Unahitaji nguvu ile ile kufanya kazi kama unayotumia kutoroka kufanya kazi.

Watu wengi wamekuwa wanatumia nguvu zao siyo kwenye kufanya kazi, bali kutoroka kufanya kazi.

Wanapanga vizuri ni hatua zipi watakazochukua, lakini inapofika wakati wa kuchukua hatua, hawakosi kuwa na dharura. Na hata wanapoanza kufanya na wanakutana na ugumu, wanaacha kufanya wanachofanya na kwenda kwenye usumbufu.

Tunahitaji kuwa makini sana, kujua kazi yetu muhimu kabisa ni ipi, kipaumbele chetu cha kwanza ni kipi. Halafu kuweka nguvu zetu katika kutekeleza kipaumbele chetu.

Kufanya kipaumbele cha pili wakati cha kwanza bado hujakikamilisha siyo kufanya kazi, bali kutoroka kufanya kazi.

Kupangilia eneo lako vizuri wakati bado hujamaliza kazi uliyopanga kufanya siyo kufanya kazi bali kutoroka kufanya kazi.

Kuna njia nyingi tumekuwa tunazitumia kutoroka kufanya kazi, usipozijua unaweza kufikiri unafanya kazi, na siku inaisha ukiwa umechoka kweli, ila ukiangalia ulichokamilisha kwenye siku hiyo hukioni.

Kama unachofanyia kazi siyo kipaumbele cha kwanza kabisa kwenye maisha yako basi hapo hufanyi kazi, unatoroka kufanya kazi.

Unafanya kazi pale tu nguvu zako zinapokuwa kwenye kipaumbele cha kwanza kwenye maisha yako, ambacho ukikikamilisha unaleta matokeo ya tofauti kabisa kwenye maisha yako. Mengine yote, nje ya kipaumbele hicho kwa wakati huo ni upotevu wa muda na kutoroka kufanya kazi.

Fanya kazi na siyo kutoroka kufanya kazi, nguvu hizo hizo unazotoroka nazo, ndizo unazohitaji ili kusonga mbele zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha