Tunaweza kusema kwamba sehemu kubwa ya matatizo ya binadamu yanatokana na matatizo ya kifedha. Kinachofanya watu waibe, wafanye uhalifu ni fedha. Na hata kinachofanya watu kufanya kazi kwa muda mrefu na wakati mwingine kulazimika kufanya kazi wasizozipenda ni ili kupata fedha za kukimu mahitaji yao.

f8dc1-fedha2bmkopo

Fedha ni moja ya vitu muhimu sana kwenye maisha ya kila binadamu. Japokuwa kuna kipindi watu hupenda kutumia maneno ya kuonesha kwamba fedha sio muhimu sana, ukweli utabaki pale pale kwamba fedha ni muhimu. Vitu vyote muhimu kwenye maisha vinapatikana kwa fedha. Huduma nzuri za afya, huduma nzuri za elimu, chakula bora na hata maisha bora vyote vinawezekana kwa kuwa na fedha. Hitaji hili kubwa la fedha ndio linafanya watu kuhangaika sana kuitafuta fedha.

Pamoja na kila mtu kuhangaika sana kuitafuta fedha bado kumekuwa na matabaka tofauti kwenye jamii. Kuna tabaka la watu ambao fedha kwao sio tatizo kubwa, watu hawa wameshafikia uhuru wa kifedha. Na pia kuna tabaka jingine ambalo wao maisha yao yanategemea kipato kijacho, kama ni mfanyakazi, maisha yake yote yanategemea mshahara ujao, kama ni mfanya biashara, maisha yake yanategemea faida atakayopata. Tabaka hili la pili bado halijafikia uhuru wa kifedha na ndio lina matatizo mengi sana yanayochochewa na ukosefu wa fedha.

Kwa Bahati mbaya sana sehemu kubwa ya watu wako kwenye tabaka hili la kutokuwa na uhuru wa kifedha. Hawa ni watu ambao wanaweza kuonekana wanafanya kazi sana lakini hawajui fedha zinaenda wapi. Ni watu ambao wanaishi maisha yao kwa kile wanachopata ila miaka inavyokwenda na kufikia umri ambao hawawezi tena kufanya kazi wanajikuta katika hali ngumu sana kifedha.

Leo katika makala hii utapata kujifunza kanuni moja muhimu sana ambayo kama ukiweza kuitumia, baada ya muda utaondoka kwenye matatizo ya fedha uliyonayo sasa. Kanuni hii imetumika karne na karne na imewawezesha watu wengi kufikia uhuru wa kifedha kwa kuanzia chini kabisa.

Fedha haitoshi.

Kwanza kabisa, kabla hatujaingia kujifunza kanuni utakayotumia tunahitaji kujadili jambo moja muhimu sana. Jambo hilo ni kwamba fedha huwa haitoshi, kadiri inavyoongezeka ndivyo matumizi nayo yanaongezeka. Ukitaka kudhibitisha hili angalia wafanyakazi. Eneo moja linaweza kuwa na wafanyakazi tofauti tofauti na wenye viwango tofauti vya mishahara. Lakini inapofika mwisho wa mwezi wote wanakuwa wameishiwa fedha bila ya kujali kiwango cha mshahara wanachopata.

Kadiri fedha inavyoongezeka ndivyo matumizi yanavyoongezeka. Ndio maana hata wafanyakazi wanapoongezwa mshahara, huwa hawaoni thamani kubwa ya ongezeko lile kwa sababu gharama za maisha nazo zinaongezeka.

Ni muhimu sana wewe kujua dhana hii maana utaitumia kwenye kanuni utakayojifunza ili kuhakikisha haikuzuii wewe kufikia uhuru wa kifedha.

Kanuni moja ya kufikia uhuru wa kifedha.

Kanuni muhimu itakayokuwezesha wewe kuondokana na matatizo ya kifedha kwa siku za baadae ni kuweka akiba asilimia kumi ya kipato chako na kisha kuwekeza akiba hiyo kwa muda mrefu. Kwa kanuni hii unapopata kipato, unaondoa asilimia kumi na kuweka pembeni, ni vizuri kuweka sehemu ambayo hutaweza kuifikia kwa urahisi. Kwa hiyo kama kipato chako ni laki tano, unaweka pembeni elfu hamsini, kama ni milioni moja unaweka pembeni laki moja.

Kama utaweka asilimia kumi ya kipato chako kila mwezi na ukaweza kujiwekea nidhamu hii kwa muda mrefu, baada ya muda kuiwekeza akiba hiyo kwenye eneo ambalo linaweza kukuzalishia, utaondoka kwenye matatizo ya kifedha.

SOMA; Maana Halisi Ya Dhana Ya Kujilipa Wewe Mwenyewe Kwanza Kabla Hujafanya Matumizi Ya Fedha Zako.

Kama ni rahisi hivi kwa nini watu hawafanyi?

Tumeona kwamba kanuni muhimu ya kufikia uhuru wa kifedha ni kuweka pembeni asilimia kumi ya kipato chako, rahisi kama hivyo. Lakini mbona watu hawafanyi hivyo? Kwa nini watu wanashindwa kuweka pembeni asilimia kumi ya kipato chao?

KWA NINI SIYO TAJIRI

Hapa kuna sababu nne kubwa kwa nini wengi wanashindwa kutumia kanuni hii na huenda hata wewe zimekuzuia.

  1. Kushindwa kudhibiti matumizi.

Kama tulivyoona hapo juu, fedha huwa haitoshi. Na kadiri kipato kinavyoongezeka, matumizi nayo yanaongezeka. Hali hii imewafanya wengi kujikuta wanatumia kipato chao chote na wanapitiliza mpaka kukopa. Kwa kuwa kwenye madeni inakuwa vigumu kwa mtu kutenga asilimia kumi maana hata hiyo anayopata siyo ya kwake, tayari anadaiwa.

Ili kuepuka hali hii kukuzuia wewe kufikia uhuru wa kifedha hakikisha unapunguza matumizi yote ambayo sio ya msingi. Jiwekee nidhamu ya kutoruhusu matumizi yako kuongezeka tu na kuzidi kipato.

  1. Kuweka akiba baada ya matumizi.

Changamoto kubwa sana inayowazuia wengi kushindwa kuweka asilimia kumi ya kipato chao akiba ni kutokujua ni wakati gani wa kuweka akiba hiyo. Watu wengi wakishapata fedha wanatumia kwanza na kile kinachobaki ndio wanafikiria kuweka akiba. Swali ni je baada ya matumizi unabakiwa na kiasi gani? Haubakiwi na kitu na huenda hata matumizi hayajatosheleza. Hivyo kusema uweke akiba baada ya kumaliza matumizi yako yote ni kujidanganya. Badala yake unapopata kipato chako weka kwanza akiba halafu inayobaki ndio unaiweka kwenye matumizi. Kwa kufanya hivi utaona inakuwa rahisi kwako kukuza akiba yako.

  1. Kuiweka akiba hiyo kwenye matumizi ya baadae.

Kuna wengi ambao wanafanikiwa kuweka akiba lakini tatizo linapokuja kutokea baadae wanaingia kwenye akiba hiyo na kuitumia yote. Hivyo inakuwa rahisi kujiridhisha kwamba aliweka akiba ila matatizo yamemfanya atumie akiba hiyo. Kama na wewe unafikiria hivi hebu nikuulize swali moja, unaponunua nguo, je siku ukiwa na matatizo unaenda kwa aliyekuuzia nguo na kumwambia nipe fedha yangu na uchukue nguo yako kwa sababu nina matatizo? Hapana, hufanyi hivi na sababu ni rahisi sana kwamba tayari umeshamlipa, na ukishalipa fedha hairudi.

Hivi ndivyo unavyotakiwa kufanya kwenye asilimia kumi unayoweka pembeni. Fedha hii hesabu kwamba umemlipa mtu na huwezi kuipata tena, hivyo unapopata matatizo fikiria njia nyingine zote kabla hujaweka wazo lako kwenye eneo hilo.

  1. Kuweka akiba hiyo kwenye eneo ambalo ni rahisi kuifikia.

Changamoto kubwa inayowafanya wengi kushindwa kuweka akiba hii na kuwawezesha kufikia uhuru wa kifedha ni kuiweka eneo ambalo ni rahisi kuifikia na kuitoa. Kama akiba hii umeiweka tu benki ni rahisi sana kufikiria kwenda kuitoa pale unapokuwa na tatizo. Ila kama utaiweka katika mfumo ambao sio rahisi kuitoa, unapopata tatizo utafikiri zaidi na hivyo kupata suluhisho jingine na akiba yako kuendelea kuwepo. Hapo chini utajifunza ni maeneo gani mazuri kuwekeza akiba yako.

SOMA; Vigezo Vitano (05) Vya Kutumia Kufanya Maamuzi Ya Matumizi Ya Fedha Zako.

Ni wapi uwekeze akiba yako?

Mpaka sasa tumeshajifunza hatua ya kwanza muhimu ambayo ni kuweka pembeni asilimia kumi ya kipato chako. Lakini kuiweka tu hii fedha katika hali ambayo haizalishi ni sawa na kuipoteza. Hii ni kwa sababu kadiri siku zinavyokwenda mfumuko wa bei unaongezeka na thamani ya fedha inapungua. Thamani ya elfu kumi miaka mitano iliyopita sio sawa na sasa. Hivyo ili akiba hii unayojiwekea iweze kuwa na tija kwako hapo baadae ni lazima uiwekeze katika shughuli ambazo zitakuletea faida.

Kuna maeneo mbalimbali ambapo unaweza kuwekeza akiba hii, hapa tutajadili matatu muhimu yanayowezekana kwa mazingira yetu ya kitanzania.

  1. Kuwekeza kwenye biashara.

Kama tayari unafanya biashara unaweza kuwekeza kwenye biashara yako ili kuikuza zaidi. Kwa uwekezaji huu utaweza kuitanua biashara yako, kuanzisha matawi zaidi na baadae kuwa kubwa sana na kupata faidia kubwa. Kama upo kwenye ajira unaweza kuangalia biashara unayoweza kuwekeza fedha hiyo, ila jiridhishe kwamba biashara hiyo unaweza kuisimamia vizuri ili usije kupata hasara.

Njia hii ina hatari zake ikiwepo kupata hasara au biashara kufa. Ukifikia hali hiyo maana yake umepoteza akiba yako yote uliyojiwekea. Lakini hili lisikuogopeshe na kukuzuia kufanya, maana hata ukishindwa kuna vitu utakuwa umejifunza.

  1. Kuwekeza kwenye hisa au vipande.

Uwekezaji mwingine unaoweza kufanya kwa akiba yako ni kununua hisa au vipande. Kwa kununua hisa maana yake unakuwa sehemu ya umiliki wa kampuni na hivyo kampuni inapopata faida na wewe mwanahisa unapata faida. Hatari ya njia hii ni kwamba kampuni ikipata hasara na wewe mwanahisa unapata hasara. Kwa kufuatilia makampuni vizuri na kwa ushauri mzuri wa wataalamu unaweza kununua hisa nzuri na zitakazokufaidisha baadae.

Kuwekeza kwenye vipande, unanunua vipande ambapo fedha yako inatumika kwenye uwekezaji mbalimbali. Na kadiri uwekezaji huo unavyoleta faida thamani ya vipande vyako inaongezeka na hivyo kuweza kupata faida pale utakapotaka kuuza vipande vyako.

  1. Kuwekeza kwenye mali.

Aina nyingine nzuri ya uwekezaji ambayo unaweza kuifanya kwa akiba yako ni kuwekeza kwenye mali. Hapa unanunua mali ambazo thamani yake inakua kadiri muda unavyokwenda, na mali hizi ni ardhi na majengo. Unaweza kuweka akiba yako na ikifikia kiwango fulani unakwenda kununua ardhi, au kununua nyumba, au kujenga nyumba kwenye ardhi uliyonunua. Hivi vyote vitakuja kuwa na thamani kubwa baadae na hivyo kukuwezesha kufikia uhuru wa kifedha.

Hii ndio kanuni moja unayoweza kuitumia kujitengenezea uhuru wa kifedha na kuondokana na matatizo mengi. Weka pembeni asilimia kumi ya kipato chako na wekeza akiba hiyo kwenye eneo ambalo linaweza kukuzalishia. Kama utafuatilia vizuri kanuni hii kwa kujiwekea nidhamu kwenye kuweka akiba na kufuatilia uwekezaji uliochagua hakuna kitakachokuzuia kufikia uhuru wa kifedha. Kumbuka haya yote tuliyojadili hapa yatakuchukua muda mrefu, miaka kumi, ishirini mpaka hata hamsini. Kadiri unavyoanza zoezi hili mapema ndivyo utakavyofikia uhuru wa kifedha mapema.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge