“I will keep constant watch over myself and—most usefully—will put each day up for review. For this is what makes us evil—that none of us looks back upon our own lives. We reflect upon only that which we are about to do. And yet our plans for the future descend from the past.”
—SENECA, MORAL LETTERS, 83.2
Tumeiona siku nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu rafiki.
Tumeipata nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari MAPITIO YA SIKU YAKO…
Kila unapoimaliza siku yako, tenga muda wa kuipitia siku hiyo.
Ipitie siku yako tangu unaianza mpaka unaimaliza.
Mambo gani ulipanga kufanya na umeyatekelezaje.
Umewezaje kuzidhibiti fikra zako kwenye siku hiyo?
Kipi cha tofauti ulichofanya kwenye siku hiyo?
Kitu gani kipya ambacho umejifunza?
Wapi ambapo hukufanya vizuri na unahitaji kurekebisha kwa siku zijazo?
Kama anavyotuambia mstoa Seneca, huwa tunakazana kufikiria kile tunachokwenda kufanya na kusahau ambacho tumeshafanya na hivyo kujikuta tunarudia yale yale ambayo tumeyakosea siku za nyuma.
Unapoipitia siku yako, unapotafakari kila ulichofanya unajipa nafasi ya kuona ulipokosea na kuweza kujirekebisha.
Utakachofanya kesho, kinaathiriwa sana na ulichofanya leo. Hivyo ipitie leo yako na ujifunze kwa kila ulichofanya na jinsi ya kufanya kwa ubora zaidi wakati mwingine.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kufanya tafakari na mapitio ya siku yako pale unapoimaliza, ili uweze kujua sehemu za kuchukua hatua uwe bora zaidi.
#MalizaSikuKwaTafakari, #IpitieSikuInayoisha, #KuwaBoraKilaSiku
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha