Rafiki yangu mpendwa,

Maisha ya mafanikio na yaliyokamilika lazima yawe na vitu vitatu muhimu sana. Vitu hivyo ni afya bora, fedha na hekima. Bila ya vitu hivi vitatu maisha hayawezi kuwa yamekamilika.

Na ukiangalia kila tunachopigania kwenye maisha yetu ya kila siku ni vitu hivyo vitatu.

Tunakazana kula vizuri na hata kwenda hospitali ili afya zetu ziwe imara, maana bila ya afya imara hatuwezi kufanya kazi zetu.

Tunaamka asubuhi na mapema kuwahi kwenye kazi na biashara zetu ili kupata fedha, kwa sababu bila ya fedha maisha yetu hayawezi kwenda.

Kadhalika tunakwenda shule kujifunza na pia tunanunua vitabu vya kujisomea ili kuongeza uelewa wetu na kwa njia hii tunajijengea hekima zaidi kwenye maisha yetu.

Sasa mwaka huu 2019 ni mwaka ambao sisi wanamafanikio tunaongozwa na maneno hayo matatu, AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA.

key2success

Na kwenye makala hii ya leo, nakwenda kukushirikisha ni jinsi gani unavyoweza kupata vitu hivyo vitatu kwa mwaka huu 2019 na miaka mingine ijayo.

Karibu ujifunze na uchukue hatua ili kuweza kuyaboresha maisha yako zaidi.

AFYA.

Afya ndiyo mtaji wa kwanza na muhimu sana kwenye maisha yetu, bila ya afya bora na imara huwezi kufanya chochote kikubwa kwenye maisha yako. Afya unaweza kuichukulia kirahisi sana unapokuwa nayo, lakini ukishaipoteza gharama zake ni kubwa sana.

Mwaka 2019 tunakwenda kuweka juhudi kubwa katika kujenga na kuboresha afya zetu. Na tutafanya hili kwa kuzingatia mambo matatu muhimu; KULA vyakula vya afya, KUFANYA MAZOEZI ya mwili na kupata muda wa kutosha wa KUPUMZIKA. Kwa kuzingatia vitu hivi vitatu kwa mwaka huu 2019, tunakwenda kuimarisha sana afya zetu.

KULA VYAKULA vya kiafya kwa kuepuka sukari, kupunguza wanga na kuongeza zaidi mbogamboga, matunda, mafuta na protini. Sumu namba moja kwenye afya zetu ni wanga na sukari, ukiweza kudhibiti hili utakuwa na afya bora.

KUFANYA MAZOEZI, kila siku fanya mazoezi ya kukimbia kwa angalau nusu saa. Mazoezi ya kukimbia ni mazoezi bora kabisa na yasiyo na gharama kwako. Hakikisha unafanya haya kila siku.

KUPUMZIKA, pata muda wa kutosha wa kulala kulingana na uhitaji wa mwili wako. Kwa wastani binadamu tunahitaji masaa 6 mpaka 8 ya kulala kwa siku. Jua mwili wako unahitaji kiasi gani na kila siku upe muda huo. Hili litakufanya uwe imara na kuweza kuweka juhudi kwenye shughuli zako.

Ukizingatia hayo matatu kila siku, mwaka huu 2019 utakuwa wa tofauti kabisa kwako.

UTAJIRI.

Fedha ni sehemu muhimu sana ya maisha yetu, ukiondoa pumzi ambayo kila mtu anaipata bure, kila kitu kinahitaji fedha. Na hata hiyo pumzi unapoumwa inaacha kuwa bura na unaanza kuilipia. Fedha ni hitaji muhimu sana kwenye maisha yetu, kwa sababu ndiyo inatuwezesha kupata kila tunachotaka.

Mwaka huu 2019 tunakwenda kuweka kipaumbele kikubwa kwenye fedha, kwa kuzingatia maeneo haya matatu muhimu sana kwenye fedha. Kuongeza KIPATO chetu kwa kutoa thamani zaidi kwa wengine, Kudhibiti MATUMIZI yetu kwa kuweka vipaumbele na kuacha mashindani yasiyo muhimu na kuweka akiba na KUWEKEZA, sehemu ya kumi ya kila kipato tunapaswa kuiweka akina na kuwekeza maeneo ambayo yanazalisha zaidi.

KIPATO; ongeza kipato chako kwa kutoa thamani zaidi, kujituma zaidi na kuwafikia wengi zaidi. Kama umeajiriwa tekeleza majukumu mengi zaidi na magumu zaidi. Kama unafanya biashara wafikie wateja wapya na wengi zaidi. Fanya zaidi ya ulivyozoea kufanya huko nyuma na kipato chako kitaongezeka.

MATUMIZI; Dhibiti sana matumizi yako, peleka fedha zako kwenye yale mambo ambayo ni muhimu pekee kwenye maisha yako, kama kitu siyo muhimu, achana nacho. Matumizi huwa yana tabia ya kukua kadiri kipato kinavyokua, usipoyadhibiti yatakurudisha nyuma.

UWEKEZAJI; Hutakuwa na nguvu za kufanya kazi kama unavyofanya sasa  miaka yako yote. Hivyo unahitaji kuifanya fedha yako ikufanyie kazi na kukiingizia kipato. Na hapa ndipo uwekezaji unapokuwa muhimu. Weka akiba na wekeza akiba hiyo kwenye maeneo ambayo yanazalisha zaidi kwa baadaye.

HEKIMA.

Bila ya hekima, fedha na afya tunazopigania kuwa nazo, zitatupoteza kabisa. Hekima ndiyo inayotuongoza vizuri kwenye maisha yetu, ndiyo inayotuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwetu ambayo yanafanya maisha yetu yawe bora zaidi.

Mwaka 2019 tunakwenda kuweka nguvu kubwa kwenye kujijengea hekima zaidi. Tunakwenda kufanya hivi kwa KUSOMA zaidi vitabu, kujifunza kupitia uzoefu na makosa ya WENGINE na pia KUTAFAKARI kwa kina kila uzoefu na makosa ambayo tumewahi kuyafanya ili tusiyarudie tena.

KUSOMA; kila siku ya maisha yako, soma angalau kwa dakika 30, na soma vitabu vinavyoongeza maarifa na uelewa wako kwenye kile unachofanya na hata maisha kwa ujumla. Tenga na linda sana muda huu wa kujisomea, ndiyo utakaokutoa hapo ulipo sasa na kukufikisha mbali zaidi.

UZOEFU WA WENGINE; chagua watu ambao utajifunza kupitia wao, hawa tunawaita menta. Unapaswa kuwa na mtu ambaye unataka kufikia hatua ambazo amefikia yeye, kisha kujifunza kila kitu kuhusu yeye. Kama yupo hai na yupo karibu unaweza kutafuta nafasi ya kuonana naye. Na kama yupo mbali huwezi kumfikia au alishafariki basi jifunze kupitia maandiko yake na hata maandiko yaliyoandikwa kuhusu wewe. Mazuri aliyofanya na pia jifunze makosa aliyoyafanya ili uweze kuyaepuka.

KUTAFAKARI; Unapaswa kuwa na muda wako mwenyewe, muda wa kutafakari, kuyatafakari maisha yako na kutafakari kila unachofanya, kuanzia ulikotoka, ulipo sasa na kule unakokwenda. Kila mwisho wa siku yako tafakari kila hatua uliyochukua kwenye siku hiyo na angalia wapi umefanya vizuri, wapi umekosea na wapi unahitaji kurekebisha na kuboresha zaidi. Majibu ya maswali mengi uliyonayo kuhusu maisha tayari unayo, ni wewe kutafakari na kujisikiliza na utapata majibu mengi sana.

Rafiki, kwa maneno haya matatu yanayokwenda kutuongoza 2019, na kama tutachukua hatua sahihi, mwaka 2019 unakwenda kuwa mwaka bora na wa kipekee sana kwetu.

Kwa muhtasari na ili uondoke na hatua za kuchukua 2019, haya ndiyo maneno matatu ya kutuongoza na hatua za kuchukua kwenye kila eneo;

AFYA; KULA, MAZOEZI, KUPUMZIKA.

UTAJIRI; KIPATO, MATUMIZI, UWEKEZAJI.

HEKIMA; KUSOMA, UZOEFU, MAKOSA.

Ni hayo muhimu sana rafiki yangu katika kuhakikisha mwaka huu 2019 unakuwa bora na wa kipekee sana kwetu.

Endelea kunifuatilia kwa karibu rafiki, ipo zawadi kubwa sana ninayokuandalia ya kwenda kuishi kwa msingi huu wa AFYA, UTAJIRI na HEKIMA kwa mwaka huu 2019. Nakwenda kutoa nafasi za kufanya kazi kwa karibu na watu wachache ambao wamejitoa kweli na wanataka kupiga hatua kwenye maeneo hayo matatu. Kama unataka kupata nafasi hii, endelea kunifuatilia, nitatoa nafasi hizi siku siyo nyingi.

NB; KAMA HUTAKI KUKOSA NAFASI HII, MAANA ZITAKUWA CHACHE, TUMA UJUMBE WENYE MAJINA YAKO NA NAMNA YA SIMU WENYE MANENO “AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA” Kwenda namba 0717396253.

Kwa sasa hakikisha hukosi zawadi hii ya vitabu vya mafanikio niliyoitoa, kwa sababu itakusaidia sana kupiga hatua 2019. Kupata zawadi hii, fungua na usome hapa; Zawadi Ya Vitabu Nane (08) Vya Mafanikio Vya Kuuanza Mwaka 2019 Na Kuufanya Uwe Mwaka Bora Sana Kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge