Rafiki yangu mpendwa,

Karibu kwenye TANO ZA JUMA la tatu la mwaka huu 2019. Hapa nimekukusanyia yale matano muhimu sana ya kukupa maarifa na hamasa ya kuchukua hatua ili kuweze kufikia malengo yako makubwa.

Kwenye tano za juma hili la tatu nimekuandalia neno muhimu sana kwa mafanikio ambalo unapaswa kuliishi kila siku, nimekushirikisha uchambuzi wa kitabu kizuri sana kinachokuwezesha kuimiliki siku yako na kuitumia kwa makubwa, nimekushirikisha pia nguvu kubwa ya Uungu iliyopo ndani yako. Pia nimekufafanulia uhusiano wa mafanikio ya kifedha na mawazo yetu tuliyonayo kifedha, na mwisho kabisa nimekushirikisha umuhimu wa kuwa na ndoto kubwa, ndoto ambazo wewe mwenyewe unakuwa na wasiwasi nazo, lakini unaendelea kuziamini na unazifikia.

Karibu kwenye makala hii ya TANO ZA JUMA, tujifunze hayo matano kwa kina na uondoke na mambo unayokwenda kuyafanyia kazi kwenye maisha yako kwa kuanza na juma lamba 4 la mwaka huu 2019.

#1 NENO LA JUMA; UNG’ANG’ANIZI.

Kuna mtu anasoma hapa, tarehe 31 mwezi wa 12 alikesha akiusubiri mwaka mpya, akajiambia hatalala mpaka auone mwaka mpya. Akauona mwaka kweli, akajiwekea ahadi nyingi na kubwa kwa mwaka huu mpya.

Akajiambia atapunguza kupoteza muda, ataweka juhudi kwenye kazi zake, ataanza kufanya mazoezi na kula vizuri, ataweka akiba, ataanza biashara, ataanza ujenzi na mengine mengi mzuri.

Leo juma la tatu baada ya mipango ile mikubwa, amesharudi kwenye maisha ya kawaida. Alifanya mazoezi siku mbili tatu sasa ameshaacha, alikazana kula kwa afya juma la kwanza na leo hakumbuki tena kama alijiambia atakula vizuri. Na yale malengo ya akiba, biashara na ujenzi anajiambia muda bado upo, mwaka bao mchanga.

Sasa mtu huyu atakuja kustuka mwaka unaisha na hakuna hatua kubwa alizopiga zaidi ya kuishi kwa mazoea kama alivyoishi miaka iliyopita.

Rafiki yangu, kama wewe ni huyu mtu, nina neno moja kwako, unahitaji UNG’ANG’ANIZI ili kupata chochote unachotaka kwenye maisha. Mambo hayatakuwa rahisi, njia haitakuwa nyepesi na kukuachia nafasi ufanye kila unachotaka.

Kwenye kila kubwa unalopanga kufanya, utakutana na magumu na vikwazo vingi, lakini hilo halipaswi kukukatisha tamaa, badala yake linapaswa kukusukuma zaidi ili uendelee kuweka juhudi.

Rafiki, kama chochote ulichojiambia unataka kufanya au kufikia mwaka huu unataka ukifikie kweli, basi unahitaji UNG’ANG’ANIZI.

Unahitaji kujipa kauli hii; NITAPATA NINACHOTAKA AU NITAKUFA NIKIKITAFUTA. Unapojitoa kwa kiasi hiki kufanikiwa, hata dunia yenyewe itakupisha upate unachotaka. Watakapokuja wale wakatishaji tamaa ambao wamewarudisha wengi nyuma, ukiwaambia kauli hiyo watakukimbia kabisa, watajua wewe siyo wa ngazi zao.

Rafiki, bila ya UNG’ANG’ANIZI naweza kukuambia hata usijaribu kujiwekea malengo na mipango mikubwa, maana utakuwa umeshindwa kabla hata hujaanza.

Nenda KANG’ANG’ANE ili mwaka huu uwe wa tofauti kabisa kwako, usikubali kurudi nyuma au kuacha kama bado upo hai.

MASAA MAWILI YA ZIADA

#2 KITABU CHA JUMA; KLABU YA SAA KUMI NA MOJA ALFAJIRI.

Kitabu chetu cha juma la nne kinatoka kwa mwandishi na mhamasishaji mashuhuri, Robin Sharma.

Robin Sharma amekuwa kwenye tasnia ya uandishi, hasa kwa upande wa maendeleo binafsi kwa zaidi ya miaka 20 sasa. Amekuwa mwalimu, mshauri na kocha wa watu mashuhuri na wenye mafanikio makubwa sana duniani, akiwafundisha misingi muhimu ya mafanikio.

Robin alikuwa mwanasheria ambaye kazi yake ilimpa msongo sana kiasi cha kushindwa kufurahia maisha yake. Na hapo ndipo aliporudi kwenye nafsi yake na kuamua kufanya kile anachopenda kufanya, ambacho ni uandishi na kufundisha. Kitabu chake kilichosomwa sana na kujulikana na wengi ni kitabu kinachoitwa The Monk Who Sold His Ferrari, ambacho kilielezea maisha ya mwanasheria ambaye alikuwa na mafanikio makubwa sana kifedha, lakini hakuna na furaha ya maisha. Hapo aliamua kuachana na mali zake zote na kujifunza utawa, kitu ambacho kilimwezesha kujua maana ya maisha, kujijua mwenyewe na kuwa na furaha.

Kitabu cha juma hili ninachokwenda kukuchambulia ni kitabu chake kipya kinachokwenda kwa jina la THE 5 AM CLUB; Own Your Morning, Elevate Your Life.

Kwenye kitabu hiki, Robin Sharma anatushirikisha umuhimu wa kuianza siku yako asubuhi na mapema, wakati watu wengine bado wamelala. Anasema kwa kuimiliki asubuhi yako, utaweza kuyainua zaidi maisha yako.

Robin anatuambia ya kwamba, wale wote wenye mafanikio makubwa, tangu enzi na enzi, ni wale ambao walikuwa wanaamka mapema kabla wengine hawajaamka na kutumia muda huo kujiimarisha kimwili, kiakili, kiroho na kiafya.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa mfumo wa hadithi ya watu wawili, mwanamke mjasiriamali na mwanaume msanii ambao walikutana kwenye semina ya maendeleo binafsi, na hapo wakapata nafasi ya kukutana na bilionea ambaye aliwafundisha msingi muhimu wa mafanikio ambao ni kuamka mapema, saa kumi na moja asubuhi.

Hapa nakwenda kukushirikisha yale muhimu sana yatakayokuwezesha kuianza siku yako mapema na kuweza kuitawala siku yako na uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.

  1. TUNAISHI ZAMA ZENYE CHANGAMOTO KUBWA.

Hakuna kipindi kizuri kuwa hai kama sasa, kwa sababu teknolojia zimerahisisha sana maisha. Lakini pia hakuna kipindi kigumu kuwa hai kama sasa, kwa sababu teknolojia hizi hizi zinazorahisisha maisha yetu, zinayavuruga pia.

Ukiangalia maendeleo ya teknolojia ambayo yametuletea mtandao wa intaneti na simu janja, yamerahisisha sana mawasiliano na hata kujifunza. Lakini pia yameleta usumbufu mkubwa kiasi kwamba watu hawana tena muda wa kufanya yale mambo muhimu. Simu na mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya wengi kupoteza muda ambao wangeweza kuutumia kufanya makubwa.

Watu wengi wanaenda kwenye kazi zao, lakini badala ya kuweka muda wao kwenye kufanya kazi zao kwa ustadi na utofauti wa hali ya juu, wanatumia muda huo kuzurura kwenye mitandao ya kijamii kwa mambo ambayo hata hayana uhusiano na kazi zao.

Robin kwenye kitabu hiki anasema kwamba watu sasa wamekuwa misukule wa kiteknolojia (cyber zombies) watu ambao wanapelekeshwa tu na teknolojia na wasiweze kujizuia. Na ukiangalia hili ni kweli kabisa, watu wengi wanajikuta wanatumia mitandao ya kijamii, wanajua kabisa kwamba inawapotezea muda, lakini hawawezi kuacha kuitumia.

Unahitaji kuamka kutoka kwenye usukule ulioingia, kwa namna yoyote ambayo umeruhusu teknolojia iingie na kutawala maisha yako ifute kabisa. Kama unajua kuna kitu kinakupotezea muda lakini huwezi kukiacha kwa sababu unaogopa utapitwa, ni wakati wa kukiacha sasa.

Robin kwenye kitabu hiki anatufundisha kuwa na muda wetu binafsi kwenye siku, muda ambao hakuna teknolojia yoyote ile, ni sisi na mawazo yetu. Na muda huu ni asubuhi na mapema unapoamka na jioni unapoimaliza siku yako. Pia anatuambia siku moja au mbili kwenye wiki, tunapaswa kufanya kuwa siku ambayo hatutumii teknolojia kabisa. Yaani kwa siku nzima unaendesha maisha yako bila ya teknolojia hizi ambazo zinakupotezea muda sana.

Jaribu hili kwenye maisha yako, anza kuweka mipaka kati yako na teknolojia ambazo umeshazizoea sana na unajiambia huwezi kuishi bila teknolojia hizo. Anza kutenga masaa ambayo hutatumia kabia simu yako wala teknolojia nyingine yoyote. Pia tenga siku moja kwa wiki ambayo utakuwa mbali kabisa na teknolojia.

Kwa kufanya zoezi hili, utaona jinsi ambavyo una muda mwingi na pia utapata utulivu mkubwa wa akili yako.

  1. HUWEZI KUPATA BILA YA KUPOTEZA.

Robin ametufundisha na kutukumbusha kitu kingine muhimu sana kuhusu mabadiliko na kupata tunachotaka. Watu wengi tunapenda kupata vitu vipya, lakini hatutaki kupoteza vya zamani ambavyo tayari tunavyo. Hii ni sawa na mtu mwenye kikombe kimoja, ambacho kimejaa chai, halafu anataka maziwa, lakini pia anataka kubaki na chai yake.

Robin anatuambia chochote tunachotaka kwenye maisha, lazima tuwe tayari kupoteza kitu. Na hili ni muhimu sana kwenye kujijengea tabia za mafanikio, wengi wanapenda kuwa na tabia nzuri za mafanikio, lakini hawataki kuacha tabia za zamani.

Wengi wanapenda kuwa watu wapya, lakini hawataki kuachana na marafiki wao wa zamani. Halafu wanashangaa pale ambapo hawapigi hatua, wanabaki pale pale.

Mabadiliko ya tabia yanakutaka upoteze vitu vingi ambavyo ulishavizoea na huenda unavipenda sana.

Robin anasema, mabadiliko yoyote ni magumu sana mwanzoni, mabaya katikati na mazuri sana mwishoni. Ili kufika kwenye uzuri, lazima upite kwenye ugumu na ubaya.

  1. HATUA TATU ZA KUELEKEA KWENYE MAFANIKIO.

Zipo hatua tatu muhimu ambazo mtu unapaswa kuzipitia ili kuweza kufika kwenye mafanikio makubwa.

Hatua ya kwanza ni utambuzi, hapa lazima upate utambuzi wa unachotaka na mafanikio yenyewe. Hii ni hatua ya kujua unachotaka na kujifunza zaidi kuhusiana na kitu hicho.

Hatua ya pili ni kuchagua, baada ya kujifunza, unapaswa kuchukua hatua, na hapa ndipo unapochagua kipi cha kufanya kwenye yale uliyojifunza.

Hatua ya tatu ni matokeo, hapa sasa ndipo unapovuna matokeo ya hatua ulizochukua.

Wengi wamekuwa wanakosea sehemu mbili, kujua halafu wasichukue hatua, au kuchukua hatua bila ya kujua. Fuata hatua hizi na hutashindwa kwenye lolote.

  1. MAENEO MANNE YA KUWEKA MKAZO ILI KUFANIKIWA.

Robin anatuambia watu wote waliofanikiwa sana na kuacha historia kubwa hapa duniani, waliweka mkazo kwenye maeneo manne muhimu ya maisha yao;

Eneo la kwanza ni kutumia uwezo ulio ndani yako. Watu wengi wamekuwa wanafikiri wale wanaofanikiwa wana uwezo mkubwa kuliko wasiofanikiwa. Ukweli ni kwamba, watu hawatofautiani sana kwenye uwezo, ila wanatofautiana kwa jinsi wanavyotumia uwezo uliopo ndani yako. Ili kufanikiwa, jua uwezo uliopo ndani yako na utumie kwa kuendeleza zaidi.

Eneo la pili ni uhuru kutoka kwenye usumbufu. Tunaishi kwenye zama za kelele, zama ambazo kila mtu anaweza kukufikia na kelele yoyote ile kwa masaa 24 kwa siku. Ili ufanikiwe lazima ujitoe kwenye kelele hizi, lazima utenge muda ambao hutasumbuliwa kabisa. Lazima uwe na muda wa utulivu kwenye siku yako, ni katika utulivu ndiyo unaweza kufikiri sawasawa na kuja na hatua bora kabisa za kuchukua.

Eneo la tatu ni kujitawala wewe mwenyewe. Safari ya mafanikio haina tofauti na vita, kwenye vita wanasema jinsi unavyotokwa jasho jingi kwenye mazoezi, ndivyo itakavyotokwa damu kidogo kwenye mapambano. Ili kufanikiwa unahitaji kuwa na maandalizi binafsi na kuweza kujitawala wewe mwenyewe. Hapa Robin anatushirikisha maeneo manne yanayohitaji maandalizi mazuri ambayo ni mwili, fikra, roho na hisia. Anasema mafunzo mengi yamekuwa yanawakazania watu kubadili fikra, lakini wanasahau maeneo hayo mengine matatu na ndiyo maana hawafanikiwi.

Eneo la nne ni kuimiliki siku yako. Kitu pekee unachohitaji ili uwe na uhakika wa kuwa na maisha ya mafanikio ni kuweza kumiliki siku yako, kuweza kupangilia na kuyatawala masaa yako 24 na kupanga jinsi ya kuyatumia vizuri kwa mafanikio yako. Wengi hufikiri wanamiliki siku zao, lakini wanapozianza kwa habari na mitandao ya kijamii, wanagundua siku imeisha, wamechoka na hakuna kikubwa walichofanya.

  1. HATUA NNE ZA KUTENGENEZA TABIA MPYA.

Watu wengi ambao wamekuwa wanajaribu kutengeneza tabia mpya kwenye maisha yao wamekuwa wanashindwa kwa sababu huwa hawazijui hatua nne za kutengeneza tabia mpya na kuzifuata. Robin ametushirikisha hatua hizi na jinsi ya kuzitumia.

Hatua ya kwanza ni kichocheo cha tabia, lazima kuwe na kitu kinachokukumbusha kuhusu tabia mpya unayotaka kujenga. Kama ni kuamka basi alamu itakuwa kichocheo cha tabia.

Hatua ya pili ni kile unachofanya baada ya kichocheo kukumbusha kuhusu tabia. Lazima uwe na utaratibu ambao unaufuata mara zote, ili mwili uweze kuzoea na pale kichocheo kinapokuja, basi mwili unafuata utaratibu wenyewe. Kwenye mfano wa kuamka mapema, alamu inapoita, unatoka kitandani na kwenda kwenye jukumu la kwanza ulilojipangia. Baada ya muda mwili wako unazoea na kuwa unafanya bila hata ya kujiuliza.

Hatua ya tatu ni zawadi, ukitaka tabia mpya ijijenge, unapaswa kujipa zawadi pale unapokamilisha tabia hiyo. Mfano kila siku unayoamia mapema unajipa zawadi ya kitu fulani unachopenda sana. Siku unayochelewa kuamka unajinyima kitu hicho, na hapo mwili wako utakusukuma kuamka mapema kesho ili upate zawadi hiyo.

Hatua ya nne ni marudio, tabia mpya huwa inanasa kwa marudio, lazima urudie rudie sana mpaka iwe sehemu ya maisha yako. Na Robin anatuambia kwa mujibu wa tafiti, unahitaji angalau siku 66 za kufanya kitu kila siku mpaka kiwe tabia kwako. Kwenye kuamka asubuhi, unapaswa kuamka asubuhi kila siku kwa siku 66 bila ya kuacha na baada ya hapo itakuwa kitu cha kawaida kwenye maisha yako, hutasumbuka tena kuamka.

Wengi wamekuwa wanashindwa kwenye kujenga tabia mpya, hasa hatua ya nne ya kurudia, wanafanya kwa muda mfupi na kuacha. Sasa umeshajua urefu wa muda, ni angalau siku 66, hakikisha unaweka siku hizo kabla hujakata tamaa na kuona tabia haijengeki.

  1. KANUNI YA 20/20/20.

Kama jina la kitabu lilivyo, Robin anatufundisha kuamka mapema asubuhi, tuamke kabla ya jua kuchomoza, na muda anaoshauri ni saa kumi na moja asubuhi.

Baada ya kuamka, ile saa ya kwanza kabisa inakuwa saa takatifu kwako, saa ambayo huipotezi kwa namna yoyote ile.

Na ili kuhakikisha saa hii inakuwa takatifu kweli, Robin anatushirikisha kanuni kuu ya kuitumia kwenye saa hiyo. kanuni hiyo ni 20/20/20.

Kanuni hii unagawa saa yako takatifu kwenye dakika 20 ambazo utazitumia kama ifuatavyo;

DAKIKA 20 ZA KWANZA kwenye saa yako takatifu ni muda wa KUFANYA MAZOEZI, hapa unajihusisha na mazoezi ambayo yatakutoa jasho. Mazoezi yanaufanya mwili kuwa bora na yanaongeza miaka ya kuishi. Pia huu ni wakati wa kuupa mwili wako maji ya kutosha ili kuweza kukabili siku iliyopo mbele yako.

DAKIKA 20 ZA PILI ni muda wa kutafakari, hapa unakaa kwenye utulivu na kusali, kutahajudi, kutafakari, kupitia malengo yako na mipango ya siku iliyopo mbele yako.  Huu pia ni muda mzuri kwako kuandika mawazo yote uliyonayo kwenye akili yako kwenye kijitabu chako. Zoezi hili la kuandika mawazo yako linakuwezesha kufikiri kwa kina na kutumia mawazo yako mazuri baadaye.

DAKIKA 20 ZA TATU ni muda wa UKUAJI, huu ni muda wako wa kujifunza ili kukua zaidi. Hapa unasoma vitabu, unasikiliza vitabu na hata kuangalia mafunzo mbalimbali ambayo yanakuwezesha kukua binafsi na hata kukua kwenye kazi au biashara unayofanya.

Ukiweza kuamka kila siku asubuhi n mapema na kulitumia saa lako la kwanza kwa kanuni hiyo kila siku, utaweza kupiga hatua kubwa sana. kidogo kidogo utaanza kujiona wa tofauti, utaanza kufikiria kwa utofauti na kujaribu vitu tofauti.

MUHIMU; Robin anasema kanuni hii unaweza kuiboresha zaidi lakini muhimu ni kutawala asubuhi yako. unaweza kutenga muda zaidi kwenye mambo hayo matatu kadiri uwezavyo, muhimu ni ufanye kila siku.

  1. MAANDALIZI MUHIMU YA KUWEZA KUAMKA MAPEMA.

Watu wengi huwa wanapenda kuamka mapema, na wanaweka kabisa alamu ya kuwaamsha, ila pale alamu inapolia, wanakuwa wamechoka kiasi kwamba labda hawaisikii, au wakiisikia basi wanaizima haraka sana na kuendelea kulala.

Ili kuondokana na hali hii, Robin anatushirikisha mambo muhimu ya kuzingatia ili tuweze kuamka mapema. Na maandalizi haya yanaanza siku moja kabla.

Yafuatayo ni mambo ambayo unapawa kuzingatia ili uweze kuamka mapema.

Moja; pata mlo wako wa mwisho wa siku masaa mawili kabla ya muda wako wa kulala. Kama unalala saa nne basi mlo wako wa mwisho uwe kabla ya saa mbili.

Mbili; achana na teknolojia saa moja kabla ya muda wa kulala. Kama unalala saa nne, basi inapofika saa tatu, uwe umeshaachana na teknolojia zote. Hasa simu kwa sababu mwanga wa simu huwa unazuia akili isizalishe homoni inayoleta usingizi. Ukiwa unatumia simu mpaka muda unaoingia kulala, utachelewa kupata usingizi.

Tatu; usiingie na teknolojia kitandani. Hasa simu, usilale na simu.

Nne; alamu yako weka mbali na unapolala, kiasi kwamba utahitajika kuamka ili kwenda kuizima.

Tano; lala sehemu tulivu na yenye giza.

Sita; tenga angalau masaa saba ya kulala. Kama unataka kuamka saa kumi na moja asubuhi, lala saa nne.

Fanyia kazi hayo muhimu kama umekuwa unajaribu kuamka asubuhi lakini unashindwa.

  1. MBINU KUMI ZA KUWA NA AKILI NA MAFANIKIO MAKUBWA.

Robin anatushirikisha mbinu kumi za kutuwezesha kutumia akili zetu vizuri na kufanikiwa sana. Na hapa nakushirikisha mbinu hizi na hatua za kuchukua;

Moja; tenga muda ambao hutaruhusu usumbufu wa aina yoyote ile, muda huo unaweka mkazo wako kwenye kazi yako pekee, hakuna kingine kinachoruhusiwa hapo. Akili yako inafanya kazi kwa uwezo mkubwa sana unapokuwa na utulivu.

Mbili; dakika 90 za kwanza kwenye kazi yako zitumie kufanya kitu kimoja ambacho ndiyo muhimu kuliko vingine vyote, kitu kimoja ambacho ukikikamilisha basi utafanikiwa sana. Fanya hivi kwa siku 90 na utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

Tatu; baada ya dakika 90 za kwanza, muda unaobakia fanya kazi kwa dakika 60 na pumzika kwa dakika 10. Dakika 60 unazofanya kazi unafanya kazi kweli, hakuna usumbufu wala kupeleka mawazo yako pengine. Zikiisha unajipa dakika kumi za mapumziko, ambapo hapo unaweza kufanya chochote unachotaka. Ila dakika kumi za mapumziko zikiisha, rudi tena kwenye dakika 60 za kazi.

Nne; kuwa na vitu vitano vidogo vidogo ambavyo unapanga kukamilisha kila siku. Orodhesha vitu hivyo unapoianza siku yako na hakikisha unavifanyia kazi kwenye siku yako. Kukamilisha vitu vitano kila siku ni ushindi mkubwa sana kwako, kwa mwezi utakamilisha vitu 150, kwa mwaka zaidi ya vitu 1800, utapiga hatua sana.

Tano; tenga nafasi ya pili ya kufanya mazoezi kwenye siku yako. Kwa kuwa mazoezi yana faida sana kwenye mwili wako, tenga nafasi ya pili ya kufanya mazoezi kwenye jioni yako. Na siyo lazima yawe mazoezi magumu, yanaweza kuwa matembezi tu lakini yakakunufaisha sana, na pia yakakupa utulivu na muda wa kuwa mbali na teknolojia.

Sita; tenga muda wa kuchua mwili wako, zipo faida nyingi za kuuchua mwili wako, kunaondoa uchovu na kuimarisha afya. Angalau mara mbili kwa wiki tenga muda wa kuchua mwili wako.

Saba; chuo kikuu cha barabarani. Kama unatumia zaidi ya nusu saa kwenda na kurudi kwenye kazi zako kila siku, basi unapaswa kutumia muda huo kujifunza. Na jifunze kwa kusikiliza vitabu vilivyosomwa, iwe unatumia usafiri wako binafsi au usafiri wa uma.

Nane; tengeneza timu bora, usikazane kufanya kila kitu mwenyewe, tengeneza timu bora ya kukusaidia na yale majukumu ambayo wengine wanaweza kufanya wape wayafanye, wewe baki na yale muhimu pekee, ambayo wewe tu ndiye unayeweza kuayafanya.

Tisa; ipangilie wiki yako kabla hujaianza, na kila unapomaliza wiki yako ipitie na kutafakari. Kila siku ya jumapili, tenga muda usiopungua nusu saa, pitia juma linaloisha na ona hatua zipi ulichukua, kisha pangilia juma unalokwenda kuanza na panga yale unayokwenda kufanya. Zoezi hili fupi litakuwezesha kufanya makubwa kwenye majuma yako.

Kumi; tenga dakika 60 za kujifunza kila siku. Achana na ule muda wa kujifunza asubuhi, achana na ule muda unaojifunza ukiwa njiani, kwenye siku yako tenga dakika 60 za kujifunza kitu kwa kina. Hapa unajifunza kitu ambacho kinakuwezesha kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, kazi zako na hata biashara zako. Huu ni muda muhimu sana kwa ukuaji wako.

Hizo ndiyo mbinu kumi za kuweza kutumia akili yako vizuri na kupiga hatua kwenye maisha yako. Zifanyie kazi kila siku na hutabaki hapo ulipo sasa.

Rafiki yangu mpendwa, haya ndiyo maarifa muhimu sana na yenye hatua za kuchukua ambayo nimekuandalia kutoka kwenye kitabu hiki kizuri sana cha Robin Sharma. Yasome na kutafakari, na panga kuanza kuyatumia kwenye juma linalokwenda kuanza. Na chagua kuamka mapema na kumiliki asubuhi yako kuwa zoezi la kila siku ya maisha yako, na maisha yako yatabadilika sana.

#3 MAKALA YA JUMA; NGUVU YA UUNGU ILIYOPO NDANI YAKO.

Dini na falsafa nyingi zinatufundisha kwamba sisi binadamu tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Na hii ina maana kwamba, zile sifa ambazo Mungu anazo, zipo ndani yetu pia.

Na wanasayansi pamoja na wanafalsafa kwa pamoja wanaendelea kudhibitisha hilo, na kuonesha dhahiri kwamba ndani ya kila mmoja wetu kuna nguvu kubwa ya uungu, unayomwezesha mtu kufanya makubwa kwa namna atakavyo.

Makala ya juma hili ilielezea kwa kina kuhusu nguvu hii kubwa iliyopo ndani yako na jinsi unavyoweza kuitumia kufanya makubwa sana kwenye maisha yako.

Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, isome sasa hapa. Ni makala unayopaswa kuisoma taratibu, kuielewa na kuifanyia kazi, hakikisha hukosi kuisoma kwa kufungua hapa sasa; Hii Ndiyo Nguvu Kubwa Iliyopo Ndani Yako, Unayoweza Kuitumia Kupata Chochote Unachotaka. (https://amkamtanzania.com/2019/01/16/hii-ndiyo-nguvu-kubwa-iliyopo-ndani-yako-unayoweza-kuitumia-kupata-chochote-unachotaka/)

#4 TUONGEE PESA; FEDHA KAMA WAZO.

Watu wawili, wanaweza kuwa wanafanya kazi sehemu moja, wana elimu sawa, wana kipato sawa, lakini mmoja akapiga hatua sana kifedha huku mwingine akibaki kwenye umasikini. Na hapo wote wanategemea kipato kimoja tu, hakuna anayeanza na cha ziada.

Watu wawili, wanaweza kuwa wanafanya biashara ya aina moja, eneo moja wakiuza vitu sawa na kwa mtaji sawa, mmoja akapiga hatua sana kifedha huku mwingine akibaki kwenye umasikini.

Hii ndiyo hali ambayo ukienda popote utaikuta, na hii inatuonesha kwamba kinachowatofautisha watu kwenye fedha siyo kiasi cha fedha wanachoanza nacho au walichonacho, bali jinsi wanavyofikiri inapokuja kwenye swala la fedha.

Mtu mmoja atapata fedha kidogo na kuitumia kama mbegu ambayo inamwezesha kufanikiwa zaidi kifedha. Mwingine atapata fedha kidogo na kusema haitoshi chochote na hivyo kuitumia yote, akisubiri mpaka apate nyingi kitu ambacho kimekuwa hakitokei.

Hivyo rafiki, kila kitu unachopanga kuhusu fedha, lazima kwanza urudi kwenye msingi mkuu ambao ni fikra ulizonazo kuhusu fedha.

Kama unafikiri unahitaji fedha nyingi ndiyo uweze kuanza chochote, kama unafikiri kiasi ulichonacho sasa hakitoshi, na kama unajiambia kwa pale ulipo sasa huwezi kuanza mpaka upate fedha nyingi unazotaka, unahitaji kubadili fikra zako kifedha, kwa sababu zitakuwa kikwazo cha mafanikio makubwa kwako.

Mafanikio kifedha yanaanzia kwenye fikra za kifedha ambazo mtu unakuwa nazo. Ukiwa na fikra bora, fikra za uwezekano na fikra za kuanza na ulichonacho, popote ulipo lazima utapiga hatua zaidi.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; UMUHIMU WA NDOTO KUBWA.

“Dream lofty dreams, and as you dream, so you shall become. Your vision is the promise of what you shall one day be; your ideal is the prophecy of what you shall at last unveil.” – James Allen

Ota ndoto kubwa, ndoto ambazo hujawahi kuwa nazo, maana unavyoota ndivyo unavyokuwa. Maono yako ni ahadi ya jinsi utakavyokuja kuwa. Nadharia yako ni utabiri wa jinsi utakavyokuja kuwa.

James Allen, mtu aliyeandika sana kuhusu nguvu ya fikra zetu anatukumbusha umuhimu wa kuwa na ndoto kubwa. Kwa sababu akili yako ina nguvu kubwa, ndoto yoyote utakayokuwa nayo kwa muda mrefu basi itakuwa uhalisia.

Hivyo kuwa na ndoto kubwa, tengeneza maono makubwa sana na usijiwekee ukomo wa aina yoyote ile. Kuwa na picha kubwa ya maisha yako ya mafanikio na ishi picha hiyo kila siku, na kwa hakika utafikia maono uliyonayo.

Rafiki, ule tuliokuwa tunasema ni mwaka mpya, unachanganya sasa, hivyo unapaswa kuwa tayari kwenye mwendo kasi wa yale uliyopanga kufanya kwenye mwaka huu.

Nakutakia kila la kheri kwenye juma la 4 tunakwenda kuanza, lipangilie juma hilo kabla ya kulianza na nenda kalitendee haki kwa kuishi misingi yote ya mafanikio ambayo tumekuwa tunajifunza.

Kila la kheri.

Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.

Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.

Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)

Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu