Mwanamafanikio,
Juma la pili kwa mwaka wetu mpya 2019 limeshatuacha, na kwa maana hii upya wa mwaka ndiyo unazidi kupotea.
Na pia wengi ambao waliweka malengo makubwa kwa mwaka huu, wameshaanza kurudi kwenye maisha ya mazoea kabla hata hawajayajaribu malengo waliyojiwekea.
Tafadhali wewe usiwe mmoja wao rafiki, komaa na malengo yako kwa mwaka huu mpaka uweze kupata matokeo ya tofauti.
Na popote utakapokwama, usisite kuwasiliana na mimi, kwa sababu nipo kwa ajili yako, kukupa mwongozo na mafunzo yote muhimu ya kukuwezesha wewe kufanikiwa zaidi.
Karibu kwenye tano za juma la pili, nikushirikishe mambo matano muhimu ya kujifunza na kufanyia kazi kwenye maisha yako ili yaweze kuwa bora zaidi.
#1 NENO LA JUMA; TABIA.
Zamani watu walifikiri watu waliofanikiwa walikuwa na bahati fulani, au walifanikiwa kwa sababu ya vipaji vyao, eneo walilokuwepo au kazi na biashara walizofanya.
Lakini tafiti zote za kijamii na kisayansi zinaonesha hilo siyo sahihi. Kila aina ya tafiti inaonesha eneo moja, lenye watu wenye uwezo sawa na wanaofanya kitu kimoja, mmoja anaweza kufanikiwa sana na mwingine akashindwa.
Hivyo inaonekana kipo kitu cha ziada, ambacho kinawatofautisha waliofanikiwa na walioshindwa.
Na kwa furaha kubwa napenda kukutambulisha kitu hicho kwamba ni TABIA. Waliofanikiwa wana tabia ambazo ni za tofauti kabisa na wale ambao hawajafanikiwa. Tabia ndiyo zinawatofautisha watu, ndiyo zinawapelekea kufanikiwa au kushindwa.
Hivyo rafiki yangu, jukumu lako ni moja, kama unataka kufanikiwa, angalia ni tabia gani ambazo wale waliofanikiwa wanazo, zijenge tabia hizo kwako na utasubiri kuvuna mafanikio kama ambavyo mkulima aliyepanda mbegu, kuweka mbolea, kupalilia na kunyeshea maji anavyosubiri kuvuna mazao yake.
Mchezo mzima upo kwenye tabia, tengeneza tabia zako na utaweza kufanikiwa sana.
#2 KITABU CHA JUMA; UFUNGUO MKUU WA MAFANIKIO.
Juma la pili nimepata nafasi ya kusoma kitabu THE MASTER KEY SYSTEM kilichoandikwa na Charles Haanel. Hiki ni kitabu ambacho kinatufundisha jinsi ya kutumia nguvu kubwa iliyopo ndani yetu kuweza kupata chochote tunachotaka kwenye maisha yetu.
Nguvu hii kubwa iliyopo ndani yetu, ni fikra zetu. Kitabu hiki kinatufundisha kuhusu sheria muhimu sana kwenye mafanikio ambayo ni SHERIA YA MVUTO (LAW OF ATTRACTION). Sheria hii inasema kwamba, fikra zetu zina nguvu kubwa sana ya kuvuta kitu chochote kwenye maisha yetu. Kitu chochote ambacho kinakaa kwenye fikra zetu kwa muda mrefu ndiyo kinachotokea kwenye maisha yetu.
Hii ina maana kwamba, hapo ulipo sasa, na kila ulichonacho ni matokeo ya fikra ambazo umekuwa nazo. Sheria hii inasema hakuna kitu kinachotokea kama ajali, kila kitu kinasababishwa na fikra ndiyo kisababishi cha kwanza kwenye maisha yako.
Na ndiyo maana mwandishi anaita mfumo huu wa fikra kuwa ufunguo mkuu wa mafanikio. Kwa sababu kama utaweza kutumia vizuri fikra zako, na kuwa na zile fikra za mafanikio unayotaka muda wote, basi hakuna kinachoweza kukuzuia kupata unachotaka.
Mwandishi anasema watu wengi wanashindwa kupata wanachotaka kwa sababu hawawezi kuweka fikra moja kwa muda mrefu kwenye akili zao. Muda huu wanakuwa na fikra ya wanachotaka, muda mfupi baadaye wana fikra za kukata tamaa au za mambo mengine ambayo hayana umuhimu kwao.
Mwandishi analinganisha hili na mtu aliyepanda mbegu, lakini kila baada ya dakika 10 anaenda kuifukua kuangalia kama imeota. Zoezi hilo la kufukua kila mara linainyima mbegu fura ya kukua. Ili mbegu kukua inapaswa kuachwa kwenye utulivu kwa muda.
Kadhalika ili fikra zako zilete matokeo unayotaka, lazima ziachwe zitulie, lazima ziwepo kwenye akili yako bila ya kusumbuliwa na kwa njia hiyo zitakutengenezea mazingira ya kile unachotaka.
Mwandishi wa kitabu hiki, Charles Haanel anatambulika kama mmoja wa waasisi wa vuguvugu la maendeleo binafsi. Mmoja wa watu ambao walikuwa wakifundisha jinsi mtu anavyoweza kutumia uwezo mkubwa uliopo ndani yake na akafanikiwa sana.
Kitabu hiki kina sura 24 na hapa nakwenda kukushirikisha kitu kimoja nilichojifunza kwenye kila sura na jinsi ya kukifanyia kazi ili uweze kupata kile unachotaka kwenye maisha yako.
Karibu kwenye mfumo wa ufunguo mkuu wa mafanikio;
- Huhitaji kutafuta nguvu nje yako, nguvu tayari zipo ndani yako. Unachohitaji ni kujua nguvu ulizonazo na kuweza kuzitumia. Kila binadamu ana nguvu kubwa ya kiroho ndani yake, na nguvu hii ya kiroho ipo ndani ya fikra zake. Kama akiweza kuzitumia vizuri fikra zake, zitampa chochote anachotaka.
- Magumu tunayokutana nayo kwenye maisha ni kwa sababu ya kutokujua nini hasa tunachotaka na pia kutokujua kile kilichopo ndani yetu. Ukishajua kilichopo ndani yako na ukajua kwa hakika nini unataka, na ukapeleka fikra zako kwenye hayo, hakuna kitakachokushinda.
- Usilalamikie chochote kinachotokea kwenye maisha yako, kwa sababu umekisababisha mwenyewe na nguvu ya kukibadili ipo ndani ya fikra zako. Fikra zako ndiyo kisababishi, na yale yanayotokea kwenye maisha yako ni matokeo. Hivyo kama hujayapenda matokeo, badili kisababishi ambacho ni fikra zako.
- Dunia inaendeshwa kwa upacha, kwenye dini kuna Mungu na shetani, kwenye sayansi tuna chanya na hasi, kwenye falsafa tuna wema na uovu. Lakini yote haya ni hali ya fikra zetu. Kama fikra zikisimamiwa vizuri zinaleta matokeo mazuri, kama zisiposimamiwa zinaleta matokeo mabaya.
- Tunaishi kwenye zama za fikra, zama za ubunifu. Wanaofanikiwa ni wale ambao wanaweza kutumia fikra zao vizuri. Kwa sababu dunia imekuwa na vitu vile vile miaka yote, bali wale waliotumia fikra zao vizuri ndiyo wamenufaika zaidi na dunia. Kwa mfano umeme tulionao sasa duniani hauna tofauti na umeme uliokuwepo miaka 200 iliyopita. Lakini leo tuna vitu vingi zaidi vinavyotumia umeme kuliko miaka 200 iliyopita kwa sababu watu wametumia vizuri fikra zao na kuja na vitu vipya.
- Zipo njia kuu mbili za kuendeleza na kutumia vizuri fikra zetu. Njia hizo ni umakini na msisitizo. Unaposisitiza fikra zako kwenye kitu kimoja, na umakini wako wote ukawa pale, fikra zina nguvu ya kukupa kile unachotaka. Ukikosa sifa hizo mbili, fikra zako zitakuwa zinahamahama na hutapata unachotaka.
- Baada ya kuweka umakini na msisitizo wa fikra zako kwenye kile unachotaka, unapaswa kuwa na taswira ya unachotaka na kuiweka taswira hiyo kwenye fikra zako. Pata picha ya kile unachotaka, kama vile tayari umeshakipata, jione ukiwa ndani ya kitu hicho. Kwa kutengeneza taswira hii, akili yako ya ndani itaona ndiyo maisha yako na kutengeneza maisha ya aina hiyo zaidi.
