#TANO ZA JUMA #34 2019; Ushauri Uliopitwa Na Wakati, Mambo 10 Ya Kuzingatia Kabla Ya Kuacha Ajira, Falsafa 10 Za Kijasiriamali Unazopaswa Kujijengea, Ajira Pekee Haiwezi Kukupa Utajiri Na Hatari Kubwa Ni Kutokuchukua Hatari.
Rafiki yangu mpendwa,
Tumepata nafasi nyingine ya kukutana kwenye TANO ZA JUMA, makala inayokusanya mambo matano muhimu ya kujifunza na kuyaweka kwenye maisha yetu ili tuweze kupiga hatua zaidi.
Juma hili la 34 la mwaka 2019 tunakwenda kujifunza kwa kina kutoka kitabu kinachoitwa Rich Dad’s Before You Quit Your Job: 10 Real-Life Lessons Every Entrepreneur Should Know About Building a Multimillion-Dollar Business ambacho kimeandikwa na Robert Kiyosaki. Kiyosaki anajulikana kwa mfululizo wake wa vitabu vya RICH DAD, ambavyo vinatoa elimu ya kifedha kwa watu ili waweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.
Kwenye kitabu cha BEFORE YOU QUIT YOUR JOB, Kiyosaki ametushirikisha mambo 10 ambayo mtu anapaswa kuwa na maandalizi nayo kabla hajatoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri.
Wapo watu wengi ambao wapo kwenye ajira, wanatamani sana kutoka na kwenda kujiajiri, lakini wakiwaangalia wale waliowahi kutoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri, wanapatwa na hofu kubwa. Kwa sababu wengi wanakuwa hawajapiga hatua kubwa.
Sasa iwe upo kwenye ajira na unataka kwenda kujiajiri au tayari umeshajiajiri, masomo haya kumi tunayokwenda kujifunza hapa yatakusaidia sana kuanzisha na kukuza biashara yako.
Karibu sana kwenye TANO ZA JUMA, tujifunze, tuhamasike na kisha tuchukue hatua ili kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.
#1 NENO LA JUMA; USHAURI ULIOPITWA NA WAKATI.
Nenda shule, soma kwa bidii, faulu na utapata kazi nzuri na kuwa na maisha mazuri. Huu ni ushauri ambao wazazi wamekuwa wanawapa sana watoto wao. Ni ushauri ambao kipindi cha nyuma ulikuwa unafanya kazi, na hivyo watu waliuzingatia sana.
Lakini kwa zama tunazoishi sasa, huhitaji elimu kubwa kujua kwamba ushauri huo haufanyi kazi. Kwa sababu kama kuna eneo linatangaza nafasi kumi za kazi, halafu wanaoomba nafasi hizo wanakuwa zaidi ya 500, ni wazi kwamba watu wamefuata ushauri huo, kwa kufanya jukumu lao la kusoma, lakini kazi hazipo.
Hivyo basi, ushauri huo umepitwa na wakati, haufanyi tena kazi katika zama tunazoishi sasa. Kwa sababu nafasi za ajira zinazopatikana ni chache kuliko wingi wa wale wanaozitaka nafasi hizo.
Kwa kifupi, kuendelea kuufuata ushauri huu kwa uaminifu ni sawa na kugombania kupata nafasi kwenye meli ya MV Bukoba muda mchache kabla haijazama. Unakwenda kujipoteza mwenyewe.
Sasa neno la leo linakwenda kwa sisi wazazi au wazazi watarajiwa. Huenda tulishadanganywa kwa kauli hiyo, tuliiamini na kuifuata, lakini matokeo tuliyopata kwenye maisha siyo tuliyoyategemea. Hatuna haja ya kumlaumu yeyote, elimu hizi bora tunazoshirikishana, tunaweza kuzitumia na tukatoka popote ambapo tumekwama sasa.
Kuna eneo moja ambalo sisi wazazi au wazazi watarajiwa tunapaswa kulifanyia kazi, eneo hilo ni kwenye malezi ya watoto wetu. Naona wazazi wengi wanaendeleza ushauri huo wa soma kwa bidii na utapata kazi nzuri kwa watoto wao. Ushauri huo umeshapitwa na wakati, usiutumie tena kwa watoto wako.
Badala yake, wape ushauri huu; nenda shule, soma kwa bidii, jijengee ujuzi ambao utakuwezesha kutoa thamani kubwa kwa wengine, kuwa tayari kujituma kwenye chochote unachofanya na utakuwa na mafanikio makubwa kwenye maisha yako, iwe utaajiriwa au kujiajiri mwenyewe.
Ukiwapa watoto wako ushauri huu, na ukawasaidia kuwajengea tabia bora, kwa hakika utakuwa umewasaidia sana. Kwa sababu wanakua wakijua kilicho muhimu kwenye hii dunia siyo ufaulu wao wa darasani, bali thamani wanayoweza kuitoa kwa wengine, na utayari wao wa kujituma zaidi.
Huu ndiyo ushauri mpya, huu ndiyo ushauri unaofanya kazi na ndiyo ushauri ambao tunapaswa kuwapa watoto wetu na wengine wanaohitaji kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.
#2 KITABU CHA JUMA; MAMBO 10 YA KUZINGATIA KABLA YA KUACHA AJIRA.
Katika zama tunazoishi sasa, ipo wazi kwamba kipato cha ajira pekee hakitoshelezi kuendesha maisha. Na pia ajira zimekuwa zinawabana watu wasiweze kuwa na maisha wanayoyataka. Hii imepelekea wengi kupenda kuanzisha biashara za pembeni na hata kuondoka kwenye ajira zao.
Lakini wengi wamekuwa wanashindwa kufikia ndoto zao. Kuna wale ambao huwa wanaishia kufikiria na kupanga tu, lakini wasichukue hatua kutokana na hofu wanayokuwa nayo.
Na kuna wale ambao hujaribu kuchukua hatua, lakini wanashindwa vibaya, na wengi huishia kurudi kwenye ajira ambazo waliziacha na kwenda kuanza biashara au kujiajiri.
Mwandishi Robert Kiyosaki, kupitia uzoefu wake binafsi, anatushirikisha mambo ya kuzingatia kabla mtu hujaondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri. Kwenye kitabu chake cha BEFORE YOU QUIT YOUR JOB, Kiyosaki ametushirikisha masomo kumi ambayo kila anayetaka kutoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri anapaswa kuyazingatia.
Masomo haya pia yana msaada kwa mtu yeyote anayeendesha biashara, siyo tu kwa wale waliopo kwenye ajira.
Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, ujifunze masomo haya kumi, uyaweke kwenye matendo na uweze kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
SOMO LA KWANZA; BIASHARA YENYE MAFANIKIO INATENGENEZWA KABLA BIASHARA HAIJAANZA.
Takwimu za kibiashara zinasikitisha na kukatisha tamaa. Tafiti zimekuwa zinaonesha kwamba asilimia 90 ya biashara mpya zinazoanzishwa huwa zinakufa ndani ya miaka 5. Na zile zinazosalia, asilimia 90 zinashindwa kwenye miaka mitano inayofuata. Hivyo kama mwaka huu 2019 zimeanzishwa biashara 100, mwaka 2029 itakuwa imebaki moja pekee, 99 zitakuwa zimeshindwa na kufa.
Zipo sababu nyingi zinazopelekea kiwango hiki kikubwa cha biashara kufa, hizi ni baadhi;
- Mfumo wa elimu unafundisha watoto kuwa waajiriwa na siyo wajasiriamali.
- Ujuzi unaomsaidia mtu kwenye ajira hauwezi kumsaidia kwenye ujasiriamali.
- Mwanzo wa safari ya ujasiriamali ni mgumu, wengi hushindwa kuvumilia ugumu huo.
- Wengi wanaingia kwenye ujasiriamali wakiwa na uzoefu mdogo na hawana mtaji wa kutosha.
- Wengi wanakuwa na bidhaa au huduma nzuri, lakini hawana ujuzi w akutengeneza mfumo mzuri wa kuendesha biashara zao, wao wanakuwa ndiyo kila kitu, wanachoka na kuishia njiani.
Ili biashara ifanikiwe, kazi kubwa inapaswa kufanyika kabla hata biashara haijaanza. Kama mjasiriamali, unapaswa kuweka mipango na mikakati ya biashara yako vizuri kabla hata hujaanza. Kutengeneza mfumo mzuri wa kuendesha biashara hiyo, ambao utakupa wewe uhuru na kukuacha ufanye kazi ya kukuza biashara hiyo badala ya wewe kuwa ndiye wa kufanya kila kitu.
Kabla hujaondoka kwenye ajira yako, hakikisha umeshatengeneza mfumo wa biashara unayofanya au unayokwenda kufanya. Hivyo ni vyema kuanza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa, na ukaweza kutengeneza vizuri mfumo wa kuiendesha. Pia jifunze kwa wajasiriamali wenye mafanikio makubwa, na angalia jinsi wanavyoendesha biashara zao.
SOMO LA PILI; JIFUNZE KUGEUZA BAHATI MBAYA KUWA BAHATI NZURI.
Hofu ya kushindwa ndiyo sababu kuu kwa nini watu wengi wanashindwa kufanikiwa kwenye maisha. Mfumo wetu wa elimu na hata ajira umetengenezwa kwenye msingi wa kutokufanya makosa, kwa sababu ukikosea shuleni au kazini basi unaadhibiwa.
Lakini ulimwengu wa biashara upo tofauti kabisa, kama hukosei, huwezi kupiga hatua na kufanikiwa. Ni kupitia kukosea ndiyo uvumbuzi mpya unapatikana. Ni kupitia kukosea ndipo mtu unajifunza na kuwa bora.
Hivyo jukumu lako kubwa ni kugeuza bahati mbaya (makosa) kuwa bahati nzuri (mafanikio) kwa kutumia makosa yako kujifunza na kupiga hatua bora zaidi.
Ili kufanikiwa, mjasiriamali mpya anapaswa kupita hatua hizi;
- Kuanza biashara.
- Kushindwa na kujifunza.
- Kutafuta menta.
- Kushindwa na kujifunza.
- Kujifunza kupitia kozi mbalimbali.
- Kuendelea kushindwa na kujifunza.
- Kusimama pale anapofanikiwa.
- Kusherekea ushindi.
- Kuhesabu fedha zake, faida na hasara.
- Kurudia mchakato mzima.
Kabla hujaondoka kwenye ajira, anza kwanza biashara yako, shinda na jifunze mpaka unapokuwa umesimamisha biashara imara. Na kumbuka, kujifunza hakuna mwisho, makosa hayana mwisho, utaendelea kujifunza kadiri biashara inavyokwenda.
SOMO LA TATU; JUA TOFAUTI YA AJIRA NA KAZI.
Watu wengi wanalalamika kwamba hakuna kazi, lakini huo siyo ukweli. Kazi zipo nyingi sana, kitu ambacho hakipo ni ajira. Tofauti ya kazi na ajira ni hii; ajira ni kile kitu unachofanya ili ulipwe na kazi ni kile kitu unachofanya ili kutoa thamani au kutatua kitu fulani.
Unapotoka kwenye ajira na kwenda kuanzisha biashara, unapaswa kujua tofauti ya ajira yako na kazi ya biashara.
Kitu cha kwanza unachopaswa kuelewa ni kwamba, unaweza kuwa mwajiriwa mzuri sana, mwenye mafanikio makubwa na ambaye umepewa zawadi nyingi kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yako ya ajira, lakini ukienda kuanzisha biashara ukashindwa vibaya.
Kuwa mtu mzuri wa mauzo au masoko kwenye ajira yako, hakumaanishi utakuwa mjasiriamali mzuri.
Kuna maeneo makubwa matano kwenye kutengeneza mfumo wa biashara ambazo kila mjasiriamali mpya anapaswa kuyajua na kufanyia kazi ili afanikiwe. Maeneo hayo ni;
- Mzunguko wa fedha.
Kama mjasiriamali atakuwa na udhaifu kwenye eneo lolote hapo juu, basi biashara yake haiwezi kufanikiwa.
Tutajifunza kwa kina sana maeneo hayo matano kwenye makala ya #MAKINIKIA, usikose makinikia hayo.
SOMO LA NNE; MAFANIKIO YANADHIHIRISHA UDHAIFU WAKO.
Haijalishi mtu amejifunza biashara kwa kiasi gani, unapoingia kufanya biashara unajifunza mengi mno kwa kufanya kuliko kusoma. Moja ya vitu ambavyo wajasiriamali wapya hujifunza ni kwamba kadiri wanavyofanikiwa kwenye biashara zao, ndivyo wanavyoona madhaifu mengi waliyonayo kwenye biashara. Biashara inapokuwa ndogo kuna madhaifu mengi ambayo hutayaona, lakini biashara inapokua, ndivyo madhaifu yanavyoonekana wazi zaidi.
Hivyo kazi yako kubwa kama mjasiriamali ni kujiendeleza wewe binafsi na kuhakikisha kila eneo la biashara yako linajiendesha vizuri. Kila hatua unayopiga ni nafasi ya wewe kujifunza zaidi. Kila changamoto mpya unayokutana nayo ni nafasi ya wewe kuwa bora zaidi.
SOMO LA TANO; MCHAKATO NI MUHIMU KULIKO LENGO.
Wote tumejifunza na kujua umuhimu wa kujiwekea malengo kwenye maeneo mbalimbali ya maisha yetu. Hivyo hata kwenye biashara zetu, huwa tunajiwekea malengo ambayo tunayafanyia kazi.
Katika kufanyia kazi malengo yako, unapaswa kujua kwamba kilicho muhimu siyo kufikia lengo ulilojiwekea, bali kilicho muhimu ni ule mchakato wa kulifikia lengo hilo. Mchakato ndiyo unakufanya wewe kuwa mtu bora, kukuwezesha kupiga hatua zaidi.
Unapoungia kwenye biashara, kazana kukua kama mjasiriamali na siyo kukazana kupata mafanikio kwenye biashara unayoifanya. Wengi huingia kwenye biashara kwa tamaa ya kupata fedha na wakishazipata ndiyo wanaishia hapo, wengi hushindwa vibaya.
Unapokuwa mjasiriamali bora, hata kama utapoteza kila kitu, utaweza kuanzia chini kabisa na ukafanikiwa tena. Lakini unapokuwa umekazana tu kufikia lengo bila ya wewe kuwa bora, unaposhindwa huwezi tena kuanza.
SOMO LA SITA; MAJIBU BORA YANAPATIKANA KWENYE MOYO, SIYO KWENYE KICHWA.
Mafanikio ya biashara yoyote ile yanaanzia kwenye maono ya biashara husika, pamoja na misheni ambayo mwanzilishi wa biashara hiyo anayo. Kama maono na misheni ni kubwa, na yanayogusa maisha ya wengine, biashara ina nafasi kubwa ya kufanikiwa. Lakini kama mtu anaanzisha biashara kwa sababu zake binafsi, labda kama sehemu ya kujiongezea kipato pekee, biashara hiyo inakuwa vigumu kufanikiwa.
Kitu cha kwanza kabisa unachopaswa kuwa nacho kwenye biashara unayoifanya ni kupenda biashara hiyo. Kuipenda kutoka ndani ya moyo wako na siyo kuipenda kwa sababu kuna manufaa utapata. Kitu cha pili ni kuwajali wale ambao ni wateja wa biashara hiyo, usiwaone tu kama wateja ambao wanakuletea faida, bali waone kama watu ambao wewe una jukumu la kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi ya yalivyo sasa. Vitu hivi vinaanzia ndani ya moyo wako na vinaonekana kwa matendo zaidi kuliko maneno.
SOMO LA SABA; UKUBWA WA MAONO UNAAMUA UKUBWA WA BIASHARA.
Biashara haiwezi kukua zaidi ya maono ambayo mwanzilishi wa biashara hiyo anakuwa nayo.
Kwenye kitabu cha CASHFLOW QUADRANTS, Kiyosaki ametushirikisha njia kuu nne za kuingiza kipato. Njia hizo ni kama ifuatavyo;
- Kuajiriwa (EMPLOYMENT – E)
- Kujiajiri (SELF EMPLOYED – S)
- Biashara (BUSINESS – B)
- Uwekezaji (INVESTMENT – I)
Ufafanuzi zaidi wa njia hizi nne utaupata kwenye makala ya #MAKINIKIA.
Sasa kosa kubwa ambalo watu wengi wamekuwa wanalifanya ni kutaka kutoka kwenye kuajiriwa E na kwenda moja kwa moja kwenye biashara B, bila ya kupitia kujiajiri S. Kiyosaki anasema njia bora ni kutoka kwenye E kwenda kwenye S kisha kuingia kwenye B. Lakini unaanza ukiwa na maono makubwa a kuwa na biashara kubwa, ila unachukua hatua ndogo ndogo kuyafikia. Kwa kuchukua hatua ndogo ndogo unaenda kujifunza na kukua bila ya kutengeneza matatizo makubwa.
Biashara yako inapaswa kutimiza kimoja kati ya hivi viwili; kutatua tatizo au kutimiza hitaji. Ukishaanza na kile ambacho biashara yako inafanya, kuwa na maono makubwa ya kuwafikia wengi zaidi na kutengeneza mfumo bora wa kufikia maono hayo.
SOMO LA NANE; TENGENEZA BIASHARA AMBAYO ITAFANYA KITU AMBACHO BIASHARA NYINGINE HAZIWEZI KUFANYA.
Biashara yako lazima iwe tofauti kabisa na biashara nyingine kama unataka ifanikiwe. Kama kila unachofanya kinaweza kufanywa na biashara nyingine, kama kila unachotoa mteja anaweza kukipata kwa wengine, hakuna sababu ya wewe kuwepo kwenye biashara hiyo.
Kiyosaki anashauri uwe na kitu cha tofauti na kisha kukikatia hatimiliki ili wafanyabiashara wengine wasiweze kukiiga. Iwe ni bidhaa, huduma au mchakato, tumia ubunifu wako kuja na kitu kipya na ukishakipata, kiwekee hatimiliki ambayo inawazuia wengine wasiweze kuiga na kutumia.
Wewe kama kiongozi wa biashara yako, una majukumu makubwa nane;
- Kueleza kwa uwazo maono, malengo na misheni ya kampuni.
- Kutafuta watu bora ambao utawatumia kutengeneza timu bora ya biashara yako.
- Kuimarisha kampuni kwa ndani.
- Kuikuza kampuni kwa nje.
- Kukuza faida.
- Kuwekeza kwenye utafiti na maendeleo.
- Kuwekeza kwenye mali za kampuni.
- Kuwa kiongozi bora wa biashara.
Zipo njia mbalimbali za kuikuza zaidi biashara yako;
- Kufungua tawi jipya la biashara yako kwenye eneo tofauti.
- Kuwapa watu leseni ya kuendesha biashara kama yako na wakakulipa.
- Kushirikiana na wengine katika kuzalisha na kuuza bidhaa au huduma yako.
Ili uweze kushindana na kushinda kwenye ushindani mkali uliopo kwenye biashara, kuwa na kitu cha tofauti, kinachopatikana kwako tu na hakuna mwingine anayeweza kukiiga.
SOMO LA TISA; USIPIGANIE KUPATA WATEJA WA BEI RAHISI.
Wateja wa biashara yako wanaweza kuwa chanzo cha wewe kushindwa kibiashara. Unapaswa kuwa makini sana wakati wa kufanya maamuzi ya kuchagua wateja wa aina gani unaotaka kuwahudumia kwenye biashara yako.
Ni muhimu kuchagua aina gani ya wateja utakaowahudumia vizuri, kisha kuweka nguvu zako kuhudumia wateja hao, na kuachana na wengine wote. Unapopata mteja ambaye haendani na wateja unaotaka kuwahudumia, basi unamfukuza mara moja.
Sehemu nzuri ya kuanzia kuchagua wateja wa biashara yako ni kwenye bei. Hakikisha unakuwa na bidhaa au huduma bora, kisha kuchaji gharama ya juu kuliko wengine. Hii itakufanya upate wateja wachache, lakini wanakuwa wateja bora, wanaothamini unachofanya na wasio na usumbufu. Lakini kama utachagua kuhudumia wateja wa bei rahisi, utawapata wengi, lakini pia watakusumbua sana. Wateja wa bei rahisi ndiyo huwa wanataka vitu ambavyo haviendani na kiasi wanacholipia, wanaolalamika kwa kila kitu na hupenda kutumia njia mbalimbali kunufaika zaidi ya wanavyolipa.
Ukishagundua aina hii ya wateja kwenye biashara yako, waondoe mara moja ili nguvu zako uzipeleke kwa wale wateja wachache bora.
Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanakwama kwa sababu wanataka kila mtu awe mteja wa biashara zao na wanaona kufukuza wateja ni kupoteza fedha. Lakini ukweli ni kwamba utapata faida kubwa kwa kuwahudumia watu wachache vizuru kuliko kuwahudumia watu wengi vibaya.
SOMO LA KUMI; JUA WAKATI SAHIHI WA KUACHA AJIRA YAKO.
Kutokuipenda kazi yako siyo sababu sahihi kwako kuingia kwenye ujasiriamali. Unaweza kuona ni kitu kinachokusukuma, lakini utakapokutana na magumu kwenye safari ya ujasiriamali, sababu hiyo pekee haitaweza kukuvusha. Unapaswa kuwa na maono na visheni kubwa inayokufanya uingie kwenye ujasiriamali.
Kabla hujacha ajira yako, hakikisha unafanyia kazi yafuatayo;
- Badili mtazamo wako kuhusu ajira na ujasiriamali.
- Jitengenezee uzoefu wa kutosha kwenye mfumo wa biashara.
- Mara zote kumbuka MAUZO = KIPATO, kupata zaidi, uza zaidi.
- Kuwa na matumaini lakini pia kuwa mkweli kwako mwenyewe.
- Kuwa na nidhamu nzuri kwenye matumizi ya fedha.
- Anza biashara ukiwa kwenye ajira, kama sehemu ya kujifunza.
- Kuwa tayari kuomba msaada.
- Tafuta menta.
- Jiunge na mtandao wa wajasiriamali wengine.
- Kuwa mwaminifu kwa mchakato wa ujasiriamali.
Ukizingatia mambo hayo kumi, utaweza kuondoka kwenye ajira yako na kuendesha biashara ambayo ulishaianza mapema na kuweza kukua zaidi.
Rafiki haya ndiyo masomo 10 tunayojifunza kutoka kwenye kitabu cha BEFORE YOU QUIT YOUR JOB. Kama ambavyo umeona, yanagusa kila eneo la biashara. Hivyo kazi ni kwako kuyaweka mafunzo haya kwenye vitendo ili uweze kunufaika zaidi.
Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili utakwenda kujifunza pembetatu muhimu ya kuanzisha na kukuza biashara, ambayo ina vitu 8 unavyohitaji kufanyia kazi ili kuweza kuanzisha biashara inayokupa utajiri wa mabilioni. Soma mwisho wa makala hii kujua jinsi ya kuyapata #MAKINIKIA.
#3 MAKALA YA JUMA; FALSAFA 10 ZA KIJASIRIAMALI UNAZOPASWA KUJIJENGEA.
Watu waliopo kwenye ajira, wakiwaangalia watu ambao wamejiajiri huwa wanawaonea wivu sana. Huwa wanajiambia na mimi nikiweza kujiajiri kama wengine, nitakuwa huru sana. Nitaamua saa ngapi niamke, nifanye kazi masaa mangapi na nitakuwa bosi wangu mwenyewe, hakuna wa kunipelekesha.
Ni mpaka pale wanapoingia kwenye kujiajiri ndiyo wanakutana na ukweli wenyewe, kwamba mambo siyo rahisi kama yanavyoonekana kwa nje. Wengi wanapouonja ukweli huu, huwa wanarudi kwenye ajira na kukubaliana na maisha ya ajira, hata kama siyo bora kwao.
Kama unataka kuondoka kwenye ajira na kwenda kujiajiri au kama unataka kujiajiri au umeshajiajiri mwenyewe, kuna falsafa kumi za kijasiriamali unazopaswa kujijengea, ambazo zitakuzuia usiyumbishwe na mambo mapya utakayokutana nayo.
Kwenye makala yetu ya juma tumejifunza falsafa hizi kumi muhimu. Kama hukusoma makala ya juma, unaweza kuisoma sasa hapa; Falsafa Kumi (10) Za Kijasiriamali Unazopaswa Kujijengea Unapotoka Kuajiriwa Na Kwenda Kujiajiri.
Usiache kusoma makala hiyo, hata kama upo kwenye biashara kwa muda mrefu, kuna misingi mizuri ya kujifunza, ambayo huenda hujaijua na hivyo inakukwamisha.
Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku uendelee kujifunza kupitia makala nzuri zinazowekwa kila siku.
#4 TUONGEE PESA; AJIRA PEKEE HAIWEZI KUKUPA UTAJIRI.
Tukirudi kidogo kwenye ushauri uliopitwa na wakati, ahadi ilikuwa ni kwamba, ukishapata ajira, basi maisha yako yamekamilika. Maana utadumu na ajira hiyo kwa muda mrefu na ukifika miaka 60 utastaafu ajira na kupewa mafao yako ambayo yatakuwezesha kuishi maisha mazuri kwa muda uliobaki nao hapa duniani.
Sasa kama unataka ugomvi na watu, watafute wastaafu na waulize vipi mafao waliyopata yamewafikisha wapi. Kwanza sehemu kubwa hawajapata mafao yao kama walivyotarajia kuyapata. Na kwa wale walioyapata, wengi wanajikuta wameyatumia vibaya na maisha yanakuwa magumu zaidi kwao.
Kuna tatizo kubwa sana kwenye huu ushauri, hasa upande wa maandalizi ya baadaye. Dunia nzima kuna tatizo kubwa kwenye hii mifuko ya hifadhi ya jamii. Ili mfuko uweze kumlipa mstaafu mmoja kwa ukamilifu, unahitaji kuwa na wachangiaji watatu kwenye mfuko huo. Sasa ukiangalia mwenendo wa ajira, ajira zinazidi kupungua kadiri siku zinavyokwenda. Hivyo hesabu hiyo ya wachangiaji watatu kumtoa mstaafu mmoja haziwezi kukamilika. Na hivyo kadiri siku zinavyokwenda ndivyo mifuko hii inakuwa kwenye wakati mgumu kuwalipa wastaafu.
Hii ni kukuambia kwamba, kama upo kwenye ajira, au unataka kuingia kwenye ajira ukitegemea unapostaafu utalipwa mafao ambayo yatakuwezesha kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako, unajidanganya. Kwa zama hizi hicho kitu hakipo, kadiri siku zinavyokwenda ndivyo inakuwa vigumu kwa mifuko hii kuweza kuwalipa watu mafao yao.
Hivyo basi, kama upo kwenye ajira na unataka kuwa na maisha mazuri ukiwa kwenye ajira hiyo na hata baada ha kustaafu, lazima ujue kwamba ajira pekee haiwezi kukupa matakwa yako hayo. Badala yake unahitaji kuwa na vitu vya pembeni unavyofanya huku ukiendelea na ajira yako.
Unapaswa kuwa na njia mbadala za kukuingizia kipato na siyo kutegemea ajira pekee. Na njia hizi zipo nyingi, kuanzia kuanzisha biashara, kutumia vipaji au uzoefu wako na hata kufanya uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali.
Kwenye kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA, nimefundisha hili kwa kina sana. Kama bado hujakisoma kitabu hiki, kipate na ukisome leo. Kama tayari unacho, rudia tena kukisoma leo. Kukipata tuma ujumbe kwenda namba 0717396253 na utapewa maelekezo ya kukipata.
Iwe upo kwenye ajira au umejiajiri, unapaswa kujua kwamba njia ya kukupeleka wewe kwenye utajiri na uhuru wa kifedha ni kuwa na vyanzo mbadala vya kipato. Na unapaswa kufanyia hilo kazi kila siku. Kuwa na chanzo kimoja, hata kama ni biashara ni kujiwekea ukomo. Tengeneza vyanzo mbadala vya kipato na utajijengea uhuru mkubwa kwenye maisha yako.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; HATARI KUBWA NI KUTOKUCHUKUA HATARI.
“In today’s rapidly changing world the people who are not taking risks are the risk takers. People who are not taking risks are falling behind.” —Robert Kiyosaki
Kuna watu ambao wamekuwa wanaogopa kuanzisha biashara kwa sababu ni kitu cha hatari. Hivyo wanaona ni salama kutegemea ajira pekee na kutokujisumbua na biashara ambazo zinaweza kushindwa.
Kwa zama tunazoishi sasa, zama zenye mabadiliko makubwa na ya kazi, hatari kubwa ni kutokuchukua hatari kabisa. Kuogopa kuanzisha biashara na kuona ajira ndiyo salama ni hatari kubwa sana kwenye maisha yako. Kwa sababu kama tunavyojua, ajira za sasa siyo salama tena. Unaweza kupoteza ajira uliyoitumikia kwa miaka 20 kwa dakika tano tu za kutokuelewana na mwajiri au bosi wako.
Hivyo kama unataka kuepuka hatari kwenye maisha yako, basi chukua hatari zaidi. Ni kweli baadhi ya hatari utakazochukua zitashindwa, baadhi zitakuumiza, lakini hatari zote zitakujenga na kukufanya kuwa imara zaidi.
Kuwa mtu wa kuchukua hatua za hatari, na siyo kwa hatari yake, bali kwa sababu ndiyo njia pekee ya wewe kupiga hatua zaidi. Na kumbuka kupima kila hatari kabla hujaingia. Siyo kwa sababu umeambiwa kuchukua hatari ndiyo kufanikiwa basi ukakimbilia kila aina ya hatari. Ingia kwenye hatari ambayo upo tayari kupambana nayo.
TAFAKARI YA NYONGEZA; UJASIRIAMALI SIYO KAZI.
“Entrepreneurship is a process, not a job or profession. So be faithful to the process and remember that even when times are bad, the process will give you a glimpse of the future that lies ahead.” —Robert Kiyosaki
Leo nakupa tafakari ya nyongeza kutoka kwa Robert Kiyosaki ambaye tumejifunza mengi kutoka kwenye kitabu chake.
Robert anatuambia ujasiriamali siyo kazi wala cheo, wala taaluma. Bali ujasiriamali ni mchakato, ni mfumo wa maisha. Hivyo unapochagua kuwa mjasiriamali, unaufanya ujasiriamali kuwa maisha yako na hivyo huuachi kwa sababu mambo ni magumu. Badala yake unaweka imani yako kwenye mchakato mzima, ukijua ipo njia na kwa hakika njia itajitokeza mbele yako.
Nimekupa tafakari hii ya nyongeza kwa sababu ina nguvu sana, ina nguvu ya kutuzuia tusikate tamaa na kuishia njiani pale mambo yanapokuwa magumu. Ina nguvu ya kutusukuma zaidi, kwa kujua kwamba njia ipo, hata kama hatuioni kwa sasa.
Na kwa kumalizia, acha kutumia neno ujasiriamali kama cheo au sifa, badala yake ishi ujasiriamali. Maana siku hizi kila mtu akiulizwa anafanya nini anasema ni mjasiriamali, lakini ukiyaangalia maisha yake, hayana hata chembe ya ujasiriamali. Chagua kuuishi ujasiriamali na utakuwa na maisha bora na yenye uhuru mkubwa.
Rafiki, hizi ndizo TANO ZA JUMA hili la 34 la mwaka 2019, ambazo zimetupa funzo kubwa kuhusu kuanzisha na kukuza biashara, hasa kwa wale ambao wanaanzia kwenye ajira. Iwe upo kwenye ajira au la, masomo haya ni muhimu, yaweke kwenye matendo na utaweza kufanikiwa sana.
Kwenye #MAKINIKIA ya juma hili la 34 tunakwenda kujifunza njia kuu nne za kuingiza kipato kama ambavyo Kiyosaki anatufundisha kwenye CASHFLOW QUADRANTS na pia tutaangalia pembetatu muhimu ya kuanzisha na kukuza biashara, ambayo ina vitu 8 unavyohitaji kufanyia kazi ili kuweza kuanzisha biashara inayokupa utajiri wa mabilioni. Pembetatu hii Kiyosaki anaiita B-I TRIANGLE, kwa nje ina vitu vitatu vinavyoibeba biashara na ndani kuna vitu vitano vinavyoikuza biashara. Yote haya unapaswa kuyajua kama unataka kufanikiwa kwenye biashara. Hivyo usikubali kabisa kuyakosa #MAKINIKIA ya juma hili.
Kuyapata #MAKINIKIA ya juma, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA JUMA iliyopo kwenye mtandao wa telegram. Maelekezo ya kujiunga yako hapo chini.
#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.
Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.
Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.
Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu