“Understand at last that you have something in you more powerful and divine than what causes the bodily passions and pulls you like a mere puppet. What thoughts now occupy my mind? Is it not fear, suspicion, desire, or something like that?”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 12.19
Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ambayo tumeipata leo.
Ni fursa bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari KATA KAMBA ZINAZOVUTA AKILI YAKO….
Moja ya changamoto kubwa inayotukabili na kutuzuia kufanikiwa, ni vile vitu ambavyo vinavuta akili zetu.
Kama akili yako haiwezi kutulia sehemu moja, na kuweka umakini kwenye kile unachofanya, itakuwa adui yako badala ya rasilimali kwako.
Vipo vitu vingi ambavyo kwa makusudi vinachanganya akili zetu, vinatoa akili kwenye yale muhimu na kupeleka kwenye yale yasiyo muhimu.
Vitu kama kufuatilia maisha ya wengine, hofu, chuki, wivu na tamaa vinatumia rasilimali kubwa kwenye akili zetu lakini havina matokeo yoyote chanya.
Hapo bado hujaingia kwenye vitu vinavyotuzunguka kila siku, mitandao ya kijamii na hata watu wengine, vyote hivi vinakazana kupata sehemu kwenye akili zetu.
Kama usipokuwa mkali na kukata kabisa kamba hizi zinazovuta akili yako, kama hutachukua hatua za makusudi za kusema hapana kwa yasiyo muhimu, akili yako itaishia kuwa kibaraka na siyo mtawala.
Utaanza na kumaliza siku ukiwa umechoka, lakini ukiangalia ulichofanya huoni.
Anza leo kulinda na kutawala akili yako. Usiruhusu mawazo na fikra zozote zisizo na manufaa kutawala akili yako. Ng’oa kila aina ya magugu ya kifikra ambayo yameota kwenye akili yako. Na iachie nafasi ya kuruhusu fikra bora kuota na kumea, ambazo zitakuletea matokeo bora sana.
Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki, siku ya kukata kamba zote zinazovuta akili yako na zisizo na manufaa kwako.
#TawalaFikraZako #JuaYaliyoMuhimu, #JaliMamboYako
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha