Rafiki yangu mpendwa,
Ipo wazi kwamba kipato cha ajira hakiwezi kutosheleza mahitaji ya maisha ya mtu. Hii ni kwa sababu kipato cha ajira yaani mshahara ni kidogo na huwa hakiongezeki haraka kama ambavyo mahitaji ya mtu yanaongezeka.
Hivyo njia pekee ya mtu kushika hatamu ya maisha yake na kuhakikisha anakuwa na kipato cha uhakika ni kujiajiri mwenyewe, kuwa na biashara ambayo inamwingizia kipato kisichokuwa na ukomo.
Katika hili la kuanzisha biashara ili kuboresha kipato, kuna habari nzuri na habari mbaya.
Habari nzuri ni kwamba zama zimebadilika sana, sasa hivi ni rahisi sana kwa mtu kuingia kwenye biashara tofauti na ilivyokuwa zamani. Kwa mtaji kidogo au bila ya mtaji kabisa mtu anaweza kuingia kwenye biashara yoyote anayotaka.
Habari mbaya ni kwamba licha ya kuwa rahisi kuingia kwenye biashara, lakini pia ni rahisi kwa biashara kushindwa. Zaidi ya asilimia 80 ya biashara zinazoanzishwa zinakuwa zimekufa ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa biashara hizo. Na hata zile ambazo hazifi, nyingi zinaendeshwa kwa mazingira magumu sana, hazitengenezi faida kubwa.
Swali kubwa sana ambalo watu wamekuwa wanajiuliza miaka na miaka ni nini kinasababisha watu wengi wanaoingia kwenye biashara kushindwa?
Na hili ndiyo swali ambalo mwandishi Michael Gerber amelipatia majibu kwenye kitabu chake kinachoitwa E-MYTH REVISITED. Michael anasema kuna imani potofu kwamba biashara ndogo zinaanzishwa na wajasiriamali ambao wanajitoa kujaribu mambo ambayo yanaweza kuwa hatari kwa mategemeo ya kupata faida.
Michael anasema hili siyo kweli, wengi wanaoanzisha biashara ndogo siyo wajasiriamali bali ni mafundi ambao wamepatwa na kifafa cha ujasiriamali, na hili ndiyo linasababisha biashara nyingi kushindwa.
Anachosema Michael ni kwamba biashara nyingi ndogo zinazoanzishwa zinakufa kwa sababu watu wanaozianzisha hawajijui vizuri wao wenyewe. Wengi wanafikiri kwamba ni wajasiriamali, lakini ukweli ni kwamba ni mafundi ambao wamepatwa na kifafa cha ujasiriamali. Kifafa hicho kinawapa msukumo wa kuingia kwenye biashara, lakini baada ya muda kifafa hicho cha ujasiriamali kinaisha na hapo ndipo mambo yanakuwa magumu kwao na biashara kushindwa.
Kwenye makala hii nitakwenda kukushirikisha maana ya kifafa cha ujasiriamali na haiba tatu muhimu zilizopo ndani ya mtu zinazopaswa kuendelezwa ili mtu uweze kufanikiwa kwenye biashara.
Kifafa cha ujasiriamali.
Hivi ndivyo watu wengi wanavyoingia kwenye biashara,
Kwanza mtu huyo anakuwa ameajiriwa, akifanya kazi kulingana na ujuzi alionao. Anakuwa yuko vizuri sana kwenye kazi hiyo, lakini kipato kinakuwa siyo kizuri. Hivyo anaona ajira hiyo haiwezi kumtosheleza. Lakini pia akiangalia anaona jinsi mwajiri wake anavyotengeneza faida kubwa kuliko kile anacholipwa yeye.
Mtu anaona jinsi ambavyo kazi yake ndiyo inaingiza faida kubwa kwa mwajiri wake, na kuona kwamba anamfaidisha sana mwajiri wake kuliko anavyonufaika yeye. Anaona njia pekee ya kuwa na kipato cha uhakika na kuwa huru na maisha yake ni kuachana na ajira na kwenda kujiajiri. Akijiangalia anaweza kufanya kazi vizuri na hivyo kuona anajiweka kwenye kifungo, ni bora akawe bosi wake mwenyewe.
Hiki ndiyo kinaitwa kifafa cha ujasiriamali, mtu anapatwa na mawazo ya kuweza kufanikiwa mwenyewe kupitia biashara kuliko kuajiriwa. Hapo mtu anatoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri, anakwenda kuanzisha biashara yake kwa sababu anajua vizuri kile anachofanya na anataka uhuru. Mwanzo anakuwa na msukumo mkubwa wa kuchukua hatua katika kuanzisha biashara yake, na kweli matokeo yanakuwa mazuri.
Kwa kuwa yuko vizuri kwenye kile anachofanya, basi anatoa huduma nzuri na wateja wake wanaridhika. Hili linafanya wateja kuendelea kuja na kuwaleta wengine pia. Biashara inaendelea kukua na majukumu yanazidi kuwa mengi. Na hapo ndipo mambo yanapobadilika, kadiri biashara inavyokua kubwa, ndivyo mtu huyo anavyokosa uhuru wake.
Aliondoka kwenye ajira ili kuwa na uhuru kwa kuingia kwenye biashara, lakini anakuja kugundua biashara inamtegemea yeye kwa kila kitu. Asipokuwepo kwenye biashara basi haiendi. Wateja wake hawataki kuhudumiwa na mtu mwingine bali yeye. Hapa ndipo anagundua kwamba siyo tu hajapata uhuru, lakini bosi aliyenaye sasa, yaani biashara yake hana huruma. Yeye ndiye anayekuwa biashara yake na hili linamchosha haraka sana.
Watu wengi wanaotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri wanajikuta kwenye shimo hilo la biashara kuwategemea wao kwa kila kitu. Na ukiacha biashara kuwategemea, lakini pia inakuwa inawahitaji kufanya vitu vingi kuliko walivyokuwa kwenye ajira.
Mtu anapokuwa ameajiriwa anatekeleza majukumu yake ya ajira pekee, yaani anafanya kile ambacho ndiyo taaluma au ujuzi wake. Lakini mtu anapoingia kwenye biashara, biashara inamtaka afanye vitu vingi ambavyo viko nje ya taaluma yake. Biashara inamtaka awe mzalishaji, awe mtu wa masoko, mtu wa mauzo, mtu wa huduma kwa wateja, mtu wa fedha na mipango ya ukuaji wa biashara hiyo. Majukumu yote haya kuwa chini ya mtu mmoja, ambaye hakuwa na maandalizi sahihi yanamchosha haraka na kupelekea biashara kushindwa.
Ni vigumu sana kufanikiwa kwenye biashara kama unasukumwa na kifafa cha ujasiriamali. Kwa sababu kifafa hicho hudumu kwa muda mfupi, na baada ya hapo uhalisia unajitokeza na zile fikra kwamba ukijiajiri utakuwa bosi wako mwenyewe na hakuna wa kukupangia cha kufanya yanapotea kabisa. Kwa sababu unakuja kugundua biashara yako inakutawala wewe na wateja wako wanaweza kuyafanya maisha yako kuwa magumu zaidi.
Swali ni je unawezaje kuondokana na kifafa hiki cha ujasiriamali ili uweze kuanzisha biashara sahihi na itakayokuweka huru? Jibu ni kujijua wewe mwenyewe vizuri kabla hujaingia kwenye biashara. Ukiingia kwenye biashara kabla hujajijua vizuri lazima utashindwa. Katika kujijua wewe mwenyewe vizuri, kuna haiba tatu unapaswa kuzijua na kuzifanyia kazi kwenye biashara.
SOMA; Hatua Nane Za Kujenga Biashara Yenye Maono Makubwa Na Itakayokufikisha Kwenye Mafanikio Makubwa.
Haiba tatu unazopaswa kuzijua na kuzifanyia kazi kwenye biashara.
Wanasaikolojia wanauambia kwamba wewe siyo mtu mmoja, bali ndani yako una haiba mbalimbali ambazo zinaweza kuwa zinakinzana au kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya maisha yako. Ndani ya kila mtu kuna haiba tofauti tofauti. Tunaweza kusema mtu mmoja anaweza kuwa na watu wengi ndani yake. Na unaweza kulidhibitisha hili pale unapokuwa na ubishi ndani ya nafsi yako mwenyewe. Unataka kufanya kitu fulani lakini pia hutaki kukifanya. Haiwezekani mtu mmoja ukawa unabishana na wewe mwenyewe, hivyo basi kinachobishana ni zile nafsi tofauti ambazo zipo ndani yako.
Kwa upande wa biashara, zipo haiba tatua ambazo zinakuwa ndani ya mtu, na kama mtu hatazielewa basi hawezi kufanikiwa kwenye biashara. Kuzijua haiba hizi tatu na kuzipa nafasi sawa ni hitaji la kwanza la kufanikiwa kwenye biashara.
MOJA; MJASIRIAMALI.
Hii ni haiba ambayo inabeba nafsi ya mjasiriamali. Mjasiriamali ni mtu wa kuja na mawazo mapya ya kuzitumia fursa mbalimbali ambazo zinapatikana. Mjasiriamali ni mtu wa ndoto na maono makubwa, mtu wa kutengeneza picha za mambo yasiyoonekana. Mjasiriamali anaangalia mambo yalivyo na kujiuliza vipi kama yangekuwa tofauti.
Bila ya mjasiriamali hakuna mawazo mapya, hakuna ugunduzi na wala hakuna maono makubwa ya kibiashara.
Nafsi ya ujasiriamali ndiyo inawasukuma wengi kuingia kwenye biashara, lakini nafsi hii imekuwa haidumu kwa muda mrefu, inazidiwa nguvu na nafsi nyingine na ndiyo maana tunasema mtu anakuwa amepatwa na kifafa cha ujasiriamali. Wazo la ujasiriamali linamjia kwa muda mfupi na nafsi hii kuondoka kabisa.
MBILI; MSIMAMIZI/MENEJA.
Hii ni haiba inayobeba nafsi ya usimamizi au umeneja kwenye biashara. Meneja ndiye mtu ambaye anaisimamia biashara kwa ukaribu, kuhakikisha kwamba kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa. Huyu ni mtu ambaye anahakikisha rasilimali za biashara zinatumika vizuri. Pia meneja anahakikisha kilichofanywa kwenye biashara jana ndiyo kinafanywa leo. Mameneja hawapendi kujaribu vitu vipya kwa sababu hawana uhakika navyo.
Tofauti kubwa ya mjasiriamali na meneja ni mabadiliko, mjasiriamali anatafuta mabadiliko na kuwa tayari kuyafanyia kazi. Lakini meneja hataki kabisa mabadiliko, anataka kuendelea kufanya mambo kama ambavyo amekuwa anafanya. Meneja anapenda zaidi uhakika wa kile ambacho ameshakizoea.
Meneja ndiyo nafsi inayoiwezesha biashara kufanya kazi. Mjasiriamali anakuwa na mawazo mapya na makubwa, lakini hawezi kuyafanyia kazi mawazo hayo kwa muda. Hivyo anahitaji kuwa na meneja ambaye anafanyia kazi mawazo hayo mapya.
TATU; FUNDI/MTAALAMU.
Hii haiba inayobeba nafsi ya ufundi au utaalamu unaohitajika kwenye biashara. Huu ni ule ujuzi au utaalamu ambao mtu anaingia nao kwenye biashara. Fundi kazi yake ni kutengeneza vitu na anapenda sana kutengeneza vitu. Haiba hii ya ufundi inapenda kufanya yale yanayopaswa kufanywa kwenye biashara.
Wakati mjasiriamali anakuja na mawazo mapya, meneja anaweka mfumo mzuri wa kufanyia kazi mawazo hayo, fundi ndiye anayefanya kazi kwenye biashara hiyo na kuzalisha matokeo yanayohitajika. Fundi ndiye anayezalisha matokeo kwenye biashara.
SOMA; Eneo Moja Ambapo Biashara Nyingi Zinakwama Na Jinsi Ya Kulivuka Ili Biashara Yako Ifanikiwe.
NAFSI TATU NDANI YA MTU MMOJA.
Kama ambavyo tumejifunza kuhusu nafasi hizo tatu zinazohusiana na biashara, zote zinakuwa ndani ya mtu mmoja. Na mtu ataweza kufanikiwa kwenye biashara kama nafsi zote tatu zitapewa nafasi sawa. Nafsi hizo tatu zimekuwa zinashindana, kila moja ikitaka kutawala nafsi nyingine. Na hili ndiyo limekuwa linasababisha biashara nyingi kufa.
Kama nafsi ya ujasiriamali itashinda na kutawala, basi mtu hataweza kufanya kitu kwa muda mrefu, kila wakati anakuja na wazo jipya la kuanza kitu kipya au kuboresha zaidi anachofanya. Kabla hajafanyia kazi wazo hilo anapata wazo jingine zuri zaidi. Nafikiri unawajua watu ambao kila wakati wanakuja na mawazi mapya ya biashara lakini hakuna linalotekelezwa, hawa ni watu ambao nafsi inayotawala ni ujasiriamali.
Kama nafsi ya umeneja itashinda na kutawala, mtu ataweza kuanzisha biashara, lakini hakuna mabadiliko yatakayofanyika. Biashara itaendeshwa kwa mazoea na hata kama mambo yamebadilika mtu anaendelea kufanya biashara yake kwa mazoea. Hizi ndiyo zile biashara ambazo huwa zinapitwa na wakati lakini wamiliki hawaelewi.
Kama nafsi ya ufundi itashinda na kutawala, mtu anaanzisha biashara ambayo yeye ndiye anayefanya kila kitu kwenye biashara. Anaamini hakuna anayeweza kufanya kama yeye. Kufanya kila kitu kunamchosha sana na kushindwa kuwa na maono makubwa ya biashara hiyo au kuisimamia vizuri. Kinachotokea ni biashara kushindwa kujiendesha vizuri.
Ili kufanikiwa kwenye biashara, lazima nafsi hizo tatu zifanye kazi kwa ushirikiano. Lazima uvae kofia hizo tatu kwa wakati mmoja.
Nafsi ya ujasiriamali ikupe mawazo mapya, nafsi ya umeneja itengeneze mfumo wa kufanyia kazi mawazo hayo mapya na nafsi ya ufundi ichukue hatua za kufanyia kazi. Nafsi hizi tatu zinapokuwa na nguvu sawa wakati wote, utaweza kuanzisha biashara ambayo itakua na kudumu kwa muda mrefu.
Kabla hujaingia kwenye biashara au hata kama umeshaingia, kaa chini na tambua nafsi hizi tatu ndani yako. Usijiambie kuna nafsi huna, kila mtu ana nafsi hizi tatu, ila wengi wamezika baadhi ya nafsi mpaka wanaona hawana kabisa. Ibua nafsi hizi tatu na zifanyie kazi kwa ushirikiano. Hilo litakuwezesha kuanzisha biashara yenye mlinganyo sahihi, inayozalisha bidhaa au huduma bora, inayosimamiwa vizuri na kuweza kukua pia.
Kwa kuamsha nafsi zote tatu utaweza kutengeneza mifumo bora kwenye biashara yako na hivyo biashara hiyo kukufanya kuwa huru, kuacha kukutegemea wewe kwa kila kitu na biashara kuweza kujiendesha yenyewe hata kama wewe haupo kwenye biashara hiyo moja kwa moja.
Je ungependa kujifunza jinsi ya kutengeneza mfumo wa kuendesha biashara yako ambao unakupa wewe uhuru, ambao unakuwezesha kuondoka kwenye biashara na biashara hiyo kuendelea kwenda vizuri bila ya uwepo wako? Kama jibu ni ndiyo basi usikose makala ya TANO ZA JUMA hili la 20 ambapo nitakuchambulia kwa kina kitabu E-MYTH REVISITED ambapo mwandishi Michael Gerber ametupa mbinu za kutengeneza biashara inayojiendesha yenyewe.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge