Watu wengi wanaotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri huwa wanashindwa mapema sana kuendelea na kile ambacho wamekianzisha. Zipo sababu nyingi zinazochangia hali hiyo, lakini kubwa kabisa ni falsafa ambayo mtu anakuwa anaiishi anapokuwa kwenye ajira na anapokwenda kujiajiri.
Wengi wanaenda kujiajiri wakitumia falsafa za kuajiriwa, kitu ambacho kinawapelekea kushindwa haraka.
Kwenye kitabu cha Rich Dad’s Before You Quit Your Job: 10 Real-Life Lessons Every Entrepreneur Should Know About Building a Multimillion-Dollar Business, Robert Kiyosaki ametushirikisha maandalizi muhimu sana mtu unapaswa kuwa umeyafanya kabla hujaacha kazi na kwenda kujiajiri. Moja ya vitu alivyoshirikisha ni falsafa ya kijasiriamali.
Katika falsafa hiyo, Robert ametushirikisha mambo haya kumi muhimu katika kujijengea mtazamo mpya wa mafanikio kupitia biashara na ujasiriamali.
- Penda uhuru na siyo usalama.
Watu wengi wanakaa kwenye ajira kwa sababu wanapenda usalama, ule uhakika wa kuwa na kazi na kipato mara zote. Japokuwa ajira hizo zinawanyima uhuru mkubwa wa maisha yao.
Unapotoka kwenye ajira kwenda kujiajiri, acha kutafuta usalama, badala yake yafuta uhuru. Unapokuwa huru, unaweza kujitengenezea usalama. Lakini ukitafuta usalama pekee, unajinyima uhuru.
- Penda utajiri mkubwa na siyo mshahara wa uhakika.
Tofauti kubwa ya kuwajiriwa na kujiajiri ni hii; ukiajiriwa kila mwezi una uhakika wa kupata mshahara, japo ni kidogo. Unapojiajiri, uhakika wa kipato kila mwezi haupo, ila kuna miezi utapata fedha nyingi sana, miezi mingine hutapata.
Badili mtazamo wako kutoka kupenda mshahara mdogo wa uhakika na upende utajiri mkubwa ambao kuna vipindi utakuwa na hali ngumu kifedha.
- Ona thamani kwenye kujitegemea na siyo kutegemea wengine.
Unapoajiriwa unamtegemea mwajiri wako na wafanyakazi wenzako kwa kila siku. Unapojiajiri unajitegemea wewe mwenyewe kwa kila kitu.
Unapoenda kujiajiri, unapaswa kubadili mtazamo wako kutoka utegemezi kwenda kujitegemea. Lazima ujue hakuna wa kukuongoza bali wewe mwenyewe, hakuna ambaye atabeba majukumu yako kama utashindwa au kukosea, bali wewe mwenyewe.
- Tengeneza sheria zako mwenyewe badala ya kufuata sheria za wengine.
Unapokuwa kwenye ajira, unakutana na sheria nyingi ambazo nyingine hukubaliani nazo, kwa sababu unaona hazina tija. Lakini huna nguvu ya kuzibadili kwa sababu wewe ni mwajiriwa tu. Unapokwenda kujiajiri mwenyewe, una nguvu ya kutengeneza sheria zako mwenyewe na kuzifuata, sheria ambazo zina maana kwako na zenye tija kulingana na kile unachofanya.
Hivyo usiende kujiajiri kwa kutumia sheria za wengine, bali tengeneza sheria zako mwenyewe.
- Penda kutoa maagizo badala ya kupokea maagizo.
Hapa ndipo waajiriwa wengi wanaposhindwa pale wanapojiajiri. Wanapokuwa wameajiriwa huwa wanasubiri kupewa maelekezo ya nini cha kufanya na wakifanyeje. Huwa hawajiongezi na kufanya kitu cha tofauti au kilicho bora zaidi.
Unapokwenda kujiajiri, lazima ujue kwamba hakuna mtu wa kukupa maelekezo na maagizo, wewe ndiye mtoaji wa maelekezo na maagizo. Hivyo lazima ujiamini na uwe tayari kujituma zaidi ya ulivyozoea ulipokuwa umeajiriwa.
SOMA; Hivi Ndivyo Kifafa Cha Ujasiriamali Kinavyowatesa Wale Wanaotoka Kwenye Ajira Na Kwenda Kujiajiri.
- Kubali kubeba majukumu yote badala ya kusema siyo jukumu langu.
Ukiwa umeajiriwa, unaweza kufanya makosa, lakini ukasingizia wengine na ukakwepa lawama hizo. Lakini unapokuwa umejiajiri, hakuna wa kumlaumu, kila kitu ni jukumu lako. Kila kosa unalofanya ni lako, na mbaya zaidi, hata kama umeajiri watu kwenye biashara yako, wakifanya makosa huwezi kuwalaumu, hayo ni makosa yako mwenyewe.
Jifunze kubeba majukumu kwenye kila unachofanya badala ya kutupa lawama kwa wengine au kusema hilo siyo jukumu langu. Unapojiajiri, kila kitu ni jukumu lako.
- Tengeneza utamaduni wa biashara yako badala kulazimika kupokea utamaduni wa wengine.
Unapokuwa umeajiriwa, huna uhuru mkubwa wa kupanga namna gani eneo lako la kazi liende. Huna nguvu ya kuchagua watu wa aina gani waajiriwe au ufanye nao kazi. Inabidi upokee utamaduni wa eneo lako la kazi.
Unapojiajiri, una uwezo wa kutengeneza utamaduni wa biashara yako iweje. Unaamua ni tabia zipi zinakubalika na zipi hazikubaliki. Unachagua ni aina gani ya watu watakaoajiriwa na wapi ambao hawataajiriwa kwenye biashara yako. Kwa kutengeneza vizuri utamaduni wa biashara yako, unakuwa na mazingira mazuri kwako kufanya kazi.
- Leta mabadiliko kwenye dunia badala ya kulalamikia matatizo ya dunia.
Sehemu kubwa ya waajiriwa ni watu wa kulalamika mara zote. Ni watu wa kuangalia matatizo na kusema hayawezekani au ni magumu. Ni watu wa kukata tamaa na kuona mambo ni magumu.
Huwezi kwenda na mtazamo huu kwenye kujiajiri na ukafanikiwa. Unapojiajiri, unapaswa kuwa mtu wa kuleta mabadiliko kwenye dunia badala ya kuwa mtu wa kulalamika. Usijihusishe kabisa na malalamiko ya wengine, wewe angalia ni matokeo gani unaweza kuyabadili na kazana kubadili hayo. Waachie wengine kazi hiyo ya kulalamika.
- Jua jinsi ya kutafuta matatizo na kuyageuza kuwa fursa.
Unapokuwa kwenye ajira, matatizo ni sehemu ya kujificha, sehemu ya kusingizia na kutafuta wa kulaumu. Unapokuwa umejiajiri, matatizo ni fursa za wewe kupiga hatua zaidi. Hivyo ondoka kwenye mtazamo wa kuyakimbia matatizo na nenda kwenye mtazamo wa kuyatafuta matatizo na kuyageuza kuwa fursa.
- Chagua kuwa mjasiriamali badala ya kuwa mwajiriwa.
Maisha ni kuchagua, unapata kile unachochagua. Hakuna mtu aliyezaliwa mjasiriamali, wala aliyezaliwa mwajiriwa. Haya ni machaguo ya maisha, ambayo tuliyafanya kwa kujua au kutokujua na kisha kuweka juhudi kuwa bora kwenye kile tulichochagua.
Kama umeamua kuingia kwenye ujasiriamali, basi chagua kuwa mjasiriamali kweli. Kubali kuwa wewe ni mjasiriamali, ishi maisha ya kijasiriamali na achana kabisa na maisha ya uajiriwa. Jifunze kila siku, kazana kuwa bora na utafanikiwa kwenye ujasiriamali.
Hizo ndizo falsafa kumi unazopaswa kujijengea ili uweze kufanikiwa pale unapotoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri.
Kuna mambo kumi ambayo Kiyosaki ametushirikisha kwenye kitabu chake cha Rich Dad’s Before You Quit Your Job: 10 Real-Life Lessons Every Entrepreneur Should Know About Building a Multimillion-Dollar Business, ambayo ni maandalizi unayopaswa kuwa nayo kabla hujaondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri. Utajifunza mambo hayo kumi kwenye makala ya TANO ZA JUMA hili la 34 la mwaka 2019. Usikose makala ya TANO ZA JUMA ili uwe na maandalizi sahihi ya kuanzisha na kukuza biashara yako baada ya kutoka kwenye ajira.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha