“Tranquility can’t be grasped except by those who have reached an unwavering and firm power of judgment—the rest constantly fall and rise in their decisions, wavering in a state of alternately rejecting and accepting things. What is the cause of this back and forth? It’s because nothing is clear and they rely on the most uncertain guide—common opinion.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 95.57b–58a

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari UTULIVU NI KUSIMAMIA UNACHOAMINI…
Watu wengi wamekuwa wanakosa utulivu kwenye maisha yao kwa sababu hawawezi kusimamia kile wanachoamini.
Kila mara wanabadilika kutokana na maneno na matendo ya wengine.
Wanaamua kufanya kitu fulani, lakini wengine wanawaambia hicho siyo kitu sahihi kufanya au hawataweza na wao wanakubaliana nao na kuacha.

Mtu unachagua kufanya kitu fulani, lakini kwa kuwa wengine wanafanya tofauti na hichom basi unaacha kufanya ulichochagua na kufanya kile ambacho wengi wanafanya.

Huwa inaonekana kama kufanya wanachofanya wengi kuna usalama zaidi. Lakini ukweli ni kwamba, wengi hawajui wanachotaka hivyo nao wanafuata kile ambacho wengine wanafanya.

Njia pekee ya kupata utulivu wa akili, njia pekee ya kuweza kuchukua hatua na kusonga mbele ni kujua kile unachotaka na kuweza kukisimamia mpaka upate kile unachotaka.
Ukishachagua unachotaka, usipoteze muda wako kuangalia au kufuatilia wengine wanasema au kufanya nini. Huo ni muda ambao utakuwa umechagua kuupoteza.

Kusikikiza maoni ya wengi ah kufuata kile kinachofanywa na wengi ni kujiandaa kushindwa, kwa sababu wengi hao huwa hawana uvumilivu na wanatafuta njia za mkato ambazo huwa hazipo.
Jua unachotaka, amini kwenye uwezo mkubwa uliopo ndani yako na weka juhudi mpaka upate unachotaka.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kusimamia kile unachoamini na kuendelea na ulichochagua bila ya kujali wengine wanasema na kufanya nini.
#JuaUnachotaka, SimamiaUnachoamini, #EpukaKundiLaWengi

Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha