“From Rusticus . . . I learned to read carefully and not be satisfied with a rough understanding of the whole, and not to agree too quickly with those who have a lot to say about something.”
—MARCUS AURELIUS, MEDITATIONS, 1.7.3
Tunayo siku nyingine nzuri na ya kipekee sana mbele yetu.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa AFYA, UTAJIRI NA HEKIMA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari JISUKUME KUELEWA KWA KINA…
Unapojifunza kitu chochote kile, usiridhike tu kuelewa kwa juu juu, badala yake jisukume uelewe kwa kina.
Kama umesoma kitu, kisome kwa umakini na uelewe kwa kina kile ulichojifunza, na siyo kusoma haraka ili unalize kusoma.
Kama unamsikiliza mtu, msikilize kwa umakini uelewe kwa kina kile anachosema, na siyo kusubiri amalize kuongea ili na wewe upate nafasi ya kuongea.
Jifunze kwa kina, uliza maswali, jihoji kwa kila unachojifunza kuona umeelewa kwa kiasi gani.
Kwa sababu haina maana kupoteza muda na nguvu zako kujifunza kitu ambacho hukielewi kwa undani na hukifanyii kazi.
Ni bora kujifunza vitu vichache, ukavielewa kwa kina na kufanyia kazi, kuliko kujifunza vitu vingi ambavyo umeelewa juu juu na huvifanyii kazi.
Mstoa Marcus alijifunza hili karibu miaka elfu 2 iliyopita, lakini lina umuhimu mkubwa sana kwa zama tunazoishi sasa kuliko wakati mwingine wowote.
Kwenye zama hizi ambazo vitabu vya kusoma ni vingi kuliko muda wa maisha yako yote, makala za kusoma ni kama mvua, video za kuangalia ni nyingi mno na bado washauri na wanaofundisha ni wengi, watu wamekuwa wanakimbilia kujifunza mengi wawezavyo, lakini wanaishia juu juu, hawazami ndani.
Wewe rafiki, chagua maarifa machache ambayo utazama ndani zaidi, chagua waandishi wachache ambao utazama ndani na uelewe kila wanachofundisha. Chagua walimu wachache ambao utajifunza kila wanachojua na utapata majibu ya maswali na wasiwasi wowote ulionao.
Hii itakusaidia kuondoka na kitu cha kufanyia kazi kwenye kila unachojifunza na maisha yako yatakuwa bora sana.
Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kujifunza kwa kina kwa chochote unachotenga muda wako kujifunza.
#ZamaNdani, #MaarifaNiMengiKulikoMuda, #JifunzeKwaWachche
Wako rafiki katika safari ya kuelekea mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha