Rafiki yangu mpendwa,

Pamoja na msisitizo mkubwa unaowekwa kwa watu kuingia kwenye biashara na ujasiriamali, njia hii siyo rahisi kama wengi wanavyofikiri wakati wanaingia. Ni njia nzuri inayoweza kukupa uhuru, lakini kabla hujapata uhuru huo utapitia mateso makali.

Watu wengi huwa wanafikiria kwamba ukishakuwa na wazo zuri la biashara, ukawa na mtaji wa kutosha na ukawa eneo zuri basi wateja watakuja wenyewe. Na palikuwa na usemi zamani kwamba jenga biashara na wateja watakuja wenyewe.

Hiyo ilikuwa enzi hizo, ambapo biashara zilikuwa chache na watu hawakuwa na uhuru wa kuchagua. Lakini enzi hizi ambazo kila mtu anafanya biashara, enzi ambazo mteja ana machaguo mengi kuliko anavyoweza kufikiri, mpango wa kujenga watakuja haifanyi kazi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakwama kwenye kutengeneza wateja wapya kwenye biashara zao. Biashara inaanza na wateja fulani na hao ndiyo wanaendelea kuwa nao kwa muda mrefu.

Sasa kwa kuwa maisha ya wateja yanabadilika, kuna ambao wanapungua kwa sababu mbalimbali. Wengine wanahama eneo, au uhitaji wao kwenye biashara yako unakuwa haupo tena. Hivyo kadiri muda unavyokwenda, wateja wa biashara wanakuwa wanapungua.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Na hili ndilo linaloleta matatizo yote kwenye biashara, kwa sababu ukiwa na wateja wachache, unakuwa na mauzo kidogo, faida inakuwa kidogo na biashara haiwezi kujiendesha.

Ili kuvuka mkwamo huu wa kibiashara, unapaswa kuwa unatengeneza wateja wapya kila mara kwenye biashara yako. Kila siku unahakikisha kuna watu wapya wanajua kuhusu biashara yako, na hao unawashawishi wanunue na wakinunua mara moja unahakikisha wanaendelea kununua zaidi na zaidi.

Hata kama biashara yako inajulikana kiasi gani, hata kama ina wateja wengi kiasi gani, usijidanganye kabisa na kuona kwamba huhitaji tena kutafuta wateja wapya. Kutafuta wateja wapya ni zoezi endelevu kwenye biashara yako, kitu ambacho unapaswa kukifanya kila siku.

Unafikiri kwa nini makampuni ya simu ambayo yana wateja wengi na yanajulikana kila siku yanaendelea kujitangaza kila siku? Je kuna siku inapita hujaona au kukutana na matangazo ya makampuni ya simu? Kampuni hizi zinaelewa kila wakati zinapaswa kuwa zinatengeneza wateja wapya.

Kila wakati tengeneza wateja wapya kwenye biashara yako, andaa matangazo ya vipeperushi, matangazo ya mitandao ya kijamii na hata matangazo ya vyombo vya habari kulingana na uwezo wako. Na washawishi wateja wapya kufika kwenye biashara yako na wanapofika wanapaswa kupata huduma bora sana, ambayo hawajawahi kuipata popote pale.

SOMA; Hii Ndiyo Njia Moja Ya Uhakika Ya Kuwashawishi Wateja Kununua Chochote Unachouza.

HATUA ZA KUCHUKUA KWENYE BIASHARA YAKO.

Fikiria kwa mwezi mmoja uliopita, ni wateja wangapi wapya ambao wamenunua kwenye biashara yako, kama hakuna kabisa upo pabaya.

Andaa mpango wa kufikia wateja wapya kila wiki na gawa kwa siku, kila siku chukua hatua za kuwafikia wateja hao wapya.

Unapowapa wateja wapya taarifa za biashara tako, chukua mawasiliano yao na tengeneza mfumo wa mawasiliano wa wateja wako. Hawa unapaswa kuendelea kuwasiliana nao mara kwa mara ili wakukumbuke na waje kununua kwako pale wanapokuwa na uhitaji.

Kila wakati biashara yako inapaswa kuwa inatengeneza wateja wapya, usiridhike kwa kuona tayari una wateja wa kutosha, kitu chochote ambacho hakikui kinakufa, hiyo ni sheria ya asili. Kuza zaidi biashara yako kwa kuongeza wateja wapya kwenye biashara hiyo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge