatafuta mahali pa kujipa kazi hata kama siyo kazi bora.
Kila wakati hakikisha akili yako inakuwa na kitu inachofanyia kazi ili iwe na manufaa kwako. Kama ambavyo usemi maarufu unasema, akili iliyo tupu ni karakana ya uovu. Epuka kujiweka kwenye hali ya kuruhusu akili yako kuwa karakana ya uovu. Ipe kazi na itumie vizuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,