Rafiki yangu mpendwa,

Duniani kuna makundi makuu mawili ya watu.

Kundi la kwanza ni wazalishaji, hawa ni wale wanaozalisha na kutengeneza vitu ambavyo wengine wanatumia. Hili ni kundi la watu ambao wanakaa chini, kufikiri kwa kina na kuja na bidhaa au huduma ambayo wengine wanatumia. Kwa kuzalisha kwao wanaingiza kipato zaidi. Kundi hili lina watu wachache sana.

Kundi la pili ni walaji, hawa ni wale wanaotumia bidhaa na huduma mbalimbali zinazozalishwa na wengine. Hili ni kundi ambalo linasubiri watu waje na kitu na wao watumie. Wanatumia kipato chao kulipia bidhaa na huduma zinazozalishwa na wengine. Kundi hili lina watu wengi kuliko kundi la kwanza.

Ili dunia iwe na uwiano, lazima makundi haya pia yawe na uwiano, yaani wazalishaji na watumiaji wawe na uwiano.

Lakini kwa zama tulizo sasa, na kadiri muda unavyokwenda, wazalishaji wanazidi kupungua huku walaji wakiwa wengi. Na hili limechangiwa zaidi na maendeleo ya kiteknolojia, kila siku kuna kitu kipya cha kutumia, ambacho kinachukua muda wa watu na kuwazuia kuzalisha.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Chukua mfano wa mitandao ya kijamii, kila siku kuna mitandao mipya ya kijamii na yenye ushawishi mkubwa sana wa kutumia. Mtu asipoingia kwenye mitandao hii anajikia vibaya kabisa, anaona kuna kitu kikubwa anachokikosa. Hivyo wengi wanatumia muda mwingi kwenye mitandao hii, kwa kuwa walaji, muda ambao wangeweza kuutumia kwenye uzalishaji.

SOMA; Fanya Mambo Haya 19 Pekee Kila Siku Na Mwaka 2019 Utakuwa Wa Mafanikio Makubwa Sana Kwako.

Sasa rafiki yangu, nina ushauri mzuri kwako kwa mwaka huu 2019, nakushauri mwaka huu upunguze ulaji na uongeze uzalishaji.

Hakikisha kwenye kila eneo la maisha yako, unapunguza ulaji na kuongeza uzalishaji.

Punguza kuangalia video mbalimbali na anza kuzalisha video ambazo watu wataziangalia.

Punguza kufuatilia habari mbalimbali na anza kuzalisha habari ambazo wengine watazifuatilia.

Punguza muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii kufuatilia wengine wanafanya nini, na fanya kitu kitakachowapelekea watu wakufuatilie wewe.

Mwaka 2019 punguza kuwa mfuasi na anza kuongoza, acha kuwa chini ya watu wengine na chagua watu wa kuwa chini yako.

Kwa namna dunia na teknolojia inavyokwenda, tunatengeneza kundi kubwa la watu ambao hawana fikra zozote kwenye kuzalisha bali kula. Kila wakati watu wanajiuliza teknolojia ipi mpya ya kutumia, mtandao upo wa kijamii mzuri kutembelea.

Ondoka kwenye kundi hili kubwa kwa kuweka muda wako mwingi kwenye uzalishaji. Kila mara jiulize ni nini unachoweza kuzalisha na wengine wakatumia.

Na kumbuka, ukizalisha unalipwa, ukila unalipa. Zalisha zaidi ili ulipwe zaidi. Hili liwe lengo lako kuu kwa mwaka 2019 na kuendelea.

Usikose zawadi hii nzuri sana kwako kuuanza mwaka huu 2019 kwa mafanikio makubwa, ipate hapa; Zawadi Ya Vitabu Nane (08) Vya Mafanikio Vya Kuuanza Mwaka 2019 Na Kuufanya Uwe Mwaka Bora Sana Kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge