“We control our reasoned choice and all acts that depend on that moral will. What’s not under our control are the body and any of its parts, our possessions, parents, siblings, children, or country—anything with which we might associate.”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 1.22.10
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana tuliyoipata leo.
Tunapaswa kushukuru sana kwa nafasi hii, na pia kuhakikisha tunaitumia vizuri kwa sababu tunaweza tusipate nafasi nyingine.
Kwa kufuata msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tutakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari WIGO WA UDHIBITI WAKO…
Pamoja na kujifunza sana kwenye ustoa kuhusu upacha wa udhibiti, bado mara kwa mara tunasahau ukubwa wa wigo wetu wa udhibiti.
Mara kwa mara tunajikita tukitoka nje ya wigo huu, tukitaka kudhibiti vitu ambavyo havipo kwenye ndani ya wigo wetu.
Asubuhi hii, kupitia Mstoa Epictetus tunajikumbusha yaliyo ndani ya wigo wetu wa udhibiti na yaliyo nje ya wigo huu.
Kilicho ndani ya wigo wetu wa udhibiti ni fikra zetu na matendo yote yanayotokana na maamuzi yetu. Kwa kifupi tunaweza kusema kitu pekee kilicho ndani ya udhibiti wetu ni akili na fikra zetu.
Vingine vyote vipo nje ya wigo wetu wa udhibiti.
Hata mwili wako hauko ndani ya udhibiti wako, unaweza kupata maradhi muda wowote ambayo hukupanga kuwa nayo na yakakusumbua sana.
Kadhalika mali tulizo nazo, hazipo ndani ya wigo wa udhibiti wetu, tunaweza kuzipoteza muda wowote.
Ndugu zetu, watoto wetu, wazazi, wenza na wengine wote tunaojihusisha nao, hawapo ndani ya wigo wetu wa udhibiti.
Tukumbuke wigo huu muhimu kabla ya kuchukua hatua yoyote ili tusijiumize kwa kukazana kubadili tusichoweza kubadili. Na kwa kujua hili, tutajipunguzia masumbuko na kuweka muda na nguvu zetu kwenye yale hasa tunayoweza kudhibiti.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kusumbuka na yale yaliyo ndani ya wigo wako wa udhibiti na kupokea yale yaliyo nje ya wigo huo.
#UpachaWaUdhibiti #TawalaFikraZako, #JiwekeHuru
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,