Mwandishi mmoja amewahi kuandika kwamba zama hizi ambazo mtu unaweza kufanya kila kitu mwenyewe, zimekuwa zama ambazo ubora wa kazi umeshuka sana.
Akitumia mfano wa sanaa na uandishi, anasema zamani msanii aliweka nguvu zako kwenye kutengeneza sanaa yake, na kazi ya masoko na kusambaza ilikuwa kazi za watu wengine, hasa zile taasisi zinazozalisha kazi zao.
Lakini sasa hivi ule ukuta umeondoka, huhitaji tena kuaminiwa na taasisi fulani ndiyo uwe msanii au mwandishi. Unachohitaji ni kuanza mwenyewe kazi yako na ukiikamilisha basi unaisambaza mwenyewe.
Hivyo sasa majukumu yameongezeka, msanii au mwandishi anahitaji kuzalisha kazi yake, halafu tena huyo huyo aitafutie wateja kwa maana ya kuitangaza na pia kuisambaza kwa wateja wake.
Sasa msanii au mwandishi asipokuwa makini hapa, anaweza kujikuta anatumia muda na nguvu nyingi kwenye kutangaza na kusambaza kazi zake kuliko kwenye kuzalisha. Hili linaathiri ubora wa kazi hizo na kujikuta inabidi atumie nguvu zaidi na zaidi kila wakati.
Njia bora ya kuepuka hili ni kuhakikisha unakazana kufanya kazi iliyo bora sana, kazi ambayo inajitangaza yenyewe, kazi ambayo mtu akikutana nayo anatamani kila anayemjua akutane nayo pia.
Ili kufikia hali hiyo, lazima muda mwingi utumike kwenye kuzalisha kuliko kwenye kutangaza na kusambaza. Lazima uwekeze sana kwenye kile unachozalisha, lazima kila wakati ukazane kuzalisha kwa ubora wa hali ya juu sana.
Unapokuja na kitu bora, hutumii nguvu kubwa kukiuza. Ndiyo, lazima utatangaza na lazima utasambaza, lakini hutahitaji kutumia nguvu sana na kuwalazimisha watu wachague kazi yako, maana kazi nzuri inajiuza kwa urahisi zaidi.
Wewe fanya kazi yako, na ifanye kwa ubora wa hali ya juu sana, halafu waache watu wachague. Kadiri kazi yako inavyokuwa bora, ndivyo wengi watakavyoichagua.
Na hii siyo kwa wasanii na waandishi pekee, ni kwa kila anayefanya kazi au biashara inayohusisha watu wengine. Uwe ni fundi mwashi, fundi seremala, kinyozi, daktari, mwalimu na kila aina ya kazi na taaluma, kazana kuboresha kile unachofanya na watu wataambiana wenyewe na kuja kwako.
Weka muda na nguvu za kutosha katika kuboresha kile unachofanya, kwa sababu hilo ndilo eneo kubwa unaloweza kuliathiri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,