Hii ni kauli maarufu na inayotumiwa na wengi, kwamba unapaswa kujikubali kama ulivyo.
Ni kauli nzuri yenye lengo la mtu kupata utulivu wa ndani, na kuacha kujilinganisha na wengine, maana hakuna unayeweza kulingana naye.
Lakini pia kauli hii ina madhara yake isipotumiwa vizuri.
Pale mtu anapotumia kauli hii kujiridhisha na kuacha kupiga hatua zaidi inakuwa kikwazo zaidi kwake.
Pale mtu unapojikubali kama ulivyo na kuacha kukazana kuwa bora zaidi unashinda kukua na kupiga hatua zaidi.
Unapaswa kujikubali kama ulivyo, lakini kila wakati kukazana kuwa bora zaidi. Kwa sababu kila mtu anaweza kuwa bora zaidi ya alivyo sasa, kama akiweka juhudi zaidi ya anazoweka sasa.
Hakuna aliyekamilika na hivyo kujikubali na kuridhika ulivyo ni kuchagua kurudi nyuma, kwa sababu kwenye maisha kuna kwenda mbele au kurudi nyuma, hakuna kubaki palepale.
Kila mtu anahitaji kukua zaidi, kila mtu ana nafasi ya kukua zaidi bila ya kujali kwa sasa yupo wapi. Pata njaa hii ya kukua zaidi kwenye kila hatua ya maisha yako na maisha yatakuwa bora.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,