Kutumia hadithi za mafanikio ya wengine kama hamasa ya wewe kufanikiwa zaidi ni kuzuri. Lakini unapaswa kuangalia zaidi ya unachoona.
Maana hadithi nyingi za mafanikio huanza na mtu alikuwa chini na baadaye yuko juu, amefanikiwa sana. Kuna vitu vingi sana hutaviona kwenye hadithi za mafanikio ya wengine, hivi ni vitu ambavyo itabidi uvitafute mwenyewe.
Kwa sababu wanaokupa hadithi hizo labda hawana muda wa kukueleza kila kitu, au hawataki kukueleza na upande wa pili ili usikate tamaa.
Hivi ni baadhi ya vitu ambavyo hutaviona wala kuvisikia kwenye mafanikio ya wengine, ni mpaka uchimbe mwenyewe ndani kuvipata.
- Muda ambao mtu ameweka mpaka kufanikiwa. Huwa tuna tabia ya kuona muda ni mdogo sana tangu kuanza na kufanikiwa. Lakini utakuwa kwa chini sana, mtu aliyefanikiwa ameweka siyo chini ya miaka kumi ya kazi mpaka kufika alipofika sasa. Utaona hili kama utatafuta mwenyewe.
- Kukatishwa tamaa, hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa ambaye hakuwahi kukatishwa tamaa kwamba anachotaka hakiwezekani au atashindwa, hakuna, na wewe hutakuwa wa kwanza.
- Kuchekwa na kudharauliwa, watu wamepewa mpaka majina mabaya, kwamba ni vichaa, wamechanganyikiwa na mengine mengi, hayo hutayaona mtu akishafanikiwa, kwa sababu wale waliokuwa wanawadharau huko nyuma sasa unakuta wanawaheshimu.
- Kuangushwa, waliahidiwa vitu vingi na wengine, lakini waliowaahidi au walikuwa wanawategemea waliwaangusha mara nyingi mno.
- Majaribu ya kukata tamaa, kila aliyefanikiwa, kuna mahali alifika na kujiambia hapa siwezi kuendelea tena, imetosha sasa na naachana na hili. Hapa ni baada ya kuweka kila walichoweza kuweka lakini bado hawapati wanachotaka. Lakini kuna sauti ndani yao iliwaambia wasukume zaidi kidogo na hapo kila kitu kikabadilika.
- Kushindwa, kama yupo mtu aliyefanikiwa ambaye hajawahi kushindwa kwenye mambo mengi huko nyuma, anakudanganya au wewe hutaki kuangalia. Kila aliyefanikiwa leo, kuna mambo mengi ambayo alishindwa huko nyuma. Lakini aliendelea kupambana, hakukata tamaa.
Rafiki, unapochagua hadithi ya mtu aliyefanikiwa kwa ajili ya kujifunza na kupata hamasa, acha kuangalia nafasi yake ya sasa, acha kuangalia mali alizonazo, ushawishi alionao.
Badala yake rudi kwenye miaka kumi ya kwanza ya safari yake, tangu alipoanzia sifuri kabia mpaka kufika pale alipo saa. Utajifunza mengi ambayo yatakusaidia kuliko hadithi za juu juu ambazo zinawahamasisha wengi, lakini wanapoanza kufanyia kazi wakakutana na kikwazo wanakata tamaa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,