- Kusudi kuu la maisha ni kukua na kuongezeka. Na dunia nzima kwa asili inakua na kuongezeka. Angalia kila kiumbe, kuanzia miti, wanyama na hata samaki, wanaendelea kuzaliana na kukua zaidi. Hivyo ili kufanikiwa kwenye maisha, unapaswa kuwa na fikra za ukuaji.
- Tabia uliyonayo siyo kwa bahati mbaya, bali umeijenga wewe mwenyewe kwa juhudi kubwa sana. Umekazana wewe mwenyewe kujenga tabia zote ulizonazo, kwa kuanzia kwenye fikra zako, kwa namna unavyojitambulisha ndani yako. Hivyo ili kubadili tabia, anza kubadili fikra zako na weka juhudi kujenga tabia mpya.
- Hakuna uhaba kwenye dunia, bali kuna utele. Dunia ina kila kitu kwa wingi kadiri watu wanavyohitaji. Na hata vikipungua basi itatengeneza zaidi kadiri watu wanavyohitaji. Hivyo hupaswi kufikiri kwenye uhaba bali kwenye wingi, hupaswi kuona mwingine akifanikiwa basi wewe unashindwa. Dunia ina rasilimali za kumtosha kila mtu kufanikiwa.
- Maisha yanaendeshwa kwa sheria na kanuni fulani, ukizijua na kuziishi utafanikiwa. Lakini usipozijua basi zitakuumiza. Kwa mfano dunia ina nguvu ya mvutano, ambayo inavuta kila kitu kwenye dunia. Kama hujui kanuni hii na ukajaribu kuruka kama ndege, utaanguka kwenye dunia na kuumia sana. Kanuni ipo pale na kama huijui inakugharimu.
- Unahitaji vitu vitatu ili kuweza kunufaika na nguvu ya fikra iliyopo ndani yako. Moja unahitaji kujua kwamba una nguvu ndani yako, mbili, unahitaji kuwa na uthubutu wa kujaribu kuitumia nguvu hiyo na tatu unahitaji kuwa na imani ya kutumia nguvu hiyo.
- Sisi binadamu siyo viumbe wa mwili ambao tuna roho, bali sisi ni viumbe a kiroho ambao tuna mwili. Roho ndiyo inayoongoza maisha yetu na ndiyo yenye nguvu ya fikra. Mtu anapofariki, kinachoondoka ni roho, mwili unabaki pale na unakuwa hauna nguvu ya kufanya chochote. Hivyo kama unataka kujiendeleza, endeleza roho yako, endeleza fikra zako na hizi zitakupa unachotaka.
- Ulimwengu mzima ni kitu kimoja na tunaongozwa na nguvu moja. Kila kitu kwenye ulimwengu, ukikiangalia kwa undani unagundua ni nguvu ama nishati. Jua ni nishati ya mwanga na jito, ambayo ikifika kwenye mimea inabadilika na kuwa nishati ya kikemikali, mimea ikiliwa na wanyama nishati hiyo inahamia kwa wanyama. Kila kitu kwenye dunia ni nishati, hata sisi binadamu, ukivunja miili yetu mpaka kwenye ngazi ya seli, unagundua sisi ni nishati. Hivyo ulimwengu mzima ni kitu kimoja, nishati.
- Kukua ni kupoteza, kupata kipya ni kupoteza cha zamani, hii ni kanuni muhimu sana kwenye mafanikio. Hakuna kiumbe anayekua na kubaki na vitu vya zamani, na huwezi kupata kitu kipya kama bado unang’ang’ana na vya zamani. Ili ukue unahitaji kupoteza kile ambacho tayari unacho sasa. Matatizo mengi ambayo watu wanayapata ni kutokana na kung’ang’ana na vitu vya zamani.
- Ipo kanuni kuu ya maisha kwamba kila kitu kinazaliwa, kinakua, kuzalisha na kufa. Na kanuni hii inaenda kwa mzunguko. Kwa mfano kwetu sisi binadamu, kila baada ya miaka saba, maisha yetu yanabadilika kabisa na kuwa mapya. Miaka saba ya kwanza ni ya utoto, miaka saba inayofuatia ni ya kuanza kujifunza majukumu, saba inayofuata ni ya kuanza ukuaji wa utu uzima. Miaka saba mingine ni kufikia ukuaji kamili, inayofuatia ni ya kuzalisha na kuwa na mali na familia. Miaka saba inayofuata, 35 mpaka 42 ni kipindi cha mabadiliko makubwa kimaisha. Inafuatiwa na miaka saba mingine ya kujijenga upya kwenye utu uzima.
- Vitabu vya dini vinatuambia kwamba binadamu tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Na hili lina maana kwamba tunazo sifa za uungu ndani yetu. Sifa hizi zipo kwenye fikra, mungu ana sifa ya kuumba na fikra zetu pia zina sifa ya kuumba. Kadhalika kwenye nguvu na ujuzi, fikra zetu zinajua mengi na zina nguvu kubwa. Tukiweza kuzitumia tunaweza kufanya makubwa sana.
- Usichotumia unakipoteza. Wengi hujiuliza kama fikra zetu zina nguvu sana kwa nini wengi hawazitumii. Sababu kubwa ni kwamba wengi hawajui kama wana nguvu kubwa kwenye fikra zao, na usichokijua huwezi kukitumia, na usichotumia unakipoteza. Hivyo hatua ya kwanza ya kutumia nguvu zako ni kujua zipo, na kuanza kuzitumia.
- Hofu ni matumizi mabaya ya nguvu ya fikra zako. Kwa kuwa na hofu unatumia fikra kutengeneza yale ambayo hutaki yatokee na kwa kuwa fikra zina nguvu, zinaleta hayo hayo unayofikiria. Hivyo unapaswa kuondokana kabisa na kila aina ya hofu, kwa kujua nguvu kubwa iliyopo ndani yako ya kukuwezesha kufanya chochote.
- Jukumu lako kuu kwenye maisha, na biashara pekee ambayo inalipa ni kufikiri. Wale wanaoweza kufikiri kwa kutumia akili zao ndiyo wanaokuja na vitu vipya na njia mpya za kufanya vitu na wananufaika sana. tumia nguvu yako ya fikra kufikiri na utaweza kufanya makubwa.
- Unapofikiri, unapaswa kufikiri mawazo makubwa sana. Ukifikiri kidogo nguvu iliyopo ndani yako inaleta matokeo madogo. Ukifikiri makubwa nguvu hiyo inaleta makubwa. Usiogope kufikiri makubwa, una nguvu ndani yako ya kupata chochote unachofikiri.
- Kinachotutofautisha ni kanuni ya mtetemo (law of vibration). Tumeona kwamba kila kitu duniani ni nishati, je nini kinakutofautisha wewe binadamu na mti? Ni kanuni ya mtetemo. Wewe ni binadamu kwa sababu seli zako zina mtetemo tofauti na za mti. Na hata nishati inapobadilika kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine, kinachobadilika ni mtetemo wake. Hata baina ya watu, wale wanaofanikiwa ziadi wana mtetemo wa juu kuliko wale wanaoshindwa. Fikra zetu zinaendana na mtetemo, hivyo tunapokuwa na fikra za juu tunavutia mtetemo wa juu. Unaweza kufananisha nguvu hii ya mtetemo na kutafuta mawimbi ya redio, unasikia redio fulani pale unapofikia kwenye mawimbi yake.
- Kanuni kuu ya mafanikio ni HUDUMA. Tunafanikiwa kwa kadiri tunavyowahudumia wengine, tunapata kadiri ya tunavyotoa. Hivyo kama unataka zaidi, unapaswa kutoa zaidi, kama unataka kufanikiwa zaidi unapaswa kuwahudumia wengi zaidi na kwa ubora zaidi.
- Ili kuwa huru na ili kupata chochote unachotaka, unapawa kuujua ukweli. Kumbuka kauli inayosema IJUE KWELI NAYO ITAKUWEKA HURU. Watu wengi hawapo huru kwa sababu hawajui ukweli, na usipokuwa huru huwezi kuwa na mafanikio. Ujue ukweli kwa kujua nguvu kubwa iliyopo ndani yako na pia kwa kujua umoja wa dunia, kwamba kila kitu ni nishati na tunavuta vile vitu ambavyo vipo kwenye mtetemo wa fikra zetu.
Rafiki, kanuni kuu kabisa tunayoondoka nayo kwenye kitabu hiki ni kwamba fikra zetu zina nguvu kubwa sana ya kutupa chochote tunachotaka. Tunachopaswa kufanya ni kuijua nguvu hii na kuweza kuitumia. Kwa sababu tusipoitumia tunaipoteza na tunatengeneza maisha magumu kwetu wenyewe.
Nenda kaishi nguvu kubwa iliyopo ndani yako ili uweze kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yako.
#3 MAKALA YA JUMA; MANENO MATATU YA 2019.
Rafiki, kila mwaka nimekuwa nakushirikisha maneno matatu ambayo yanatuongoza kwa mwaka mzima.
Na hivyo mwaka huu 2019 nimekuandalia maneno matatu muhimu ambayo ukiweza kuyafanyia kazi, utaweza kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa. Kwa sababu maneno matatu ya mwaka huu yamegusa maeneo matatu muhimu ya maisha yetu.
Kama hukusoma makala ya maneno matatu ya mwaka 2019, isome sasa hapa; Haya Ndiyo Maneno Matatu Ya Kutuongoza Kwa Mwaka 2019 Ili Uweze Kuwa Mwaka Wa Mafanikio Makubwa Kwetu.
Rafiki, pia nilikuandalia makala nyingine nzuri ya jinsi unavyoweza kufanikiwa kwenye maneno matatu ya mwaka 2019, unaweza kusoma makala hiyo hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kupata AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA Kwa Mwaka Huu 2019.
Soma makala hizo mbili muhimu sana kwako rafiki yangu na chukua hatua mara moja ili maisha yako yaweze kuwa bora zaidi.
#4 TUONGEE PESA; TENGENEZA GEREZA LA AKIBA.
Kila mwaka malengo ya watu yamekuwa ni kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji. Na kweli wanaweka sana akiba, wanajinyima na kuanza kutengeneza akiba zao.
Lakini haupiti muda inajitokeza dharura ambayo inawapelekea kutumia zile akiba walizokuwa wamejiwekea, hivyo wanarudi sifuri kabisa, wanakuwa hawana akiba yoyote.
Rafiki, iwe una fedha au huna, dharura hazitaacha kutokea kwenye maisha yako. Hivyo njia pekee ya kulinda akiba yako siyo kuombea usipate dharura, badala yake ni kutengeneza gereza kwa ajili ya akiba yako.
Gereza hili ni kuweka akiba eneo ambalo huwezi kuitoa hata ardhi ipasuke. Na ukishaweka huko unasahau kabisa, hivyo kama dharura itakuja, utaangalia njia nyingine za kuitatua na siyo kuangalia akiba hiyo.
Magereza ya fedha yapo mengi, unaweza kuziweka kwenye akaunti maalumu, ambayo huwezi kutoa fedha hiyo mpaka muda uliochagua uishe. Pia unaweza kufungua akaunti ya pamoja na mtu mwingine na makubaliano yakawa ni hakuna kutoa hata iweje. Pia unaweza kutumia mitandao ya simu, ukapoteza namba ya siri ya mtandao wa simu unaotumia kuweka fedha ili isiwe rahisi kwako kutoa.
Angalia njia bora kwako ni ipi na itumie, usiache akiba yako ikakaa kirahisi rahisi kiasi kwamba ukiwa na shida kidogo tu unaitumia. Iweke kwenye gereza ambalo hutaweza kuitumia kabisa.
#5 TAHAKARI YA KUFIKIRISHA; SIFA YA WASHINDI.
“Victory belongs to the most persevering.” – Napoleon Bonaparte
Ushindi unaenda kwa wale ambao ni ving’ang’anizi na wavumilivu.
Huwa tunawaangalia wale waliofanikiwa na kupenda sana kufika walipofika. Lakini sisi wenyewe kuna vitu vingi ambavyo tulishawahi kuanza kwenye maisha yetu, lakini havikutufikisha mbali, kwa sababu tulikosa ung’ang’anizi na uvumilivu.
Sasa chagua kitu kimoja au vichache unavyotaka kwenye maisha yako, kisha weka juhudi zako zote na usikate tamaa mpaka umekipata, na ninakuhakikishia utakipata. Maana washindi wote wameng’ang’ana na kupata walichotaka.
Hizi ndizo tano za juma namba mbili kwa mwaka wetu 2019, jifunze kwa kina, tafakari na ondoka na hatua za kwenda kutekeleza kwenye maisha yako.
Nikutakie kila la kheri kwenye juma namba 3 la mwaka 2019, likawe juma la kufanya makubwa kwako, juma la kujenga tabia bora, kuwa na gereza la fedha na kuwa king’ang’anizi mpaka upate unachotaka.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu