Kuna wakati tunakazana sana kupata kile tunachotaka, lakini pamoja na kuweka juhudi kubwa, hatupati kile tunachotaka. Tunafanya kile ambacho tunapaswa kufanya, kile ambacho wengine wanaopata wanafanya, lakini sisi hatupati.
Zipo sababu nyingi zinazopelekea hilo, lakini kipo kimoja kikubwa ambacho wengi huwa hawakijui.
Kitu hicho ni kutokuwa tayari kupoteza kile ambacho tayari mtu anacho. Yaani unataka kupata kitu kipya, lakini hutaki kupoteza kile cha zamani ulichonacho.
Sasa kwa sheria ya asili, huwezi kupata kitu kipya kama hutapoteza cha zamani ulichonacho. Ni sawa na kuwa na kikombe ambacho kimejaa maji halafu unataka kutumia kikombe hicho kunywa chai. Ni lazima uyaondoe kwanza maji ndiyo upate nafasi ya kuweka chai.
Kwenye kila unachotaka kwenye maisha yako, angalia ni kipi ulichonacho sasa, ambacho tayari umeshakizoea na hutaki kukipoteza. Hicho ndiyo kinakuzuia usipate kile unachotaka.
Kupata chochote kipya, lazima uwe tayari kupoteza kile cha zamani ulichonacho. Kuendelea kung’ang’ana na kile ulichozoea hutaweza kupokea kipya unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,