“Ask yourself the following first thing in the morning:
What am I lacking in attaining freedom from passion?
What for tranquility?
What am I? A mere body, estate-holder, or reputation? None of these things.
What, then? A rational being.
What then is demanded of me? Meditate on your actions.
How did I steer away from serenity?
What did I do that was unfriendly, unsocial, or uncaring?
What did I fail to do in all these things?”
—EPICTETUS, DISCOURSES, 4.6.34–35
Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nzuri ya leo.
Tumepata nafasi mpya na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari; UTARATIBU WA KUTAFAKARI KILA ASUBUHI….
Kila siku asubuhi, tenga muda wa wewe kujitafakari na kuyatafakari maisha yako.
Jiulize maswali yafuatayo katika kila tafakari;
Je nakosa nini ili ili niweze kuwa huru kutoka kwenye tamaa?
Na nahitaji nini ili kupata utulivu?
Je mimi ni nini? Mwili tu, mmiliki wa mali au sifa yangu kwa wengine? Yote haya siyo sahihi.
Mimi ni nini basi? Kiumbe mwenye uwezo wa kufikiri.
Je nini kinahitajika kutoka kwangu? Kutafakari kila hatua unayochukua.
Je ni nini kinaniondoa kwenye utulivu?
Je ni vitu gani nimefanya ambavyo siyo vya kirafiki, siyo vya kijamii na siyo vya kujali?
Na je nimeshindwa kufanya nini kwenye yote hayo?
Wastoa wamekuwa na utaratibu wa kuyatafakari maisha yao na kila hatua wanayochukua kwenye maisha.
Kwa njia hii wanajijua vizuri wao wenyewe na wanajirekebisha wenyewe kwa makosa mbalimbali wanayokuwa wamefanya.
Tenga muda kwenye kila siku yako, hasa asubuhi na fanya tafakari hii ya kina kuhusu maisha yako na kila hatua unayochukua.
Unaweza kufikiri unajijua, lakini utakapoanza kufanya tafakari hizi za kina ndiyo utajua kweli kwamba hujijui kama unavyofikiri unajijua.
Kila mmoja wetu ana eneo analoweza kujiboresha zaidi,
Kila mmoja wetu ana maeneo ambayo ana udhaifu, na mengine ana uimara.
Na kama wanavyosema wanafalsafa wengi, kama unataka kuijua dunia, jijue vizuri wewe mwenyewe.
Na kama unataka kuitawala dunia, jitawale wewe mwenyewe kwanza.
Anza kujipa muda wa kutafakari na utajijua na kujitawala wewe mwenyewe, halafu dunia haitakuwa shida yoyote kwako.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujitafakari na kutafakari kila unachofanya na kujiboresha zaidi.
#JitafakariMwenyewe, #FikiriUnachofanya, #KuwaBoraKilaMara
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha.