#TANO ZA JUMA #20 2019; Kufanya Kazi Ndani Na Nje Ya Biashara, Imani Potofu Kuhusu Ujasiriamali, Kifafa Cha Ujasiriamali Kinavyowatesa Wengi, Mashine Ya Kuchapa Fedha Na Kama Biashara Yako Inakutegemea Hiyo Siyo Biashara Bali Kazi.
Hongera sana rafiki yangu mpendwa kwa juma hili bora sana ambalo tumekuwa nalo na tunakwenda kulimaliza. Naamini lilikuwa juma la kipekee sana kwako, juma ambalo umeweza KUJIFUNZA maarifa sahihi na ukayaweka kwenye VITENDO ili kuweza kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Umefika wakati mzuri kwetu kulimaliza juma hili la 20 kwa ‘dozi’ sahihi ya maarifa, maarifa ambayo yanakwenda kutujenga na kutufanya kuwa bora zaidi kwa siku zijazo za maisha yetu.
Kwenye juma hili la 20 la mwaka huu 2019 tunakwenda kujifunza kuhusu imani potofu ambazo zimekuwepo kwenye ujasiriamali. Watu wengi wanaojiita wajasiriamali siyo wajasiriamali, badala yake ni wachuuzi ambao wao ndiyo biashara zao. Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara wakiwa na mipango mizuri na mikubwa, lakini wanaishia kushindwa kabisa au wasiposhindwa basi wanadumaa, hawakui.
Kupitia kitabu tunachokwenda kujifunza kwa juma hili, kitabu kinachoitwa The E-Myth Revisited: Why Most Small Businesses Don’t Work and What to Do About It mwandishi Michael E. Gerber anatupa maarifa sahihi ya kutuwezesha kuanzisha na kuendesha biashara zetu kwa mfumo ambao zinafanya vizuri na kutupa uhuru mkubwa. Michael anasema uhuru kwenye biashara upo kwenye mfumo. Kama unaendesha biashara na huna mfumo, huna biashara, bali una kazi, na hiyo ni kazi mbaya kuliko zote.
Karibu kwenye tano hizi za juma, tujifunze mfumo sahihi wa kuendesha biashara zetu kwa mafanikio makubwa.
#1 NENO LA JUMA; KUFANYA KAZI NDANI NA NJE YA BIASHARA.
Watu wengi ambao wapo kwenye biashara hawajui kama wanafanya kazi ndani ya biashara au nje ya biashara, na hilo ndiyo tatizo kubwa sana linalopelekea biashara nyingi kufa. Kabla sijakueleza tofauti hizi, je unajua kama unafanya kazi ndani ya biashara yako au nje ya biashara yako?
Chukua mfano huu; umeanzisha biashara yako, ambapo wewe ndiye unayefanya kila kitu kwenye biashara hiyo. Wewe ndiye mzalishaji au mwandaaji wa bidhaa au huduma unazotoa, wewe ndiye mtu wa masoko, wewe ndiye mtu wa mauzo, wewe ndiye mtu wa fedha na wewe ndiye mtu wa huduma kwa wateja. Kwa majukumu yote haya, hutapata muda wa kufanya majukumu makubwa ya biashara yako kama kuweka mipango ya ukuaji zaidi wa biashara hiyo.
Kwa mfano huo mdogo, unapata picha ya kufanya kazi ndani ya biashara na kufanya kazi nje ya biashara.
Kufanya kazi ndani ya biashara yako (working IN your business) ni pale ambapo biashara inakutegemea wewe kwa kila kitu. Wewe ndiyo biashara na biashara ni wewe. Bila ya uwepo wako biashara haiwezi kwenda. Na pia majukumu yako ya biashara yanakuchosha kiasi kwamba huwezi kupata muda wa kufikiria makubwa kwa ajili ya biashara hiyo. kufanya kazi ndani ya biashara ndiyo kikwazo kwa ukuaji wa biashara nyingi. Wafanyabiashara huanzisha biashara wakiwa na nia njema ya kukua, lakini wanamezwa na kazi za biashara hiyo na hawapati muda wa kufikiria makubwa kuhusu biashara hiyo.
Kufanya kazi nje ya biashara yako (working ON your business) ni pale unapoiangalia biashara kama mmiliki na siyo mfanyakazi. Hapa unapata muda wa kuondoka kwenye majukumu ya kila siku ya biashara na kutengeneza maono makubwa ya biashara hiyo. Kwa kufanya kazi nje ya biashara yako, unaona mbali zaidi kupitia biashara hiyo na unaweza kuweka mipango na mikakati ya ukuaji wa biashara yako. Kufanya kazi nje ya biashara yako ndiyo njia pekee unaweza kuikuza biashara yako na ikafanikiwa zaidi.
Najua kwa kusoma tofauti hizi mbili, ni rahisi kujiambia wanaoweza kufanya kazi nje ya biashara zao ni wale wenye biashara kubwa na ambao wameajiri watu wa kufanya kazi kwenye biashara hizo. Lakini huo siyo ukweli, hata kama majukumu yote ya biashara yako unayafanya wewe, bado unaweza kufanya kazi nje ya biashara yako na kuweza kuikuza zaidi.
Kitu cha kufanya kama wewe ndiye mfanyakazi pekee wa biashara yako, ni kutenga muda na siku za kufanya kazi nje ya biashara yako. Kila siku kabla ya kuanza siku yako ya kibiashara, tenga muda wa kufanya kazi nje ya biashara yako, huu ni muda ambao unapitia malengo yako makubwa kibiashara, unapitia yale uliyofanya kwenye siku uliyopita na pia kuangalia fursa mbalimbali unazoweza kuzifanyia kazi kupitia biashara hiyo. Ni muhimu ufanye hili mapema kabla hujaanza kufanya kazi ndani ya biashara yako, maana siku ya biashara ikishaanza, unatingwa sana na mwisho wa siku unakuwa umechoka sana.
Pia siku moja kila wiki tenga muda wa kutosha zaidi kufanya kazi nje ya biashara yako. Huu ni muda ambao unapitia yale uliyofanya kwa wiki nzima, unazipitia namba zako muhimu za kibiashara kama mauzo, matumizi, faida, wateja waliohudumiwa, wateja wapya na kadhalika. Namba hizi zinakupa picha wapi biashara inakwenda. Pia huu ni wakati wa kupitia na kuboresha mikakati yako ya kibiashara na kuangalia jinsi gani unaweza kuifikia.
Nikuambie kitu kimoja rafiki yangu, kama hutatenga kwa makusudi muda wa kufanya kazi nje ya biashara yako, kwa kujiambia uko bize kufanya kazi nje ya biashara yako, jua utakuwa mtumwa wa biashara hiyo maisha yako yote. haijalishi upo bize kiasi gani, tenga muda w akufanya kazi nje ya biashara yako na hilo litakuwezesha kununua uhuru wako kutoka kwenye biashara hiyo.
#2 KITABU CHA JUMA; IMANI POTOFU KUHUSU UJASIRIAMALI.
Siku hizi kila mtu aliyepo kwenye biashara anajiita mjasiriamali au mfanyabiashara mdogo. Lakini ukiangalia kwa undani wanachofanya watu hao, hakiendani kabisa na wanachopaswa kufanya wajasiriamali au wafanya biashara. Tunachoweza kuwaita wengi waliopo kwenye biashara ni wamejiajiri wenyewe, na wanachofanya ni ufundi ambao wanalipwa kupitia wanachofanya au kuzalisha.
Mwandishi Michael Gerber kwenye kitabu chake kinachoitwa E-Myth Revisited: Why Most Small Businesses Don’t Work and What to Do About It, ameeleza dhana hii potofu ambayo wengi wanayo kuhusu biashara na ujasiriamali. Michael ametueleza kwa nini biashara nyingi ndogo zinakufa na hatua za kuchukua ili kunusuru biashara zetu zisife.
Kama upo kwenye biashara au unapanga kuingia kwenye biashara basi jifunze kwa kina sana mambo haya, kwani yataokoa muda na nguvu nyingi utakazopoteza kwa kufanya biashara zako kwa namna umezoa kufanya.
TATIZO LA BIASHARA YAKO NI WEWE.
Kama biashara yako ina tatizo, basi wewe ndiye mwenye tatizo na siyo biashara hiyo. Japokuwa biashara yako ni kitu kinachojitegemea, lakini huwa inabeba tabia zako wewe kama mmiliki wa biashara hiyo.
Kama wewe ni mzembe basi biashara yako nayo itaenda kizembe, kama uko makini basi biashara yako itakuwa makini.
Hivyo somo la kwanza kabisa kutoka kwa Gerber kuhusu kuendesha vizuri biashara zetu ni kujijua sisi wenyewe kwanza. Kama hutajijua wewe mwenyewe na kujua uimara na mapungufu yako, hutaweza kuijua biashara yako na kuiendesha vizuri.
Kadhalika kwenye ukuaji wa biashara yako, biashara yako haiwezi kukua kukuzidi wewe mmiliki wake. Kama wewe mwenyewe hukui, biashara yako haiwezi kukua. Hivyo kama unataka kuendesha biashara ambayo inakua zaidi kila wakati, basi anza wewe kukua kila wakati. Wekeza kwenye ukuaji wako kwa kujifunza maarifa sahihi ya kuendesha biashara yako.
Kama umechagua kuwa mjasiriamali au mfanyabiashara, kuna kitu kingine umekichagua bila ya wewe mwenyewe kujua. Umechagua kuwa mwanafunzi maisha yako yote, umechagua kuwa mtu wa kujifunza kila siku ya maisha yako. Na kama hujifunzi kila siku, utaendelea kuwadanganya wengine kwamba wewe ni mfanyabiashara au mjasiriamali, lakini hakuna unachofanya kitakachoashiria vitu hivyo.
Rafiki yangu mpendwa, jikumbushe kauli hii kila siku, kama biashara yako ina tatizo, basi tatizo la biashara hiyo ni wewe. Kama biashara yako haikui, basi ambaye hakui ni wewe. Biashara yako ni kama kioo kinachokuonesha wewe ni nani. Itumie kuhakikisha unakuwa bora zaidi wewe mwenyewe na hata biashara yako pia.
NAFSI TATU ZILIZOPO NDANI YAO UNAZOPASWA KUZIJUA ILI KUFANIKIWA KWENYE BIASHARA.
Watu wengi wanaoingia kwenye biashara na ujasiriamali wanaishia kuwa wamejiajiri na mafundi wazuri lakini hawakui. Hii ni kwa sababu kuna nafsi tatu ambazo zipo ndani ya kila mmoja wetu ambazo zinahusika na biashara. Lakini wengi huwa wanajua na kutumia nafasi moja pekee.
Kipengele namba tatu hapo chini, cha makala ya JUMA, kimeeleza kwa kina kuhusu nafsi hizi tatu, soma kipengele hicho na fungua makala ya juma ili uzielewe nafsi hizo tatu na jinsi ya kuzitumia vizuri kwa mafanikio ya biashara yako.
Kama hutazijua nafsi hizo tatu, huwezi kufanikiwa kwenye biashara, utakazana sana lakini kama tulivyojifunza hapo juu, tatizo linabaki kuwa wewe.
HATUA TATU ZA UKUAJI WA BIASHARA.
Kuna hatua tatu muhimu za ukuaji wa biashara ambazo kila biashara inazipitia. Biashara zinazofanikiwa zinafika kwenye hatua ya tatu. Biashara zinazoshindwa zinaishia kwenye hatua ya kwanza au ya pili. Ni muhimu sana kuzijua hatua hizi tatu na mambo ya kufanya kwenye kila hatua ili kuweza kufanikiwa kwenye biashara.
Hatua ya kwanza; UCHANGA.
Hapa biashara inakuwa changa, na inamtegemea mwanzilishi wake kwa kila kitu. Hapa biashara haina tofauti na mtoto mchanga ambaye anamtegemea mama yake kwa kila kitu.
Katika hatua hii ya biashara, mfanyabiashara anakuwa ndiyo biashara na biashara inakuwa mfanyabiashara. Yeye ndiye anayefanya kila kitu kwenye biashara hiyo.
Hatua hii huwa ni ya furaha kwa wengi, kwa sababu mtu anakuwa anapenda kufanya anachopenda kufanya, ana uhuru kwa kuwa anafanya kitu chake na hajaajiriwa na kwa kuwa anajituma, basi wateja wanamsifia kwa huduma nzuri sana. Mfanyabiashara anafurahia sana maisha na biashara yake katika hatua ya uchanga, kama ambavyo watoto huwa wanayafurahia maisha wasijue majukumu makubwa yaliyopo mbele yao.
Kwa namna ambavyo mfanyabiashara anajituma kwenye biashara hiyo, inakua kwa kasi sana mwanzoni, na hapo inaelekea kwenye hatua ya pili ya biashara hiyo.
Hatua ya pili; UJANA.
Hii ni hatua ambayo biashara inakua kwa kasi sana, wateja wanazidi kuwa wengi na majukumu ya biashara yakuwa mengi. Hapa mfanyabiashara anakuwa anaanza kuchoshwa na biashara hiyo, majukumu yanakuwa mengi na muda wa kuyafanyia kazi yote hana.
Hapa mfanyabiashara anapata wazo, kwa kuwa biashara imekua basi anaweza kuajiri mtu wa kumsaidia. Na kweli anaajiri mtu wa kumsaidia, na kumgawia baadhi ya majukumu yake kwenye biashara hiyo. Hapa anapata uhuru mkubwa na anabaki na majukumu machache anayopenda kuyafanyia kazi.
Biashara inazidi kukua na hivyo uhitaji wa kuajiri zaidi unakuwepo. Na kwa kuwa biashara inakua na kutengeneza faida, kuajiri inakuwa siyo tatizo, watu wanazidi kuajiriwa.
Lakini inafika hatua ambapo biashara imekua sana, na wafanyakazi kwenye biashara hiyo ni wengi, lakini hakuna matokeo mazuri yanayozalishwa. Bidhaa au huduma zinachelewa, wateja wanalalamika na biashara inaonekana kuwa imevurugika.
Katika hatua kama hii, mwanzilishi wa biashara anajikuta kwenye wakati mgumu, mwanzo aliipenda biashara yake, alijituma sana, lakini sasa hivi biashara imekuwa mzigo kwake. Ameajiri watu wa kumsaidia lakini watu hao wamekuwa kazi zaidi kwake.
Na hapa wengi hufanya maamuzi magumu, maamuzi ya kurudi kwenye uchanga, kuifanya biashara hiyo kuwa ndogo kiasi ambacho wanaweza kuidhibiti wenyewe na kuondokana na usumbufu wa kuhangaika na watu wengi. Na hii huwa ndiyo njia ya kufa kwa biashara nyingi.
Kwa wafanyabiashara wachache, wale wanaofanikiwa, huwa wanaenda hatua ya tatu ya ukuaji wa biashara.
Hatua ya tatu; UKOMAVU.
Biashara inakuwa imefikia hatua ya ukomavu pale ambapo hamtegemei mwanzilishi wake au mtu yeyote katika kujiendesha. Hapa biashara inakuwa na mifumo inayofanya kazi, ambapo mtu yeyote akiwekwa kwenye mfumo huo anaweza kuzalisha matokeo yanayotarajiwa.
Biashara komavu ndiyo inawapa watu uhuru na mafanikio makubwa.
Wachache wanaopitia hatua ya ujana wa biashara, wanajifunza kwamba ili waweze kudumu kwenye biashara, wanapaswa kuacha kuajiri watu bila mpangilio na badala yake kutengeneza kwanza mfumo na majukumu ya kazi kisha kuajiri watu ambao watatekeleza majukumu hayo.
Kwa kuanza na mfumo kisha majukumu ya kazi, biashara inapoajiri watu inapunguza usumbufu wa mmiliki wa biashara kuanza kuhangaika na wafanyakazi mmoja mmoja na badala yake kuhangaika na mfumo.
BIASHARA BORA ZINAANZA KAMA BIASHARA KOMAVU.
Sasa kwa mtiririko wa hatua hizi tatu, ni rahisi kuona kwamba ili ufanikiwe kwenye biashara unapaswa kuanzia kwenye hatua ya uchanga, uhangaike mwenyewe kisha uende kwenye hatua ua ujana ukue zaidi na kufikia hatua ya ukomavu. Lakini hilo siyo sahihi.
Biashara bora huwa zinaanza kama biashara komavu, kisha kupitia hatua za uchanga, ujana na ukomavu zikiwa tayari ni komavu.
Hili linamaanisha kwamba, kabla mtu hajaanza biashara yako anakaa chini kwanza na kutengeneza mfumo wa kuendesha biashara hiyo, anatengeneza nafasi za watu kufanya kazi na majukumu yao kisha ndiyo anaingia kwenye biashara.
Hivyo hata anapoanza mwenyewe, tayari anakuwa na mfumo na hata anapofanya kazi kwenye biashara yake anajua majukumu ya kila nafasi. Jinsi mtu anavyoendelea kukua, anapoajiri hafanyi makosa ambayo wengi wanayafanya kwenye hatua ya ujana wa biashara, kosa la kuajiri mtu ambaye hana majukumu kamili anayosimamia. Anayeanza biashara na mifumo iliyo tayari anapoajiri mfanyakazi wa kwanza anajua kabisa majukumu yake yanakuwa yapi na anapimwaje kwa majukumu hayo.
Kwa kuanza biashara ukiwa tayari na mfumo, inakusaidia kuwa huru kadiri unavyokua. Kwa mfano unapokuwa umetengeneza nafasi ya mauzo na masoko kwenye biashara yako, na kuorodhesha majukumu yote ya nafasi hiyo, siku unapoajiri mtu wa masoko na mauzo unampa majukumu hayo na kisha kumpima kwa utekelezaji wake. Huhitaji tena kuendelea kumsimamia mtu huyo kila wakati, kwa sababu majukumu yake yanakuwa wazi. Hilo linakupa wewe uhuru wa kuweka nguvu zako kwenye maeneo mengine.
Haijaishi kwa sasa upo kwenye hatua ipi kibiashara, kaa chini sasa kutengeneza mfumo bora wa kuendesha biashara yako. Mafanikio kwenye biashara ni matokeo ya kuwa na mfumo bora wa kuendesha biashara hiyo.
Kwa wale watakaohitaji huduma ya kutengeneza mfumo bora wa kuendesha biashara zao tuwasiliane kwa wasap 0717396253, kuna huduma bora ambayo itakusaidia sana kwenye kutengeneza mfumo bora wa kuendesha biashara yako na kujipa uhuru sana baadaye.
ENDESHA BIASHARA UNAYOWEZA KUIUZA.
Kama umewahi kula kwenye migahawa inayoandaa vyakula vya haraka (fastfood) kama McDonalds, KFC, Pizza Hut na mingineyo, utakuwa umegundua kwamba haijalishi umekula kwenye mgahawa gani, huduma zao zinafanana. Yaani kama utakula kwenye McDonalds iliyopo eneo moja, ukienda McDonalds iliyopo eneo jingine huduma ni zile zile. Unaweza kujiuliza inawezekanaje biashara moja iliyopo kwenye maeneo tofauti kutoa huduma ambazo zinafanana kabisa.
Na jibu ni moja, ni kwa sababu biashara hizo zinaendeshwa kwa mfumo ambao ndiyo unafanya biashara hizo kufanikiwa. McDonald haifanikiwi kwa sababu ya vyakula wanavyopika, bali wanafanikiwa kwa sababu ya mfumo bora walionao kwenye kuendesha biashara hizo.
Biashara hizi zimekuwa zinaendeshwa kwa mtu kupewa kibali cha kufungua biashara hiyo kwenye eneo ambalo haipo, lakini kwa kufuata mfumo ambao anapewa na wamiliki wa biashara. Mfumo huu unaitwa FRANCHISE, ni mfumo bora sana wa kuendesha biashara zenye matawi mengi. Unapopewa kibali cha kuendesha biashara hiyo, unafuata mfumo kama ulivyoeleza na huruhusiwi kuongeza kitu chochote kile, hata kama utaona ni kizuri kiasi gani.
Mfumo huu umekuwa unaleta matokeo mazuri na kwa miaka mingi haujashindwa.
Hivyo basi, kama wewe unataka kuendesha biashara ambayo itafanikiwa na kukupa uhuru, lazima uiendeshe kama biashara ambayo unataka kuiuza au kutoa leseni wengine wakaifanye.
Unapaswa kuwa na mfumo wa kuendesha biashara hiyo, ambao una nafasi zote za biashara hiyo pamoja na majukumu ya kila nafasi. Kila kitu kinapasa kuwa kimeandikwa na jinsi biashara inavyofanyika. Mtu anapoajiriwa kwenye biashara hiyo hafanyi vile anavyojisikia, bali anafanya kama mwongozo wa biashara na mfumo unavyomtaka afanye.
Kwa kuendesha biashara yako kwa mfumo na miongozo, inakuhakikishia kupata matokeo bora wakati wote na pia kukupa wewe uhuru. Huhitaji kuwa kwenye biashara wakati wote kuwaelekeza watu nini cha kufanya, kila mtu anajua nini anapaswa kufanya na anapaswa kufanya hicho na siyo kile anachojisikia yeye kufanya.
MCHAKATO WA MAENDELEO YA BIASHARA.
Katika kuendeleza biashara yako, upo mchakato ambao unapaswa kuufanyia kazi. Mchakato huu ndiyo unaokuwezesha kutengeneza mfumo na kuuboresha na kuwapa watu majukumu ya kufanyia kazi kwenye mfumo huo.
Mchakato wa maendeleo ya biashara una vipengele vitatu;
Kipengele cha kwanza ni UVUMBUZI, hapa unakuja na wazo au njia bora ya kufanya chochote unachofanya kwenye biashara yako. Siyo lazima kiwe kitu kikubwa sana, inaweza kuwa jinsi wateja wanasalimiwa, jinsi wanavyohudumiwa, mavazi wanayovaa waliopo kwenye biashara na kadhalika. Kwenye uvumbuzi ndipo unakuja na mawazo mbalimbali ya kuboresha zaidi biashara yako.
Kipengele cha pili ni TATHMINI, hapa mtu unaweka kwenye matendo ule uvumbuzi unaokuwa umekuja nao. Unapofanyia kazi uvumbuzi wako, unapima matokeo ambayo unayapata na kisha kufanya tathmini. Kama matokeo ni mazuri basi unaendelea kufanyia kazi hatua hiyo. Kama matokeo siyo mazuri unarudi kwenye kipengele cha uvumbuzi na kufikiria njia bora zaidi ya kufanya.
Kipengele cha tatu ni MAJUMUISHO, hapa hatua ulizochukua na kupata matokeo mazuri zinajumuishwa kwenye mfumo wa biashara. Hapa sasa inakuwa ni kitu ambacho lazima kila mtu akifanye. Siyo mtu anakifanya kama anajisikia kufanya, bali ni lazima akifanye. Kwa mfano kama umegundua watu wa mauzo wakivaa shati na tai wanauza zaidi, basi uvaaji wa shati na tai unakuwa sehemu ya mfumo wa biashara na ni lazima kila mtu wa mauzo avae shati na tai, siku kwa kupenda, bali ni lazima. Kwa sababu upo tayari kupoteza fedha kwa kuruhusu watu waache njia inayoleta fedha zaidi na kufanya kile wanachojisikia kufanya? Kwa hakika hakuna awezaye kufanya hivyo.
Mchakato huu wa maendeleo ya biashara yako, yaani UVUMBUZI, TATHMINI NA MAJUMUISHO ni endelevu. Siyo kitu cha kufanya mara moja halafu ukawa umemaliza. Hili ndiyo jukumu lako kubwa kama mmiliki wa biashara, kila wakati kuja na uvumbuzi wa kuboresha zaidi biashara yako, kufanyia tathimini na kujumuisha kwenye mfumo kama matokeo yake ni mazuri. Na utaweza kufanya hivi kama utaacha kufanya kazi ndani ya biashara na kufanya kazi nje ya biashara yako.
HATUA SABA ZA KUTENGENEZA MFUMO WA KUENDESHA BIASHARA YAKO.
Baada ya kujifunza misingi muhimu ya kuendesha biashara yako kwa mfumo, sasa tunakwenda kujifunza hatua saba za kutengeneza mfumo bora wa kuenesha biashara yako.
Kwa kuzijua na kufanyia kazi hatua hizi saba, utaweza kuwa na biashara inayojiendesha yenyewe, yenye mafanikio makubwa na inayokupa uhuru. Kwa kukamilisha hatua hizi saba na kuzisimamia vizuri, siyo tu unakuwa na biashara, bali unakuwa na mashine ya kuchapa fedha.
Hatua ya kwanza; KUSUDI LAKO KUU.
Hatua ya kwanza ya kufanikiwa kwenye biashara ni kujua kusudi lako kuu kwenye maisha.
Kama hujui wapi unataka kufika na maisha yako, hutajua biashara sahihi kwako kuanzisha na biashara yoyote utakayoanzisha hutaweza kudumu nayo.
Pata picha ya maisha yako miaka 20 ijayo, unajiona ukiwa wapi, miaka kumi ijayo unajiona wapi, kadhalika kwa miaka mitano na hata mitatu. Pata taswira ya jinsi unavyoyaendesha maisha yako, mafanikio uliyonayo na kila kitu kama unavyotaka kiwe.
Hili ndiyo kusudi kuu la maisha yako na hili litakusaidia kujua biashara ipi ufanye na unaifanyaje.
Hatua ya pili; MKAKATI WA KUFIKIA KUSUDI.
Baada ya kujua kusudi kuu la maisha yako, sasa unajiuliza unawezaje kufika pale? Umeshajiona unapotaka kuwa miaka kumi ijayo, je utafikaje pale?
Jua kabisa kwamba hakuna muujiza utakaokufikisha kwenye ndoto zako, kuna hatua unapaswa kuchukua, na hapa ndipo biashara yako inapoingia.
Chagua biashara ambayo inaendana na kusudi lako la maisha na jinsi unavyojiona kwenye picha yako ya miaka 10 au 20 ijayo.
Kisha weka mkakati wa jinsi unavyoweza kuitumia biashara yako kufikia ndoto yako kubwa.
Jua kiwango cha mauzo na mapato unachopaswa kutengeneza kwa mwaka kupitia biashara yako ili kufikia lengo, na hapo weka mkakati wa jinsi ya kufikia mauzo hayo. Jua ukubwa wa biashara unaopaswa kuwa nao na kama kuna matawi basi idadi ya matawi ya biashara hiyo.
Vyote hivi vinapaswa kuwa kwenye mkakati wako, ione biashara yako ikiwa kubwa na jinsi unavyofika kwenye ukubwa huo.
Hatua ya tatu; MKAKATI WA UENDESHAJI WA BIASHARA.
Baada ya kujua biashara unayokwenda kufanya na ukubwa wake, unapaswa kuweka mkakati wa jinsi biashara hiyo itakavyoendeshwa.
Hapa ndipo unapotengeneza nafasi zote za biashara yako na majukumu ya kila nafasi. Mfumo huu ndiyo utakaotumika kwenye kuendesha biashara, kuajiri, kukuza na hata kufukuza wafanyakazi.
Kwa kuwa na mkakati wa kuendesha biashara, unajua kabisa nani anasimamia nini na anawajibika kwa nani. Mfano unaweza kuwa na mkakati wa uendeshaji wa biashara yako ambapo biashara inamilikiwa na mwanzilishi wa biashara, ambapo chini yake anakuwa mkurugenzi mkuu, chini ya mkurugenzi kunakuwa na mameneja wa vitengo mbalimbali vya biashara, mfano masoko, mauzo, fedha na kadhalika. Chini ya mameneja hao sasa ndiyo kunakuwa na watekelezaji wa majukumu ya kila siku ya biashara. Hii inakupa wewe mmiliki uhuru, kwa sababu mkurugenzi atawajibika kwako, ambaye mameneja watawajibika kwake na mameneja watakuwa na watu walioko chini yao ambao wanawasimamia. Hii ina maana kama kuna kitu hakiendi vizuri, kinafanyiwa kazi kwenye ngazi za chini kabla hakijafika kwako kama mmiliki au mkurugenzi mkuu.
Unapaswa kutengeneza mkakati huu mwanzo kabisa hata kabla hujawa na wafanyakazi.
Hatua ya nne; MKAKATI WA USIMAMIZI.
Baada ya kuwa na mkakati wa uendeshaji wa biashara, unahitaji mkakati wa uongozi. Hapa ni jinsi ambavyo watu watasimamiwa na kuhamasisha kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwenye biashara.
Unapaswa kuwa na mkakati ambao unawafanya watu kutekeleza majukumu yao kwa kuchagua wao wenyewe na siyo kwa kulazimishwa. Hivyo majukumu yanapaswa kuwa wazi na njia za kupimwa kuwa wazi kwa wote, kisha mtu kupimwa ufanisi wake kupitia majukumu yake.
Unapaswa kuwa na mwongozo ulioandikwa wa majukumu ambayo mtu anapaswa kutekeleza, ambapo inakuwa rahisi kufuatiliwa kama ametekeleza kweli. Mfumo bora wa usimamizi ndiyo utakuwezesha kupata matokeo bora wakati wote bila ya kujali nani anayefanya kazi hiyo.
Hatua ya tano; MKAKATI WA KUPATA WATU BORA.
Kama ambavyo tumejifunza, ukishakuwa na mfumo mzuri, unahitaji kupata watu bora wa kuendesha mfumo huo ili uweze kuzalisha matokeo unayotaka.
Unahitaji kupata watu sahihi wa kuendesha biashara yako, na hapo utatumia mkakati wako wa uongozi kuwapata. Unapotafuta watu wa kuwaajiri, kwanza hakikisha wanayaelewa majukumu yao na jinsi wanapimwa nayo. Wanaambiwa kila wanachopaswa kutekeleza na kukabidhiwa miongozo yao ya kazi.
Kwa kuajiri watu kwa njia hii, utawapata walio sahihi, maana mtu anapoambiwa kabla majukumu yake ni yapi na atapimwaje, kama atakubali itamlazimu kutekeleza kile alichokubali. Lakini kama unaajiri watu bila ya majukumu na njia ya kuwapima, watakusumbua.
Hatua ya sita; MKATATI WA MASOKO.
Masoko ndiyo roho ya biashara yako, masoko ndiyo yanaleta wateja kwenye biashara yako na kuwashawishi kununua. Hivyo ili biashara yako ifanikiwe inahitaji kuwa na mkakati bora wa masoko.
Katika mkakati wako wa masoko unapaswa kuzingatia vitu vinne muhimu;
Moja; mteja wa biashara yako ni nani, lazima ujue sifa za mteja wa biashara yako, na jinsi ambavyo biashara yako inamnufaisha au kutatua changamoto zake.
Mbili; mteja wa biashara yako anapatikana wapi, lazima ujue mteja alipo ili ujue unawezaje kumfikia na biashara yako.
Tatu; njia sahihi za kumfika mteja huyo, baada ya kujua mteja ni nani na anapatikana wapi, hapa unaweka mkakati sahihi wa kumfikia. Kama ni ana kwa ana, matangazo na kwa njia gani. Yote haya lazima yawe kwenye mkakati ambao watu wanafanyia kazi.
Nne; nini kinamsukuma mteja wako kuchukua hatua lazima ujue tamaa au maumivu ambayo mteja wako anayo. Na hicho kinachomsukuma kununua ndiyo utakachotumia kumshawishi unapomfikia, iwe ni ana kwa ana au kwa matangazo.
Tengeneza mkakati sahihi wa masoko na biashara yako itaweza kukua sana.
Hatua ya saba; MKAKATI WA MFUMO.
Hatua hii inajumuisha kwa pamoja hatua zote sita tulizojifunza hapo juu. Hapa unakuwa na mkakati wa mfumo ambao unaleta mikakati yote pamoja kwa ajili ya kuzalisha matokeo bora kwenye biashara yako.
Hapa ndipo biashara yako inapounganishwa na kuwa kitu kimoja, na wewe kuwa kama dereva ambaye unaiwasha na inaenda, bila ya kuhusika moja kwa moja kwenye kila kipengele.
Kwenye mkakati wa mfumo kuna mifumo mitatu muhimu ya kufanyia kazi;
Moja ni mfumo mgumu, huu unahusisha vitu vyote vinavyoshikika vya biashara yako. Mfano eneo la biashara, mapambo yaliyopo, rangi zilizopakwa, usafi wa eneo la biashara, mavazi ya wafanyakazi, vifaa vinavyotumika na kadhalika, yote haya yanajumuisha mfumo mgumu. Lazima kila kitu kiendane na mfumo mzima wa biashara.
Mbili ni mfumo tete, huu unahusisha mawazo yote yaliyopo kwenye biashara, michakato yote inayofanyika kwenye biashara, mfano jinsi mteja anavyohudumiwa, mchakato ambao mtu anaufuata katika kumshawishi mteja kununua na mengine.
Tatu ni mfumo wa taarifa, huu ni mfumo ambao unapima ufanisi wa biashara. Kila kinachofanyika kwenye biashara lazima kipimwe, na hapo ndipo mtu unaweza kufanya tathmini kuona wapi matokeo ni mazuri na wapi siyo mazuri.
Kwa kufanyia kazi mifumo hii mitatu, utaweza kuendesha vizuri biashara yako, kwa mafanikio makubwa na ikakupa uhuru mkubwa kwenye maisha yako.
Rafiki, hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza mfumo bora wa kuendesha biashara yako, fanyia kazi mafunzo haya kwenye biashara yako ili uweze kufanikiwa.
FURSA YA KUTENGENEZA BIASHARA YAKO KWA MFUMO.
Rafiki, kama umejifunza hapa kuhusu faida na jinsi ya kuendesha biashara yako kwa mfumo, na umeona ni kitu ambacho unahitaji ili kufanikiwa, basi nakukaribisha tufanye kazi pamoja ya kukuwezesha kutengeneza biashara yako kwa mfumo.
Ninayo programu ambayo nafanya kazi na wafanyabiashara ambao wanaendesha biashara zao kwa mfumo rahisi kwao kuzifuatilia na kupata watu sahihi pamoja na kupanga na kupima ukuaji wa biashara hiyo.
Kama unataka kuwa mmoja wa wafanyabiashara waliopo kwenye programu hii, basi nitumie ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717396253 kwenye ujumbe andika PROGRAMU YA KUENDESHA BIASHARA KWA MFUMO, na nitakutumia maelekezo ya programu hiyo.
Karibu sana.
#3 MAKALA YA JUMA; KIFAFA CHA UJASIRIAMALI KINAVYOWATESA WENGI.
Tukiwa bado tunajifunza kuhusu imani potofu ambazo watu wanazo kuhusu biashara na ujasiriamali, mwandishi Michael Gerber anatushirikisha dhana moja anayoiita kifafa cha ujasiriamali.
Najua unajua kuhusu kifafa, mtu anapatwa na hali fulani ya mwili kustuka, ambayo inadumu kwa muda mfupi na kupotea yenyewe.
Michael anasema hivi ndivyo wengi wanavyoingia kwenye biashara, wanapata na mshtuko wa ghafla kwamba njia pekee ya wao kuwa huru na maisha yao ni kuingia kwenye biashara. Hali hiyo inawasukuma kuingia kwenye biashara. Lakini kwa kuwa ni kifafa, hakidumu kwa muda mrefu. Kinaondoka haraka na hapo ndipo matatizo ya biashara na ujasiriamali yanazaliwa na mateso ambayo yanawasumbua wengi yanapoanzia.
Michael ametushirikisha nafsi tatu zilizopo ndani ya kila mmoja wetu na jinsi ya kuzitumia kufanikiwa kwenye biashara na ujasiriamali.
Kwenye makala ya juma hili nimekushirikisha kwa kina kuhusu hili la kifafa cha ujasiriamali na nafsi hizo tatu za kuzijua na kuzitumia vizuri ili kufanikiwa kwenye biashara. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo ya juma unaweza kuisoma sasa hivi hapa; Hivi Ndivyo Kifafa Cha Ujasiriamali Kinavyowatesa Wale Wanaotoka Kwenye Ajira Na Kwenda Kujiajiri.
Hii ni makala ambayo kila aliyepo kwenye biashara au anapanga kuingia kwenye biashara anapaswa kuisoma. Hivyo usifanye kitu kingine chochote kama hujasoma makala hiyo, utakuwa unajizuia mwenyewe kufanikiwa, hasa kama hujazijua nafsi tatu zilizopo ndani yako. Fungua hiyo makala na uisome sasa.
#4 TUONGEE PESA; MASHINE YA KUCHAPA FEDHA.
Watu wengi wamekuwa wanahangaika sana kupata njia rahisi ya kutengeneza fedha. Katika harakati hizi wapo ambao wameweza kutengeneza mashine za kutengeneza fedha feki na wengine wamekuwa wanaiba na kutapeli. Njia zote hizo hata kama zitakupa fedha, lakini utatumia sehemu kubwa ya fedha hizo kukimbia au kujificha. Kwa kifupi unaweza kupata fedha, lakini maisha yako hayatakuwa na uhuru wowote.
Ninachotaka kukuambia wewe rafiki yangu ni kwamba unao uwezo wa kutengeneza mashine inayochapa fedha, mashine inayozalisha fedha kadiri utakavyo wewe mwenyewe. Na uzuri wa mashine hiyo ni kwamba ni halali kabisa, na utakuwa huru na fedha utakazozipata kwa sababu huvunji sheria yoyote ile.
Mashine hiyo haihitaji fedha nyingi ili kuitengeneza, ila inahitaji kazi na muda na ukiweza kuitengeneza kwa usahihi, itakuwa inachapa fedha usiku na mchana, ukiwa umelala au umesafiri, mashine inachapa fedha tu.
Je upo tayari kujua mashine hiyo ya kuchapa fedha ambayo unaweza kuwa nayo?
Kama jibu ni ndiyo basi umeshajifunza hapa, kupitia kitabu cha juma hili.
Mashine ya kuchapa fedha ni kuwa na biashara ambayo inaendeshwa kwa mifumo na haitegemei uwepo wako wa moja kwa moja.
Yaani unaanzisha biashara, ambayo umeitengenezea mifumo ya kuendesha biashara hiyo na kuiweka vizuri kwenye biashara hiyo, unapata watu sahihi wa kuendesha mifumo hiyo na mifumo inaleta matokeo mazuri ambayo ni faida.
Mifumo ya biashara ikishakuwa sawa, na ukaweka watu sahihi wa kuendesha mifumo hiyo, hapo unakuwa huru na maisha yako na kazi yako ni kuvuna faida tu. Je hapo siyo sawa na kuwa na mashine ya kuchapa fedha.
Kama una kitu kinachokuingizia fedha ukiwa umelala, umesafiri, unaumwa au unafanya kingine chochote ambacho hakihusiani na kuzalisha fedha, ila fedha zinaingia tu, je hiyo siyo mashine ya kutengeneza fedha?
Na je kwa kupitia haya tuliyojifunza leo, hujaona jinsi ilivyo rahisi kwako kutengeneza mashine hii?
Ninachokuambia ni kimoja rafiki yako, nenda kaweke mifumo kwenye biashara yako, miaka ya mwanzo utahitaji kuweka kazi kubwa, lakini baada ya hapo, utakuwa unavuna tu.
Kama utahitaji msaada zaidi wa jinsi ya kutengeneza mifumo bora ya kuendesha biashara yako na kukupa wewe uhuru wa maisha yako tuwasiliane kwa wasap namba 0717396253, ninayo programu maalumu ya wafanyabiashara ambao wananufaika sana na kuendesha biashara zao kwa mfumo sahihi.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; KAMA BIASHARA YAKO INAKUTEGEMEA HIYO SIYO BIASHARA BALI KAZI.
“If your business depends on you, you don’t own a business—you have a job. And it’s the worst job in the world because you’re working for a lunatic!” ― Michael E. Gerber
Kama biashara yako inakutegemea kwa kila kitu, basi hiyo siyo biashara bali ni kazi. Na ni kazi mbaya sana kuwa nayo duniani, kwa sababu bosi wako amevurugwa.
Ni afadhali kufanya kazi ya kuajiriwa, ambayo unapewa majukumu yanayoeleweka na unafanyia kazi majukumu hayo tu.
Lakini unapokuwa kwenye biashara ambayo inakutegemea wewe kwa kila kitu, huna majukumu maalumu, kila kitu kinakutegemea wewe hivyo maisha yanakuwa magumu sana. Kadiri biashara hiyo inavyokua ndivyo maisha yako yanakuwa magumu zaidi. Na hata ndoto kwamba biashara hiyo itakupa uhuru inafifia kabisa kwa sababu wewe ni biashara na biashara ni wewe.
Jukumu lako la kwanza kwenye biashara ni kununua uhuru wako, kuhakikisha biashara haikutegemei wewe kwa kila kitu. Hakikisha biashara yako haimtegemei mtu yeyote, bali biashara inategemea mfumo. Biashara ikishategemea mfumo, ni rahisi kuweka watu kwenye mfumo huo na wakaendesha biashara.
Kama uko kwenye biashara ambayo inakutegemea wewe kwa kila kitu, ni wakati wa kufanya maamuzi sasa. Fanya maamuzi ya kutengeneza mifumo kwenye biashara hiyo ambayo itakuweka huru. Au fanya maamuzi ya kuondoka kabisa kwenye biashara hiyo na kutafuta mtu wa kukuajiri. Maamuzi yoyote kati ya hayo mawili ni bora kwako kuliko kubaki kwenye biashara inayokutegemea kwa kila kitu.
Rafiki, hivi ndiyo tano za juma la 20, ni imani yangu umepata mwanga mkubwa sana juu ya kuendesha biashara kwa mifumo, ambapo utakuwa huru kutoka kwenye biashara yao. Nenda kayaweke mafunzo haya kwenye biashara yako, na kama bado hujawa na biashara unasubiri nini? Umeshapata mafunzo haya mazuri, hivyo unaweza kuanza ukiwa na mpango mzuri kuliko wale walioanza na kupotea.
Kwenye #MAKINIKIA nitakwenda kukushirikisha jinsi unavyoweza kutengeneza kusudi lako la maisha, mambo muhimu ya kuzingatia kwenye mkakati wa kufikia kusudi, jinsi ya kutengeneza mfumo wa kuendesha biashara yako, mambo ya kuzingatia kwenye usimamizi na kuajiri watu sahihi, jinsi ya kutengeneza mkakati bora wa masoko na mfumo bora utakaokuwezesha kuuza zaidi kwenye biashara yako.
#MAKINIKIA yanapatikana kwenye channel ya TANO ZA JUMA kwenye mtandao wa telegram, hakikisha umejiunga na channel hii ili kupata maarifa hayo adimu sana kwa ukuaji wa biashara yao. Maelekezo ya kujiunga na channel hii yako hapo chini.
#PATA KITABU NA UCHAMBUZI ZAIDI.
Rafiki yangu mpenda, kama ungependa kupata kitabu tulichochambua kwenye makala hii ya tano za juma, pamoja na kupata uchambuzi wa mafunzo zaidi kutoka kwenye kitabu hiki, karibu ujiunge na channel ya TANO ZA MAJUMA 52 YA MWAKA.
Hii ni channel ambayo ipo kwenye mtandao wa TELEGRAM MESSENGER, ambapo kila juma nakutumia kitabu cha juma, uchambuzi huu na mafunzo ya ziada yote kwa mfumo wa pdf ambapo utaweza kusoma na hata kuhifadhi vizuri kwa matumizi ya baadaye. Pia kwa kujiunga na channel hii, utaweza kupata mafunzo yote ya nyuma na hata ukipoteza mafunzo hayo utaweza kuyapakua tena muda wowote unapoyataka.
Ada ya kujiunga na channel hii ni ndogo mno, ni shilingi elfu moja tu kwa wiki. Au unaweza kuchagua kulipa kwa mwezi (elfu 3) au kwa mwaka (elfu 30). Lakini wiki ya kwanza ni bure na hulipi chochote. Karibu ujiunge leo bure kwa kutuma ujumbe kwa njia ya telegram kwenda namba 0717396253. Ujumbe uwe na maneno TANO ZA MAJUMA YA MWAKA.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu