Mabadiliko kwenye maisha yetu ni matokeo ya hatua tunazochukua na siyo maneno au mipango tuliyojiwekea.

Hata kama mipango ni mikubwa kiasi gani, hata kama tunaweza kuielezea na kubishana kiasi gani, hakuna matokeo tutakayoyapata kama hakuna hatua tunayochukua.

Nakukumbusha hili rafiki, ili kila mara ujue wapi pa kupeleka nguvu zako kama unataka kupata matokeo ya tofauti na unayopata sasa.

Maana inaonekana siku hizi watu wanafikiri maisha yao yatabadilika kwa kuwa na mipango au kuongea sana kuhusu mabadiliko. Huko ni kupoteza muda na nguvu.

Ni bora kuchukua hatua ndogo kuliko kutokuchukua hatua kabisa. Ni bora kuanza na kidogo kuliko kutokuanza kabisa.

Utajifunza mengi kwa kuanza kufanya hata kama hujawa tayari kuliko kuendelea kusubiri ukijipanga au kuzungumzia makubwa unayotaka kufanya.

Na pia kadiri unavyoweka nguvu nyingi kwenye kufanya na siyo kusema au kubishana, ndivyo unavyopiga hatua zaidi kuelekea kwenye kile unachotaka. Muda wowote unaotumia kusema au kubishana ni muda unaoutoa kwenye kufanya na hivyo unakuwa unajichelewesha.

Nasisitiza hili rafiki kwa sababu kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, watu hawawezi kufanya kitu na kutulia nacho, wanakimbilia haraka kuweka wazi kwenye mitandao ya kijamii na wanashangaa kwa nini kila mara wanakwama.

Unapoanza kufanya kitu, weka nguvu kubwa kwenye kuchukua hatua kuliko kwenye kusema au kuonesha nini unafanya. Zuia ule msukumo unaokujia wa kutaka kuweka kwenye mitandao kila unachofanya na peleka nguvu hiyo kwenye kuchukua hatua zaidi.

Kuchukua hatua, hata kama ni kidogo kiasi gani kutakusukuma zaidi kuliko kusema au kupanga, hata kama mipango ni mikubwa kiasi gani.

Peleka nguvu zako kwenye kuchukua hatua zaidi kuliko kupanga zaidi na kusema zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha