Huwa tunachanganya sana ujuzi na kipato, ndiyo maana wengi wanaoongeza elimu zaidi wakitegemea kipato chao kiwe kikubwa zaidi huishia kukata tamaa pale kipato chao kinaposhindwa kuongezeka, au kuongezeka kwa kiwango kidogo sana.
Kuongeza elimu au ujuzi hakukufanyi wewe ulipwe zaidi, kunakuongezea sifa tu.
Kinachokufanya wewe ulipwe zaidi ni pale unapofanya zaidi, pale unapotoa thamani kubwa zaidi ya ulivyokuwa unatoa awali.
Na hili unaweza kukifanya hata bila ya kuongeza elimu na ujuzi, lakini unapoongeza elimu na ujuzi unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kufanya zaidi.
Rafiki, hakuna atakayekulipa kwa unachojua, ila utalipwa kwa unachofanya, unachozalisha, ile thamani unayoitoa.
Kwa kuijua kanuni hii, ni sawa na kujua siri kuu ya kuweza kulipwa zaidi, mara zote ni kwa kuzalisha zaidi, kwa kutoa thamani kubwa zaidi.
Wapo wengi wanaojua sana, lakini kwa kuwa hawafanyii kazi wale wanayojua kipato chao hakiongezeki. Siyo unachojua bali unachofanya ndiyo kinagusa kipato chako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,