Rafiki yangu mpendwa,

Matumizi ya fedha zetu ni moja ya vikwazo vikubwa kwenye kufikia utajiri na uhuru wa kifedha. Haijalishi mtu una kipato kikubwa kiasi gani, kama matumizi yako ni makubwa kuliko kipato, upo kwenye matatizo makubwa.

Ipo kauli moja fupi sana lakini yenye funzo kubwa sana. Kauli hii inasema kama kipato chako ni laki moja na matumizi yako ni elfu tisini na tisa una akili, lakini kama kipato chako ni shilingi laki moja na matumizi yako ni laki moja na mia moja una matatizo makubwa.

Matumizi yamekuwa kikwazo kwa wengi kufikia utajiri na uhuru wa kifedha kwa sababu wengi hawawezi kudhibiti matumizi yao. Wengi pale kipato kinapoongezeka na matumizi nayo yanaongezeka. Wakati mwingine yanaonekana kama yanaongezeka yenyewe na yote ni muhimu.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Kwenye makala ya leo nakwenda kukushirikisha vigezo vitano vya kutumia katika kufanya maamuzi ya matumizi ya fedha zako. Kwa kutumia vigezo hivi, utaweza kuyadhibiti sana matumizi yako na ukaweza kubaki na fedha za kuweka akiba na kuwekeza.

Vigezo vitano vya kutumia kufanya maamuzi ya fedha zako;

Moja; HITAJI LA MAISHA.

Kigezo cha kwanza muhimu kabisa kutumia ni hitaji la maisha, je kitu unachotaka kufanya na fedha zako ni hitaji la maisha? Kwamba usipokifanya basi maisha hayawezi kwenda?

Hiki ni kigezo muhimu kabisa na unapaswa kuwa makini unapokitumia. Unaposema hitaji la maisha maana yake ni kama lisipotimizwa basi maisha hayawezi kwenda. Hapa vinaingia vitu kama chakula, mavazi, makazi, afya na kadhalika.

Kama kitu ni hitaji la maisha basi unapaswa kutumia fedha zako, lakini pia lazima uwe na ukomo kwenye matumizi hayo kwa kuzingatia yale ya msingi pekee.

Mbili; UWEZEKANO WA 100% WA KUPATA FEDHA.

Kigezo cha pili muhimu ni kama kwa kutumia fedha, una nafasi ya kupata fedha zaidi, kwa asilimia 100. Kama kwa kutumia fedha yako kwenye kitu fulani una uhakika wa kupata fedha kwa asilimia 100 basi hayo ni matumizi sahihi.

Maana yake ni kwamba unatumia fedha na inazalisha zaidi. Fedha unayoweka ni kama mbegu ambayo inakuzalishia matunda zaidi.

Hapa lazima pia uwe makini kwa kujipa uhakika wa kupata fedha baada ya kuweka fedha zako.

Mfano ni kuweka fedha yako kwenye biashara au uwekezaji ambao una uhakika wa kupata faida zaidi.

SOMA; Hii Ndiyo Kanuni Rahisi Itakayokuwezesha Wewe Kufikia Uhuru Wa Kifedha Kwenye Maisha Yako.

Tatu; UWEZEKANO WA KUPATA FEDHA.

Kigezo cha tatu ni uwezekano wa kupata fedha lakini siyo wa uhakika wa asilimia 100. Haya ni matumizi ambayo yanaweza yakakuingizia kipato, japo huna uhakika wa kipato hicho.

Matumizi haya yanakuweka kwenye nafasi ya kutengeneza kipato zaidi, japo hujui ni kiasi gani cha hicho kipato unaweza kutengeneza.

Hapa unapaswa kuwa makini ili kujua ni jinsi gani matumizi unayokwenda kufanya yataleta kipato zaidi, hata kama siyo kwa uhakika.

Mfano ni kutumia fedha kwenye kujifunza, kuna uwezekano wa kupata fedha zaidi kama utayatumia yale ambayo umejifunza.

Nne; LABDA UNAHITAJI.

Hapa ni pale ambapo unatumia fedha kwenye kitu ambacho unadhani unakihitaji au utakuja kukihitaji. Hapa hata usipotumia fedha, bado maisha yako yanakwenda vizuri tu.

Watu wengi wamekuwa wananunua vitu ambavyo kwa sasa hawana matumizi navyo, lakini wanajiambia kuna siku watavihitaji. Kinachotokea ni wanakuwa na vitu vingi ambavyo hawavitumii na hivyo fedha zao zinakuwa zimepotea au kukwama sehemu ambapo haziwezi kutumika kwa yale muhimu.

Mfano ni pale unapokutana na kitu kinauzwa kwa bei rahisi na wewe ukanunua kwa sababu unaona hutakuja kukipata kwa bei hiyo wakati unakitaka.

Tano; HUNA UHITAJI KABISA.

Hapa ni pale ambapo unatumia fedha kwenye vitu ambavyo huna uhitaji navyo kabisa. Hapa hakuna tofauti na kupoteza fedha, kwa sababu unakuwa umenunua kitu ambacho huna uhitaji nacho kabisa.

Mfano umetoka nyumbani, hukuwa na ratiba zozote za kununua nguo, na wala hujakosa nguo za kuvaa, lakini njiani ukakutana na mtu anauza nguo na ukaipenda na kununua. Hapo umepoteza fedha kwa sababu hukuwa na uhitaji kabisa wa nguo. Ungekuwa nao ungetoka nyumbani na lengo la kwenda kununua nguo, na siyo kununua kwa sababu umekutana nayo.

Rafiki, katika vigezo hivi vitano, unavyopaswa kutumia ni vitatu vya kwanza.

Kama kitu ni muhimu sana kwa maisha kuendelea basi weka fedha.

Kama kitu kina uhakika wa kutengeneza fedha zaidi weka fedha.

Na kama kitu kina nafasi ya kutengeneza fedha zaidi, angalia uwezo ulionao kisha weka kulingana na uwezo wako.

Vigezo viwili vya mwisho, usitumie fedha yako kabisa, achana navyo kabisa. Kama unajiambia kitu utakihitaji baadaye, subiri mpaka hiyo baadaye, mara nyingi unasahau kabisa. Na kama huna ratiba ya kununua kitu fulani, usikinunue hata kama utakutana nacho, hukihitaji, maana kama ungekuwa unakihitaji ungetoka na kwenda kukitafuta.

Dhibiti sana matumizi ya fedha zako ili uache kujizuia kupiga hatua ya kuelekea kwenye utajiri na uhuru wa kifedha.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge